Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Msigwa aibua mapya Chadema, wenyewe wamjibu

Peter Msigwa CCM.jpeg Mchungaji Peter Msigwa

Sun, 21 Jul 2024 Chanzo: Mwananchi

Mbunge wa zamani wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa ameeleza sababu za kukihama chama hicho na kutimkia Chama cha Mapinduzi (CCM) kuwa ni pamoja na kutafuta demokrasia.

Pia amedai sababu nyingine ni ufisadi ndani ya Chadema akidai mwaka 2015, wabunge wa chama hicho walichangishwa fedha zaidi ya Sh2 bilioni ambazo hadi sasa hazijulikani zilipo.

Msigwa amebainisha hayo jana Jumamosi Julai 20, 2024 mjini Iringa kwenye mkutano wa hadhara wa CCM na alitumia nafasi hiyo kueleza sababu za kuhamia kwenye chama hicho.

Mwanasiasa huyo alihama Chadema Juni 30, 2024 na kuhamia CCM ambapo alipokelewa na Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Samia Suluhu Hassan wakati wa kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC) kilichofanyika Ikulu, Dar es Salaam.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Msigwa amesema Chadema imepoteza dira na haina maridhiano, hivyo amekwenda CCM ili wakijenge pamoja chama hicho na kuitetea nchi.

“Msigwa ni yuleyule, tuungane kwa pamoja tushirikiane kuhakikisha tunailetea nchi yetu maendeleo. Leo Msigwa anahama na watu 15 Chadema,” amesema mwanasiasa huyo.

Amesema watalii walikuwa wachache na yeye akiwa bungeni waliilaumu Serikali, lakini sasa Rais Samia kwa moyo wa uzalendo wa kutengeneza filamu ya Royal Tour.

“Maana ya upinzani ni nini? Akifanya jambo jema hatupongezi. Watu wanasema Msigwa hajasoma, kwani alipokuwa Chadema alisoma?” amehoji.

Kuhusu makato kwa wabunge, Msigwa amesema wabunge walikuwa wanakatwa fedha kila mwezi na wabunge wa viti maalumu alikuwa wanakatwa Sh1.03 milioni, huku wabunge wa majimbo walikatwa Sh510,000.

“Viongozi wa Chadema watoke waseme hizo fedha zaidi ya Sh2 bilioni walizokuwa wanakatwa wabunge zilikuwa zinakwenda wapi kama sio baadhi ya viongozi wanajinufaisha wenyewe?” amehoji Msigwa.

Alipotafutwa Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Kanda ya Nyasa, Frank Mwakajoka kuzungumzia tuhuma za Msigwa, amekanusha akieleza hazina ukweli wowote, huku akisema Msigwa lazima azungumze hivyo kwa kuwa sasa yuko upande wa pili.

“Ni demokrasia ipi anayotaka, mbona baada ya kufanyika uchaguzi wa kanda na mshindi kupatikana alitoka mbele ya hadhara kupongeza chama kina ukomavu wa kidemokrasia na kuahidi kutoa ushirikiano kwa viongozi, sasa inakuaje anazungumza hivyo sasa?” amehoji.

Mwakajoka aliyekuwa mwandani wa Msigwa katika uchaguzi huo, amesema wakati mwingine ni vigumu kukubaliana na matokea ya uchaguzi kwa kuwa kila mmoja anapoingia, shabaha yake ni kushinda na si kupoteza.

“Kwa sasa Msigwa anazungumza maneno mengi ambayo hayana ukweli, ni kwa sababu tu hana la kufanya na kwa kuwa amehamia upande mwingine, anaona hana hoja ya msingi ya kusema,” amesema.

Kuhusu tuhuma za ufisadi wa Sh2 bilioni, Mwakajoka amesema fedha hizo zilitumika kwa uwazi, ikiwemo kuwezesha ziara za viongozi kwenda kwa wananchi kuwaeleza mambo yaliyokuwa yakifanywa na Serikali ya awamu ya tano ya kuminya uhuru.

“Ni kweli mwaka 2015 wabunge wote wa Chadema tuliweka utaratibu wa kuchanga fedha kwa ajili ya kujipanga na uchaguzi wa Serikali za mitaa na uchaguzi mkuu na katika utaratibu huo, wabunge wa viti maalumu walichangia Sh1 milioni na wabunge wenye majimbo Sh500,000 kila mmoja,” amesema.

Mwakajoka amesema sababu ya kuchangia viwango hivyo tofauti ni kwa kuwa mbunge wa jimbo anakuwa na mambo mengi ya kufanya katika jimbo lake tofauti na wabunge wa viti maalumu.

Akizungumza kwenye mkutano huo, mbunge wa Iringa Mjini (CCM), Jesca Msambatavangu amesema ikiwa kuna jambo ambalo Msigwa anaona hajakamilisha, anamualika kushauriana naye ili lifanyike.

“Kaka umethibitisha kuwa huna hiyana ndani yako, umeona kazi zinafanyika, nawe umekuja kuunga mkono, karibu sana,” amesema Jesca na kuongeza:

“Kama kuna jambo ulidhani ungefanya, karibu uje kunishauri na tufanye,” amesema Msambatavangu.

Akizungumzia kauli ya Msigwa, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Paul Loisulie amesema kinachofanywa na Msigwa kinaendelea kuthibitisha siasa za nchi bado hazijapevuka, badala ya kujadili masuala, wanajikita kuongea umbea.

Dk Loisulie amesema kukosekana kwa itikadi ni sababu ya wanasiasa wengi nchini kuzungumzia zaidi watu badala ya masuala yanayoikabili jamii.

“Watu waliopevuka wanajadili masuala (issues) na wenye upeo mdogo wanajadili mambo ya umbea na watu unatukanaje watu wakati unajua wananchi hawana maji na kama watu wanatekwa kwa sababu ya Katiba, matatizo yanaendelea,” amesema.

Chanzo: Mwananchi