Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Maombi matatu ya Pinda kwa Rais Samia

Pinda Samia  Pic Maombi matatu ya Pinda kwa Rais Samia

Tue, 16 Jul 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda amemuomba Rais Samia Suluhu Hassan Sh1.6 bilioni kwa ajili ya kuwalipa fidia wakazi walio jirani na eneo la Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Kampasi ya Katavi ili kupisha upanuzi wake.

Pinda ametoa ombi hilo jana Julai 15, 2024 alipozungumza na wananchi wa Kibaoni, wilayani Mpimbwe, wakati Rais Samia akihitimisha ziara mkoani Katavi.

Amesema eneo hilo lililopewa jina la Mizengo Pinda limepatikana na litasaidia kukiendeleza chuo hicho, ikiwa ni pamoja na kufanya upanuzi wa majengo ya hosteli.

Pinda amesema licha ya jitihada mbalimbali alizofanya akishirikiana na viongozi wa halmashauri hiyo, ulijitokeza mkwamo, hivyo kumuomba Rais Samia kuliangalia suala hilo.

“Tumefarijika sasa katika mkoa huu wa wakulima na sisi tumepata chuo ambacho ni kitengo muhimu katika utoaji wa elimu,” amesema.

Pia, amemuomba Rais Samia Halmashauri ya Mpimbwe kuwa wilaya inayojitegemea ili kuongeza ukaribu wa upatikanaji wa huduma za kijamii kwa wananchi, ombi ambalo pia lilitolewa na Mbunge wa Kavuu na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Geophrey Pinda.

Vilevile ametumia fursa hiyo kuipigia chapuo Hifadhi ya Katavi akiomba Rais Samia atakapofanya ‘Royal Tour’ kwa awamu nyingine asiisahau hifadhi hiyo. Amesema hifadhi hiyo itasaidia kuimarisha uchumi wa mkoa huo na sekta ya utalii kwa jumla kutokana na upekee wa mwonekano wa wanyama wanaopatikana eneo hilo, ambao ni wakubwa.

“Kutokana na uoto wa asili uliopo katika hifadhi hiyo muonekano wa wanyama wanaopatikana ni tofauti na hifadhi nyingine jambo linalotengeneza upekee,” amesema.

Akijibu maombi hayo, kuhusu hifadhi ya Katavi, Rais amesema tayari alishapita katika hifadhi hiyo na kujua mahitaji yake na kuahidi kufika katika hifadhi hiyo kwa ajili ya ‘Royal Tour’.

Kuhusu Halmashauri ya Mpimbwe kuwa wilaya, amesema ni jambo linalohitaji muda, akimuhakikishia Waziri Mkuu huyo mstaafu kupatikana kwa fedha kwa ajili ya upanuzi wa Chuo Kikuu cha SUA, Kampasi ya Mizengo Pinda.

Awali, Rais Samia akihutubia wananchi wa eneo hilo amesema Serikali imedhamiria kuhakikisha Mkoa wa Katavi unakuwa kanda maalumu kwa ajili ya uzalishaji na uhifadhi wa mazao ya chakula.

Amesema hilo linatokana na mkoa huo kuwa moja kati ya mikoa ambayo ni wazalishaji wakubwa wa chakula.

“Katavi ni wazalishaji wazuri wa chakula nataka niwaahidi Serikali itashirikiana na wakulima kuhakikisha uzalishaji unazidi kuongezeka,” amesema.

Amesema katika kuhakikisha kilimo kinaendelea kuimarika Serikali itaendelea kuboresha mambo mbalimbali ikiwamo kuongeza skimu za umwagiliaji sita.

Zilizojengwa mpaka sasa amesema ni 29. Pia, kuongeza maghala kwa ajili ya kuhifadhia chakula na ujenzi wa mabwawa ambayo yatasaidia shughuli za kilimo cha umwagiliaji kuendelea hata inapofika kipindi cha kiangazi.

“Hiyo yote ni kwa ajili ya kuhakikisha Mkoa wa Katavi unaendelea kuwa kinara wa uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara,” amesema.

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema mbolea ya ruzuku itaendelea kutolewa. Pia, amesema Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) utanunua mahindi kwa Sh600 kwa kilo badala ya Sh500 na vituo vya makao makuu ya miji vitanunua kwa Sh650.

Bashe amesema katika vituo hivyo kwa sasa imewekwa mizani ya kidijitali ambayo baada ya mazao kupimwa mhusika anapokea ujumbe kupitia simu yake kuwa mazao yake ni kiasi gani.

“Yale mambo ya kuambiwa na ofisa aliyekaa kwenye mzani mazao yako ni kiasi kadhaa yamepitwa ni wakati sasa unajionea mwenyewe huku ukipokea ujumbe,” amesema.

Rais Samia ameanza ziara Mkoa wa Rukwa kwa kufanya uzinduzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi.

Baada ya kukagua na kuzindua hospitali hiyo, Rais Samia amesema ameridhishwa na ujenzi na huduma zinazotolewa katika hospitali hiyo huku akitoa wito kwa wahudumu wa afya kufanya kazi kwa uzalendo na ueledi.

Amesema kwa kufanya hivyo siyo tu wanapata malipo kutoka kwa Serikali bali pia wanapata baraka kutoka kwa Mungu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live