Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wapinzani waeleza matumaini uchaguzi Serikali za mitaa

Kuraaa.png Wapinzani waeleza matumaini uchaguzi Serikali za mitaa

Fri, 16 Aug 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Viongozi wa vyama vya siasa nchini wameeleza matumaini yao kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 27, 2024, wakisema unatarajiwa kuwa bora kuliko wa mwaka 2019 kutokana na maboresho kadhaa, ikiwemo ushirikishwaji wa wadau katika mchakato wa maandalizi.

Mwenyekiti wa Chama cha NCCR Mageuzi, Haji Khamis Ambari akizungumza baada ya kutolewa kwa tangazo la uchaguzi huo, leo Alhamisi Agosti 15, 2024 amesema tofauti na uchaguzi wa mwaka 2019 ambapo vyama vya siasa havikushirikishwa kikamilifu, mwaka huu kumekuwa na ushirikiano wa karibu tangu hatua za awali za uandaaji wa kanuni.

"Kuna maboresho mengi yaliyofanyika mwaka huu. Kwa mfano, zamani ilikuwa mgombea mmoja anapita bila kupingwa, lakini sasa mfumo huo umeondolewa. Pia, wasimamizi wa uchaguzi sasa wanaombwa kuteuliwa, badala ya kuchaguliwa kienyeji," amesema Ambari.

Kwa sababu ya maboresho haya, Ambari ameeleza wana imani kubwa kuwa uchaguzi wa mwaka huu utakuwa huru na wa haki.

Ameendelea kusisitiza kuwa Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye ni msimamizi mkuu wa nchi, ameahidi kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa uadilifu, hivyo wanatarajia mabadiliko hayo yatatekelezwa kwa vitendo.

Ushirikiano na maandalizi ya wagombea

Katibu Mkuu wa chama cha UDP, Saum Rashid, alikubaliana na viongozi wenzake kuhusu maboresho ya kanuni za uchaguzi.

Amesisitiza umuhimu wa vyama vya siasa kuhakikisha wagombea wao wanaelewa ratiba na taratibu za uchaguzi, ili kuepuka changamoto zinazoweza kuzuilika.

"Ni muhimu sisi kama viongozi kutoa mwongozo kwa wanachama wetu ili wawe na uelewa mzuri wa ratiba na taratibu za uchaguzi.

“Hii itasaidia kuepuka manung’uniko na vurugu zisizo za msingi ambazo hutokea pindi mchakato unapokuwa umekamilika," ameeleza Saum.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa chama cha CUF, Profesa Ibrahim Lipumba ameeleza uchaguzi uliopita ulikumbwa na kasoro nyingi, zikiwemo kuenguliwa kwa wagombea wengi, jambo ambalo lilisababisha malalamiko.

Hata hivyo, Profesa Lipumba ameeleza matumaini yake kuwa uchaguzi wa mwaka huu utafuata misingi ya haki kwa kuhakikisha matakwa ya wananchi yanaheshimiwa na kura zinahesabiwa kama zilivyopigwa.

"Tutashiriki kikamilifu katika uchaguzi huu. Ingawa tungependa Tume Huru ya Uchaguzi isimamie, tunawahamasisha wanachama wetu kujitokeza kwa wingi na kushiriki," amesema Profesa Lipumba.

Wito wa kujitokeza

Naibu Katibu Mkuu CCM Bara, John Mongella amewahimiza Watanzania kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi za uongozi, akisisitiza kuwa ni haki yao ya kikatiba.

Ameongeza kuwa uchaguzi ni fursa muhimu ya kuwachagua viongozi bora watakaoendeleza amani na maendeleo nchini.

"Rais Samia Suluhu Hassan ameanzisha falsafa ya 4R, ambayo inalenga kudumisha amani, utulivu na kuimarisha utengamano wa Watanzania, sambamba na kuharakisha maendeleo ya nchi yetu," amesema Makala.

Amesema CCM kama chama tawala, kinatambua umuhimu wa demokrasia na amani katika maendeleo ya nchi, na kitaendelea kuwa mstari wa mbele kuhakikisha haki na uhuru vinatawala katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live