Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Msigwa anavyoongeza joto ubunge CCM Iringa Mjini

Msigwaaa 017 Msigwa anavyoongeza joto ubunge CCM Iringa Mjini

Wed, 3 Jul 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Uamuzi wa mbunge wa zamani wa Iringa Mjini (Chadema), Peter Msigwa kujiunga na CCM, umeonyesha sura mbili za mwanasiasa huyo, aliyekuwa mwiba kwa chama hicho tawala kutokana na maneno yake ya ukosoaji.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, mbunge wa zamani wa Iringa Mjini (Chadema), Peter Msigwa alipokelewa kama mwanachama mpya wa CCM baada ya kuamua kuachana na chama chake cha Chadema alichokitumikia kwa zaidi ya miaka 20.

Kuhamia kwa Msigwa CCM, siyo tu kumenogesha siasa za vyama vingi, bali pia kumeongeza joto la kisiasa katika jimbo la Iringa Mjini kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 endapo ataamua kuwania nafasi yake ya zamani.

Kwa sasa jimbo la Iringa Mjini linakaliwa na Jesca Msambatavangu (CCM) ambaye alimshinda Msigwa kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 na kuhitimisha miaka 10 ya ubunge wa Msigwa katika jimbo hilo.

Mahasimu hao kwenye uchaguzi uliopita, sasa wako kwenye chama kimoja na endapo wote wataonyesha nia ya kugombea ubunge kwenye jimbo la Iringa Mjini kupitia chama hicho tawala, basi mchuano utakuwa mkali.

Msambatavangu ambaye ni miongoni mwa wanawake wachache walioshinda uchaguzi kwenye majimbo, ana nguvu yake katika jimbo la Iringa Mjini. Msigwa naye anaongeza ushindani katika kumkabili mbunge huyo kwenye uchaguzi ujao.

Hata hivyo, wajumbe wa CCM katika jimbo hilo wataamua kumsimamisha wamtakaye na kamati Kuu ikiona inafaa itaheshimu uamuzi wa wajumbe au kupendekeza jina la mtu mwingine kwa kadiri itakavyoona inafaa.

Mwananchi limemtafuta Msigwa na kumuuliza kama atagombea ubunge kwenye uchaguzi ujao kupitia chama chake kipya, hata hivyo, hakuwa tayari kuweka wazi akidai kwamba kwa sasa amejielekeza kwenye ujenzi wa chama.

Msigwa anasisitiza kwamba hiyo sio dhamira yake, kikubwa kilichompeleka CCM ni kuleta mabadiliko katika nchi.

“Hayo mengine tutajengea daraja tutakapofika, kama nitaona ni mwafaka kufanya hivyo, nitafanya na chama kikiona nafaa, kikanipa nafasi hiyo, nitasimama. Lakini kwa sasa focus (lengo) ni kukijenga chama na kuwaaminisha wananchi, hao wanaopitapita huko barabarani na kukosoa, sio kweli,” anasisitiza mwanasiasa huyo.

Msambatavangu afunguka

Akizungumzia ujio wa Msigwa ndani ya CCM, mbunge wa Iringa Mjini (CCM), Jesca Msambatavangu anasema anafananisha kitendo hicho na usajili uliofanywa na Yanga kumsajili Clatous Chama kutoka Simba.

“Kama mshindani wako alikuwa timu ya pili na amehamia kuja pande wako, hakuna shida, naona amekuja kuongeza nguvu. Kama leo Yanga wamemsajili Chama kutoka Simba, amekuja kuongeza nguvu, hakuna ubaya hapo,” amesema.

Jesca katika maelezo yake anasema uwezo aliokuwa anaouonyesha upande aliokuwepo, anakwenda kuufanya CCM huku akieleza watakuwa wanapambana pamoja kwa kuwa wanaunganishwa na chama.

“Chama si mali ya mtu mmoja, bali kinahusisha wanachama na uwezo wa mtu hauwezi kukizidi chama na katika taasisi kama chama kunakuwa na talenti tofauti tofauti,” anasema mwanasiasa huyo.

Msambatavangu anasema CCM ni chama kikubwa, kina nguvu na umaarufu na kila anayedhubutu kujiunga na chama hicho kama Msigwa ananufaika huku akieleza kwa uzoefu wa Msigwa, anaamini wamepata askari mzuri wa kuongeza nguvu.

