Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tundu Lissu aibuka tena na mikataba ya Bandari

Tundu Lissu Chato Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu.

Wed, 25 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, amesema kuna haja mikataba ya uwekezaji na uendeshaji wa Bandari ya Dar es Salaam kuwekwa wazi kwa Watanzania ili kila mwananchi aisome.

Lissu ambaye kitaaluma ni mwanasheria, ametoa kauli hiyo ikiwa ni siku moja baada ya Serikali ya Tanzania na Mamlaka ya Dubai kupitia Kampuni ya DP World kutia saini mikataba mitatu ya uwekezaji na uendeshaji bandari hiyo.

Mwanasiasa huyo alitoa kauli hiyo alipozungumza na Jumuiya ya Watanzania wanaoishi Columbus, Ohio nchini Marekani.

Alisema kwa kuwa serikali imeeleza kwamba ilizingatia maoni ya Watanzania yaliyotolewa awali kuyaweka katika mkataba huo, ni vyema mkataba ukawekwa hadharani ili kila mwananchi ausome.

“Serikali imetuambia kwamba maoni ya wananchi katika mkataba huo yamezingatiwa. Kwa hiyo, hayo maneno mazuri ambayo tumeambiwa kwamba mawazo yamezingatiwa ni vyema yakawekwa wazi kuonesha mikataba yenyewe kwa uthibitisho zaidi ili kila mwananchi aone na asome kila kitu kilichomo katika mikataba kwa uwazi zaidi.

“Na ninasema ni vyema kufanya hivyo kwa sababu hili jambo lina uzito mkubwa na lilivuta hisia za wengi. Kwa hiyo, ili kuleta imani kwa wengi waliokuwa na wasiwasi tangu awali, ni vyema (mikataba) ikawekwa wazi.

“Nilikuwa ninafuatilia ile hafla wakati mikataba hiyo inatiwa saini, lakini sikuona hata nakala moja ambayo ilitolewa kwa watu ili wasome. Tunataka waiweke wazi na sisi tusome. Kuna msemo unasema ‘seeing is believing’ (kuamini ni kuona), tunataka tuone!” Lissu alisisitiza.

Katika hafla ya utiaji saini mikataba hiyo iliyofanyika juzi Ikulu mkoani Dodoma, mikataba iliyotiwa saini ni wa nchi mwenyeji, wa upangishaji ardhi na wa uendeshaji gati namba nne hadi saba katika Bandari ya Dar es Salaam.

Mikataba hiyo ilitiwa saini kutokana na kukamilika mazungumzo ya pande hizo mbili pamoja na kutiwa saini kwa makubaliano kati ya Serikali ya Tanzania na Mamlaka ya Dubai kuhusu uwekezaji (IGA) Oktoba 24 mwaka jana.

Hata hivyo, makubaliano ya pande hizo mbili yalikosolewa na wadau mbalimbali, hata baadhi ya wakosoaji kutishia kuitisha maandamano nchi nzima, lakini Serikali ya Tanzania ikasisitiza mkataba huo utakuwa na manufaa makubwa kwa nchi.

Rais Samia Suluhu Hassan, akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini juzi, alisema maslahi ya nchi katika mikataba hiyo yamezingatiwa na hakuna sauti iliyopuuzwa, huku akisisitiza kwamba sheria za Tanzania zitatumika katika utekelezaji mikataba hiyo.

Kwa mujibu wa Zuhura Yunus, Mkurugenzi wa Mawasiliano Ofisi ya Rais, Ikulu, mikataba hiyo mitatu imetiwa saini kwa kuzingatia kifungu cha 2 cha Sheria ya Ubia Na. 6 ya Mwaka 2023 na Kifungu cha 2 cha Sheria ya Ununuzi wa Umma Na. 5 ya Mwaka 2023.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: