Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sugu aanza kazi rasmi Nyasa

Sugu Kazini Nyasa Sugu aanza kazi rasmi Nyasa

Thu, 6 Jun 2024 Chanzo: Mwananchi

Mwenyekiti wa Kanda ya Nyasa ya Chadema, Joseph Mbilinyi (Sugu) ameanza kazi rasmi kwa kufungua kikao cha kanda hiyo, huku akieleza utekelezaji wa ahadi yake ya kuje ga ofisi ya kanda hiyo.

Sugu alishinda uchaguzi wa kanda hiyo akimwangusha aliyekuwa Mwenyekiti wa kanda hiyo, Peter Msigwa katika uchaguzi uliofanyika Mei 30, 2024 mkoani Njombe.

Tayari Msigwa ameshatangaza kukata rufaa katika Kamati Kuu ya Chadema kupinga matokeo hayo.

Akiandika katika ukurasa wake wa X jana Juni 5, 2024, Sugu amesema kikao hicho kimehusisha viongozi wote wa juu wa kanda hiyo.

"Leo (jana) nimeongoza kikao kazi cha kwanza Kanda ya Nyasa, viongozi wote wa juu wameshiriki yaani makamu mwenyekiti, katibu na mtunza hazina pamoja na wenyeviti wa mabaraza ya Bazecha, Bawacha na Bavicha," amesema.

Kuhusu ujenzi wa ofisi ya Kanda, Sugu amesema mchakato umeanza.

"Mtakumbuka tulisema tutaanza baada ya siku saba tangu siku ya uchaguzi na leo ni siku ya saba.

Mchakato wa ujenzi umeshaanza kwenye kikao cha leo. Tumekubaliana tupeleke kwenye kamati tendaji ambayo itakaa Jumatano Juni 12, kule kamati tendaji ndio itaunda kamati ya ujenzi," amesema Sugu kupitia video aliyoweka X.

Amesema katika mchakato huo kutakuwa na kamati ya ujenzi na kamati ya fedha.

"Tumeona suala hili hatuliwezi sisi viongozi wakuu wachache ndiyo maana tumelipeleka kamati tendaji ili kupata baraka pana za chama," amesema.

Chanzo: Mwananchi