Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mgogoro waibuka kiwanja cha Msikiti Arusha

Msikiti Arusha Mgogoro waibuka kiwanja cha Msikiti Arusha

Sun, 21 Jul 2024 Chanzo: Mwananchi

Mgogoro umeibuka kati ya Umoja wa Waislamu Arusha (AMU) na Baraza la Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) mkoani hapa kuhusu mradi wa kuendeleza eneo la Msikiti Mkuu wa Ijumaa ulioko katikati ya jiji.

Mbali na eneo la msikiti huo uliopo ndani ya kiwanja namba 478, kitalu H na I, linalodaiwa kumilikiwa na AMU, pia kuna ghorofa nne la Shule ya Sekondari ya Bondeni na maduka.

Hata hivyo, wakati mpango wa ujenzi wa eneo hilo uliokuwa unaratibiwa na AMU ukiwa katika hatua ya uchoraji wa ramani, kumeshuhudiwa kipande cha eneo hilo kikimegwa na kuzungushiwa uzio wa mabati na kuanza kuchimbwa msingi kwa ajili ya ujenzi wa vibanda vya biashara.

Jambo hilo limeonekana kuwakera baadhi ya waumini na kuamua kuzungumza na vyombo vya habari wakimuomba Rais Samia Suluhu Hassan aingilie kati suala hilo.

Akizungumza kwa niaba ya AMU leo Jumapili Julai 21, 2024, Sheikh Aziz Bashir amesema eneo hilo limewekwa wakfu kwa ajili ya kufanyia ibada, hivyo wameutaka uongozi wa Bakwata kuheshimu kanuni na taratibu hizo walizozikuta tangu wakati unajengwa msikiti huo maarufu Msikiti wa Bondeni mwaka 1967.

“Huu msikiti ulikuwa ndio mkubwa Tanzania na Afrika Mashariki enzi hizo, ndiyo maana hadi leo viongozi wakuu wa nchi wanaswali hapa, kwa sasa umekuwa mdogo, tunataka kujenga mwingine, tunashangaa viongozi wa Bakwata kuja kuharibu mazingira yetu, kukata miti na kuweka uzio,” amedai Sheikh Bashir.

“Kwa sasa tumewazuia mafundi, hakuna kuendelea na ujenzi, tunamuomba Rais aingilie kati suala hili, la sivyo tutaiburuta Bakwata mahakamani wakiendelea na ujenzi. Pia, tutadai mali zetu zote sambamba na mapato na matumizi hata ya miradi iliyopo ya shule na maduka kwa kuwa haitunufaishi kwa chochote.”

Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu kuhusu madai hayo, Katibu wa Bakwata Mkoa wa Arusha, Seif Banka amesema ujenzi unaofanyika katika eneo hilo ni kwa ajili ya maduka, lengo ni kuongeza mapato ya msikiti huo.

Amesema kwa sasa hawezi kuzungumzia zaidi jambo hilo kutokana na sintofahamu iliyopo katika kufanikisha mradi huo.

“Ni mradi kama miradi mingine ya kuongeza mapato, lakini kwa sasa kuna mambo yameingilia kati ambayo siwezi kuyasema, naomba unitafute baada ya siku mbili au tatu, tutazungumza kwa undani wake,” amesema Seif.

Sheikh wa Mkoa wa Arusha, Shaaban Bin Juma amesema waliazimia kuwekeza vitega uchumi katika eneo hilo, lakini kwa sasa wamesitisha kwa muda.

“Kwa sasa kuna vikao vya ndani vinavyoendelea kujadili suala hili, tutakapokuwa tayari tutawajulisha,” amesema Sheikh Juma.

Wakizungumza mgogoro huo, baadhi ya waumini wamesema tayari walishapata wafadhili wa kusaidia ujenzi eneo hilo na mchoro umefanyika, wanachosubiri ni majibu ya vipimo vya udongo ili kuanza ujenzi.

Mmoja wa waumini wa msikiti huo, Zuberi Ally amesema msikiti ni taasisi inayopaswa kushughulikia maendeleo ya imani na elimu na sio miradi ya kuvuruga mahali patakatifu, hivyo wako tayari kulipeleka suala hilo mahakamani kwa ajili ya kupigania eneo hilo muhimu.

Mkazi mwingine wa Arusha, Aisha Jumanne amesema: “Msikiti ni eneo nyeti linalotakiwa kuwa na majengo ya kufanyia ibada na pengine sehemu za kutoa elimu kama madrasa au shule za elimu dunia na mbinguni ili kuwajenga vijana kiakili na sio vinginevyo, sio vurugu.”

Mwananchi imetembelea eneo la msikiti huo na kushuhudia kiwanja kikiwa kimezungushiwa uzio wa mabati pamoja na kibao cha kibali cha ujenzi wa maduka chenye namba 163/2023 huku msingi wa ujenzi ukiwa umeanza kujengwa.

Chanzo: Mwananchi