Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mke aliyefiwa na mume, watoto watatu ajali ya moto aruhusiwa kwenda kuzika

Mke Aleifiwa Mke aliyefiwa na mume, watoto watatu ajali ya moto aruhusiwa kwenda kuzika

Mon, 24 Jun 2024 Chanzo: Mwananchi

Leo ni siku nyingine ngumu kwa Jasmine Khatibu, aliyefiwa na mume pamoja na watoto wake watatu katika ajali ya moto iliyotokea Jumamosi Juni 22, 2024 jijini Arusha.

Hakuna anayeweza kubashiri mama huyu atasimama vipo muda utakapowadia wa kutoa heshima za mwisho kwa wapendwa wake hao na kushuhudia maziko yao.

Jasmine pamoja na mama mzazi wa marehemu (Zuberi Msemo), Mariam Mussa, ambao walikuwa wamelazwa katika Hospitali ya Rufaa Mount Meru kwa matibabu, wameruhusiwa kwenda kwenye maziko yanayofanyika leo Jumatatu Juni 24, 2024 kwenye makaburi ya familia yaliyoko kijijini kwao Usangi, Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro.

Jasmine amepoteza familia yake katika ajali ya moto iliyotokea Jumamosi, Juni 22, 2024, eneo la Olmatejoo ambayo imesababisha kifo cha mumewe Zuberi Msemo pamoja na watoto wao watatu---Mariam, Salma na Bisma.

Moto huo unadaiwa kusababishwa na kompyuta mpakato (laptop) iliyokuwa imechomekwa kwenye soketi ya umeme na kuunguza kochi.

Mwanamke huyo sasa amebakiwa na mtoto mchanga wa siku sita.

Jasmine Khatibu akiwa kwenye picha ya pamoja na wanawe. Watatu waliocherewa viduara wamefariki dunia katika ajali ya moto pamoja na mumewe.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo, msemaji wa familia, Yahya Msemo amesema Jasmine na mama mkwe wake wameruhusiwa kuhudhuria maziko na wanatakiwa kurudi hospitali baada ya kumalizika maziko hayo.

Awali, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Mount Meru, Dk Kipapi Mlambu, amesema mke na mama wa marehemu wanahitajika kukaa kwa muda hospitali kwa ajili ya tiba ya akili.

"Msiba huu umewashtua, hivyo wanahitaji huduma ya ushauri (counseling), ili kuwarudisha katika hali zao za kawaida," amesema.

Serikali kugharamia mazishi

Katika msiba huo, Serikali imesema inagharamia mazishi pamoja na matibabu ya majeruhi na kukarabati nyumba iliyoungua moto na kuirudisha katika hali yake ya awali.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Felician Mtahengerwa baada ya kufika katika msiba huo na kutoa pole kwa ndugu, jamaa na majirani, sambamba na kuwatembelea majeruhi na kuwapa pole.

Mtahengerwa amesema Rais Samia Suluhu Hassan amepokea taarifa za vifo hivyo kwa mshtuko mkubwa na kutoa pole kwa ndugu, jamaa na marafiki walioguswa na msiba huo.

“Baada ya kupata taarifa hizi za msiba, Rais wetu Samia Suluhu Hassan alitoa maelekezo kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda kwamba aende akajiridhishe na kufanya tathmini ya madhara,” amesema Mtahengerwa na kuongeza:

“Baada ya kupata taarifa, alitoa maelekezo kuwa Serikali itagharamia mazishi yote kuanzia uwekaji wa msiba, ununuzi wa majeneza na kusafirisha miili hadi wilayani Mwanga kuhifadhiwa katika nyumba yao ya milele.”

Mbali na hilo, amesema Serikali itakarabati nyumba yote iliyoungua moto na kuirudisha katika hali ya kawaida.

“Pia tumepokea maelekezo ya majeruhi wote waendelee na matibabu na Serikali itagharamia kila kitu, hivyo sisi kama watendaji wake tuko hapa kusimamia utekelezaji huo kwa ajili ya ndugu zetu hawa," amesema Mtahengerwa.

Ameongeza kuwa wananchi wa Arusha wanapaswa kuchukua tahadhari dhidi ya vifaa vya umeme kama simu, kompyuta, majiko ya umeme na pasi.

"Pale unapomaliza shughuli yako, zima kila kitu na hakikisha mara mbili. Hivyo, niombe kinamama au wasaidizi wa nyumbani wafanye hivyo mara kwa mara kabla ya kulala, lakini pia baba wa nyumba ahakikishe kila kitu kinazimwa ndio alale, la sivyo tutajikuta kila siku tunapoteza nguvu kazi ya Taifa," amesema.

Chanzo: Mwananchi