Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Fichueni wanaoingiza Dawa za Kulevya Tanga

Dawa Za Kulevya Ajisaidia.png Dawa za kulevya

Fri, 21 Jun 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Serikali mkoani Tanga imesema ipo macho kuwachukulia hatua watu wanaojihusisha na uingizaji wa dawa za kulevya katika wilaya ya Tanga.

Katibu Tawala wa Wilaya ya Tanga, Dalmia Mikaya amesema hayo leo Juni 21, 2024 wakati wa hotuba yake katika maadhimisho ya Siku ya Kupinga Dawa za Kulevya Duniani, yaliyofanyika kiwilaya kwenye Kituo cha Afya Mikanjuni.

Dalmia aliyekuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho hayo, amesema Tanga imeonekana kuwa kinara wa waraibu wa dawa za kulevya na ameitaka jamii kutoa ushirikiano kwa vyombo vya ulinzi na usalama kupambana na hali hiyo.

"Tuache kutumia dawa za kulevya kwa rika zote kwani zinaleta athari na kupoteza nguvu kazi ya Taifa. Nawahamasisha wale waraibu waliofanikiwa kuacha matumizi ya dawa za kulevya, waanze kufanya shughuli za ujasiriamali kwa kuwa Serikali imewatengenezea mazingira wezeshi," amesema Mikaya.

Mganga Mkuu wa Jiji la Tanga, Dk Stephen Mwandambo amewapongeza wadau mbalimbali kwa kuelimisha jamii kupitia vyombo vya habari, shule, taasisi za dini na makongamano ya kisiasa juu ya athari za dawa za kulevya, kiuchumi na kimazingira.

Maadhimisho ya mwaka huu kitaifa yatafanyika Mwanza chini ya kaulimbiu inayosema, 'Wekeza kwenye kinga na tiba dhidi ya dawa za kulevya'.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live