Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbowe: Umaskini wetu unaanzia hapa

Mbowe 255 255 Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe.

Wed, 26 Jun 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, ameibua hoja ya kupaa gharama za maisha nchini, akichambua hali ya maisha Tanzania na nchi jirani ya Kenya.

Amesema hali hiyo inasababisha maumivu kila mahali, kutokana na bidhaa muhimu kupanda bei.

Akizungumza na wananchi wa Minjingu katika Wilaya ya Babati mkoani Manyara, Mbowe ametaja mambo yanayochochea kupaa kwa gharama za maisha nchini kuwa ni pamoja na malori yanayotoka nchi jirani, kuachwa yakizunguka mashambani yakichukua malighafi za viwandani na kusafirishwa kwenda nje ya nchi.

“Angalia malori yanayokwenda Kenya, yamebeba bidhaa za mashambani. Yamebeba nyanya za Tanzania, yamebeba vitunguu vya Tanzania, yamebeba mahindi ya Tanzania, yamebeba maharage ya Tanzania, yamebeba parachichi, yamebeba kabeji, yamebeba mboga, kila kitu wanapeleka Kenya.

“Ukiangalia malori yanayotoka Kenya kuja Tanzania, yamebeba bidhaa za viwandani. Maana yake ni nini, kwamba Tanzania tunauza mahindi kwa mfano shilingi 1,000 tunawauzia Wakenya.

…Wananunua mahindi wanakwenda kuyatengeneza wanasaga, unakuwa unga wa mahindi, ama unga wa lishe wanaturudishia Watanzania. Mahindi kilo waliyonunua Sh. 1,000 Tanzania yakienda Kenya viwanda vya Kenya, vya vijana wa Kenya vinafanya kazi, Wakenya wanapata kazi. Halafu wanarejesha mahindi Namanga, yakiwa ni unga wanatuuzia Watanzania kilo moja zaidi ya Sh. 3,000.”

Aidha, alisema machungwa kutoka Tanga, tani kwa tani, malori ya mizigo aina ya Fusso kuanzia 20 mpaka 30 yanaenda Kenya, yanachukua matunda wanakwenda kuyachakata, wanakamua juisi (sharubati) wanaweka kwenye chupa na kwenye vipaketi, wanatia kwenye malori na wanawarudishia Watanzania.

“Yaani aliyetuloga sijui ni nani! Kwa hiyo matunda yakienda Kenya, wanapata ajira vijana wao. Tunatamani vijana wa Tarangire, Minjingu wenye jeuri ya kusimama na kutetea nchi yao na kutetea malaika wa Mungu wao.

Aidha, Mbowe alidai kuwa bidhaa kutoka upande wa Kenya, zina unafuu kwa asilimia 40 ikilinganishwa na Tanzania, kwa kuwa mfuko wa saruji wa kilo 50, Kenya wanaununua kwa Sh. 9,000 na wakija Tanzania, wananunua kwa Sh. 22,000. Vilevile, Mbowe amedai kuwa sukari ya Kenya ni Sh. 1,600 ya Tanzania, na wakiileta Tanzania ni Sh. 5,000 na ukikutwa nayo ni jela.

UMASIKINI

Kuhusu hali ya umasikini katika eneo la Minjingu, Mbowe amesema: “Huu Mji wa Minjingu ulijengwa na kiwanda hiki, nyumba nzuri mnazoziona Minjingu zilijengwa na kiwanda hiki. Jana (juzi) nilikuwa pale Namanga (Wilaya ya Longido), ukienda pale kuna jambo linaumiza sana.

“Ni hivi ndugu zangu, Kenya na Tanzania ni ndugu na ni majirani, Wamasai wa Kenya, ndio Wamasai wa Tanzania. Ardhi yetu na ardhi yao ni sawasawa. Ukienda Namanga unaiona Kenya hiyo na Kenya wanaiona Tanzania hii. Nilifika Namanga jana, ninawauliza wananchi, mna maisha gani hapa mkilinganisha na Kenya? …Wakaniambia ‘Mwenyekiti, wala huwezi kulinganisha’. Nikawauliza ‘kwanini? Wakaniambia ‘upande wa Kenya, wana maji kwenye kila kaya, kila nyumba ina maji ya bomba ni safi na salama.

Upande wa Tanzania hatuna maji’. Jana waliniambia upande wa Kenya wana umeme saa 24, wakaniambia ‘hapa upande wa Tanzania tunaweza kwenda hadi wiki mbili tatu hatujaona umeme’.

…Wakaniambia ‘watoto wetu wote wale wenye uwezo wanavuka mpaka kwenda kwenye shule za Kenya, lakini hakuna mtoto hata mmoja anayetoka kuja kusoma Tanzania,” Mbowe alisema katika mkutano huo.

WAZIRI MKUMBO Juni 13 mwaka huu, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, akiwasilisha bungeni Taarifa ya Hali ya Uchumi kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka 2024/25, alitaja mambo matano yanayoonesha kuwapo tatizo kiuchumi nchini. 

Alitaja mambo hayo matano ni pamoja na: Ukuaji uchumi umekuwa ukihusisha sekta chache na ambazo haziajiri watu wengi kutoka kaya maskini; na ukuaji uchumi nchini umekuwa unategemea uwekezaji wa umma katika miundombinu huku sekta binafsi haijaonekana kuchukua nafasi yake kikamilifu katika kuchochea ukuaji uchumi kama ilivyotarajiwa.

Waziri huyo alitaja jambo lingine ni Tanzania inanunua zaidi kutoka nje kuliko kiwango inachouza. Hivyo, bado kuna urari mkubwa katika biashara. 

“Kwa mfano, thamani ya mauzo ya bidhaa za Tanzania nje ya nchi kwa mwaka 2023 ilikuwa Dola za Marekani bilioni 8.2 kulinganisha na thamani ya ununuzi wa bidhaa ambazo Tanzania iliagiza kutoka nje ya nchi ya Dola bilioni 13.7. 

“Hii ndiyo kusema nchi yetu bado inatumia fedha nyingi za kigeni kuagiza bidhaa ambazo zingeweza kuzalishwa nchini,” alisema Waziri Mkumbo na kufafanua kuwa uchumi umekuwa ukikua kwa kasi zaidi katika maeneo ya mijini kuliko vijijini. 

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: