Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kanisa Katoliki lamsimamisha padri anayetuhumiwa mauaji ya Asimwe

Padriiiii Padri Elipidius Rwegoshora (picha kubwa) aliyesimamishwa uchungaji kwa tuhuma za mauaji ya Asimwe

Fri, 21 Jun 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Kanisa Katoliki Jimbo la Bukoba limemsimamisha kutoa huduma za kichungaji Padri Elipidius Rwegoshora kufuatia tuhuma zinazomkabili za kuhusika katika mauaji ya mtoto mwenye ulemavu wa ngozi, Asimwe Novart.

Askofu wa Jimbo Katoliki Bukoba, Jovitus Mwijage ametangaza uamuzi huo kupitia gazeti la Kiongozi linalotolewa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), toleo lake la Juni 21 -27, 2024

Gazeti hilo limemnukuu Askofu Mwijage akikiri kuwa mtuhumiwa ni padri wa jimbo lake na amemsimamisha kutoa huduma zote za kichungaji mpaka hapo suala lake litakaposhughulikiwa na vyombo vya sheria.

“Tunahuzunishwa na taarifa ya mauaji ya Asimwe, kwani sisi kama Kanisa Katoliki ni walinzi wa kwanza wa uhai wa wanadamu. Tunaiombea familia yake na kuiombea roho yake ipate pumzio la amani mbinguni.

“Hata hivyo, tumesikia taarifa ya watuhumiwa na mmojawapo akiwa ni Padri Rwegoshora. Ni kweli padri huyo ni wa jimbo Katoliki Bukoba na tumechua uamuazi wa kumsimamisha kutoa huduma zote za kichugaji mpaka hapo suala lake litakaposhughulikiwa na vyombo vya sheria.

“Baada ya vyombo vya sheria kumaliza kazi yake, ndipo taratibu nyingine za kanisa zitafuata,” amesema Askofu Mwijage.

Asimwe menye umri wa miaka miwili na nusu alinyakuliwa mikononi mwa mama yake na watu wasiojulikana Mei 30, 2024 katika Kijiji cha Bulamula, Muleba mkoani Kagera.

Mwili wa mtoto huyo ulipatikana Juni 17, 2024 akiwa ameuawa kikatili kwa kukatwa baadhi ya viungo vyake, kisha kutupwa kwenye kalavati katika barabara itokayo Luhanga kwenda Makongora wilayani Muleba.

Taarifa kutoka Jeshi la Polisi nchini kupitia Msemaji wake, David Misime iliyotolewa Juni 19, 2024 iliwataja watuhumiwa tisa wa mauaji hayo akiwamo Padri Rwegoshora ambaye ametajwa kuwa ni paroko msaidizi wa Parokia ya Bugandika.

Watuhumiwa wengine ni pamoja na baba wa mtoto huyo, Novart Venant, mganga wa jadi Desdeli Evarist mkazi wa Nyakahama, Faswiru Athuman, Gozibert Alkadi, Rwenyagira Burkadi mkazi wa Nyakahama wote wakazi wa Nyakahama.

Wengine ni Selemani Selestine na Nurdin Hamada, wakazi wa Kamachumu pamoja na Dastan Kaiza, mkazi wa Bushagara.

Taarifa ya Polisi inasema Padri Rwegoshora anatuhumiwa kumshawishi baba mzazi wa marehemu kufanya biashara ya viungo vya binadamu na kwamba yeye ndiye aliyemtafuta mganga wa jadi na kulipia gharama zote za uganga.

Chanzo: Mwanaspoti