Anasema Msigwa kuhamia CCM,hajapoteza chochote huku akibainisha siasa si ugomvi na yupo tayari kufanya naye kazi pamoja katika kuwaletea maendeleo wananchi wa Iringa.

“Amekuja CCM, nipo tayari kufanya naye kazi katika kuwaletea wananchi maendeleo na hakuna ubaya wowote,” anasema mbunge huyo.

Wachambua joto hilo

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Iringa, Jimson Sanga anasema ikiwa Mchungaji Msigwa atawania ubunge katika jimbo la Iringa Mjini, ataleta ushindani mkubwa kati yake na mbunge wa sasa, Msambatavangu.

Anasema wakati bado yupo Chadema, alikuwa tishio kwa CCM, hivyo kuhama kwake kumewalegeza nguvu lakini kumewaongezea ushindani.

“Kwa hiyo, ushindani utakuwa kwa hao wawili, hata hivyo CCM wakimsimamisha Msigwa, nje ya chama bado watakuwa na nafasi nzuri,” anasema Sanga.

Mchambuzi wa siasa mkoani Iringa, Paul John anasema kuna uwezekano kwa kiongozi huyo kutokubalika kwenye siasa za nje ya CCM kwa sababu anaonekana kama msaliti.

“Kama atasimama kugombea Iringa kupitia CCM inawezekana jamii ikamkataa japo ndani ya chama hicho, atasababisha ushindani na huenda makundi ya ubunge 2025 yameanza kuparuana,” anasema John.

Mkazi wa Iringa Mjini, Stella Myovela anasema anatamani kuona mpambano utakaokuwepo kwenye uchaguzi ujao kwani anawafahamu wanasiasa hao na wote wana nguvu na wamekuwa wabunge kwenye jimbo hilo.

“kama wote watachukua fomu, nadhani kamati kuu ndiyo itaamua nani akiwakilishe chama. Wote ni maarufu na wana wapigakura wao, mtihani ni nani aachiwe kijiti apeperushe bendera ya CCM hapa Iringa Mjini,” anahoji kada huyo wa CCM.

Anaongeza kwamba muda ukifika ndiyo utaamua na hapo ndiyo wananchi watajua kama wote wanakusudia kuwania ubunge kwenye jimbo hilo au la. Hata hivyo, anasisitiza kwamba wanaIringa wanataka mtu atakayewaletea maendeleo.

Akiwa na mtazamo tofauti, meya wa zamani wa manispaa ya Iringa (Chadema), Alex Kimbe anasema kuondoka kwake ndani ya chama hicho hakuna pengo isipokuwa amewaumiza wananchi waliokuwa wanamuunga mkono na kuwa mbunge kwa miaka 10.

“Hali hiyo imemfanya kubadilisha mawazo kwa kuwa hana sehemu ya kushikilia kwa sababu ngazi ya kanda hana nafasi, mkoa hata wilaya, ingawa kidogo alikuwa na nafasi kwa baadhi ya watu waliopita katika jimbo lake,” anasema.

Anasema Msigwa ni miongoni mwa watu wenye kupenda madaraka siku zote na alichokifanya ni kuchanga karata zake kuwaaminisha CCM kwamba bado ana nguvu ya kujenga hoja kwenye ulingo wa kisiasa.

“Hata akipewa nafasi ya kuja kugombe hapa Iringa, hawezi kushinda kwa sababu amefanya usaliti mkubwa, walimpa kura na alikuwa mbunge miaka 10, inakuwaje anahamia upande wa pili ghafla,” anasema Kimbe.

Anasema kingine kilichomkimbiza Msigwa ni kuwa na mivutano na baadhi ya wanachama akiwemo yeye, baada ya kuonyesha nia ya kugombea nafasi ya ubunge mwaka 2020 kukiwakilisha chama hicho.

“Mvutano wetu ulikuwa wa mwaka mmoja na nusu hivi, tulikuwa hatusalimiani na baada ya kuona nafasi yake kichama ya kugombea ubunge ni ndogo baada ya kubaini Sugu anataka kuweka safu yake,” anasema Kimbe.

Kimbe anabainisha kuwa hata katika nafasi ya mkoa, bado hakuwa na uwezo wa kupenya na hali hiyo imekuwa ikimtia hofu kwa sababu viongozi wengi ambao haelewani nao ni wafanya uamuzi kwenye kura za maoni.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live