Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mapya watoto wawili waliopotea Arusha, baba atajwa

Mapya Arushaaaaa Mapya watoto wawili waliopotea Arusha, baba atajwa

Fri, 26 Jul 2024 Chanzo: Mwananchi

Jeshi la Polisi mkoani Arusha linamsaka mtu mmoja anayejulikana kwa jina moja la Maiko, ambaye ni baba wa watoto wawili wanaodaiwa kupotea Arumeru mkoani Arusha, akituhumiwa kuhusika na tukio hilo.

Hayo yamebainika baada ya kusambaa kwa taarifa za kupotea kwa watoto wawili – Mordekai Maiko (7) na Masiai Maiko (9), wanafunzi wa Shule ya Msingi Olosiva iliyoko Arumeru mkoani Arusha. Watoto hao walipotea Julai 24, 2024, na taarifa zilisambaa jana, Julai 25, 2024, baada ya kutoonekana ndani ya saa 24 kama ilivyoelekezwa na Jeshi la Polisi.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha, SACP Justine Masejo, amesema leo, Ijumaa Julai 26, 2024, kuwa katika upelelezi wa awali wamemshuku baba wa watoto hao kuwa huenda anahusika na tukio hilo.

“Bado upelelezi unaendelea wa kuwapata watoto hao, lakini kwa hatua za awali, tunamtafuta baba yao kwanza kujiridhisha, baadaye tutatoa taarifa iliyokamilika,” amesema Kamanda Masejo.

Amesema sababu ya kumshuku baba huyo ni kutokana na kujirudia kwa tukio hilo kama ilivyowahi kutokea mwaka mmoja uliopita. “Tunamshuku baba huyo, kwa sababu si mara ya kwanza watoto hawa kudaiwa kupotea,” amesema Masejo.

“Mwaka jana, watoto hawa walidaiwa hivyo hivyo kupotea na katika kuwatafuta tukawakuta wako salama na baba yao wilayani Karatu, hivyo kwa sasa tunashuku kuwa itakuwa hivyo hivyo,” amesema Masejo.

Akizungumzia tukio hilo, mama wa watoto hao, Elizabeth Modesta (31), amesema hata yeye amepata taarifa za minong'ono kutoka kwa watu wa karibu na ndugu wa aliyekuwa mume wake kuwa baba yao amewachukua na kuvuka nao kwenda Kenya.

“Kwa taarifa inavyoonekana, baba yao ndiye kawachukua na kwenda nao nyumbani kwao huko Kenya anakoishi kwa sasa, baada ya mimi na yeye kutengana,” amesema Elizabeth.

Elizabeth ametumia nafasi hiyo kuiomba Serikali kumsaidia kurudisha watoto wake kwani hawezi kuishi nao mbali badala yake watatengeneza utaratibu wa wazazi wote wawili kuwaona watoto wao.

“Mimi ninachoomba nisaidiwe watoto wangu warudi na kama atakuwa anataka kuwaona basi atawachukua kipindi cha likizo na kuwarudisha kwa ajili ya shule, lakini siwezi kuishi bila wanangu,” amesema Elizabeth.

Mmoja wa majirani ambaye hakutaka kutajwa jina lake, amesema wawili hao walishindwa kuelewana kwa muda mrefu baada ya kupata mtoto wa pili, hivyo kila mmoja kuishi kivyake bila mawasiliano.

“Baba wa watoto amekuwa akiomba hata kuwachukua watoto wake kipindi cha likizo akae nao, lakini mama amekuwa akikataa. Nadhani ndiyo sababu amekuwa akiwaiba “kwa nia njema ya mapenzi kwa watoto wake” na kuwarudisha,” amesema jirani huyo.

Awali akizungumza na Mwananchi, Elizabeth alisema aliagana na watoto hao na kuwapandisha daladala kwenda shule, lakini hawakurudi na alipofuatilia shuleni ilibainika pia hawakufika, hivyo akatoa taarifa polisi.

Chanzo: Mwananchi