Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vijana wafunga ofisi ya Katibu UVCCM Mufindi

Katibu Uvccm Vijana wafunga ofisi ya Katibu UVCCM Mufindi

Thu, 6 Jun 2024 Chanzo: Mwananchi

Umoja wa vijana wa CCM (UVCCM) Wilaya ya Mufindi, mkoani Iringa wamefunga ofisi ya umoja huo wakilalamika kutoridhishwa na utendaji kazi wa Katibu wao, Aizaki Mbuya.

Vijana hao wamefanya shughuli hiyo wakiongozwa na Mwenyekiti wao, Christian Mahenge.

Hata hivyo, Mahenge ametakiwa kufika kwenye kikao cha Kamati ya Maadili ya CCM Wilaya ya Mufindi, kueleza kwa nini wamechukua hatua hiyo.

Akizungumzia tukio hilo, Mahenge amemtuhumu Mbuya kuwa amekuwa akishindwa kutekeleza majumu yake ipasavyo huku fedha za umoja huo zikitafunwa.

Aidha Mahenge amesema umoja huo una miradi mingi lakini fedha zinazokusanywa zimekuwa zikitumika vibaya.

“Mfano tuna mradi mchanga kata ya Rungemba katika vikao tulikubaliana fedha za mradi huu ziingizwe kwa ‘control’ namba ili ziweze kuonekana lakini zimekuwa zikichukuliwa mikononi," amesema mwenyekiti huyo na kuongeza;

"Pamoja na mradi wa kuosha magari ambao unaingiza fedha nyingi lakini hazionekani," amesema Mahenge.

Mbali na hilo, Mahenge amesema wameamua kufunga ofisi hiyo ili kuonyesha kuwa hawawezi kufanya kazi naye.

“Tumefunga ofisi hatumuhitaji Katibu, watuletee mwingine ambaye ataweza kutetea masilahi ya vijana," amesema Mahenge.

Mjumbe wa Baraza Kuu la UVCCM Mkoa wa Iringa, Gasto Mdemu amesema imetokea sintofahamu ya namna ya utekelezaji wa majukumu ya ofisi hiyo kutoka na vijana kuwa na manung’uniko makubwa huku vikao vikiitwa kwa nadra," amesema.

Naye Mwenyekiti wa vijana kata ya Saohill, Diana Mtepa wameungana na mwenyekiti huyo kufunga ofisi hiyo huku wakiwa na sababu ya kufanya kwa jambo hilo.

“Mwenyekiti wetu amekuwa akifanya jitihada za kutafuta fursa mbalimbali za vijana lakini katibu amekuwa akitengeneza mazingira ambayo yanasababisha vijana hao kuzikosa.”amesema Diana.

Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Mufindi, Christian Mahenge akielezea sababu za kufunga ofisi ya Katibu wao.

Akizungumzia tuhuma hizo dhidi yake, Mboya amesema UVCCM na CCM ina vikao vya msingi vinavyoweza kujadili suala hilo.

Akizungumza na Mwananchi Katibu wa CCM, Wilaya ya Mufindi, Clemence Bakuli amekiri kutokea kwa tukio hilo na kwamba chama hicho kimeshachukua hatua.

Amesema tayari Mahenge ameitwa kwenye kikao cha kamati na maadili ya chama hicho kujibu sababu zilizofanya wafunge ofisi.

“Tukio tumelipata lakini hatujajua sababu ndio maana hapa nipo naandaa barua za kuwaita kesho kwenye kikao cha maadili ili waweze kueleza sababu ambazo zimefanya wao kufunga ofisi ya katibu huyo,"amesema Bakuli.

Hata hivyo mpaka taarifa hii inakwenda mtamboni bado ofisi hizo zimefungwa na utepe.

Chanzo: Mwananchi