Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Majibu ya CCM Mdahalo wa Odemba: Tunasikitishwa na jinsi alivyoupotosha umma

Nchimbi Ccm (22).jpeg Majibu ya CCM Mdahalo wa Odemba: Tunasikitishwa na jinsi alivyoupotosha umma

Mon, 2 Sep 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinapenda kutoa taarifa kwa umma kuhusu kutoshiriki kwa Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi kwenye mdahalo ulioandaliwa na Kituo cha Televisheni cha Star Tv, na kuratibiwa na Ndugu Edwin Odemba tarehe 31 Agosti, 2024.

CCM inautaarifu umma kuwa Katibu Mkuu hakukimbia wala hakudharau mdahalo huo. Balozi Nchimbi alifanya kila jitihada za mawasiliano na muaandaji na tunasikitishwa na jinsi alivyoupotosha umma.

Tarehe 10 Agosti 2024 mtangazaji wa Kituo cha Televisheni, Star Tv, Ndugu Edwin Odemba alimtafuta Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt Emmanuel Nchimbi kwa kutuma ujumbe mfupi wa simu (sms) akimuomba Katibu Mkuu ashiriki mdahalo huo wa viongozi wa vyama vya siasa uliopangwa kufanyika Jumamosi, tarehe 31 Agosti 2024.

Katibu Mkuu alimjulisha kuwa masuala ya vyombo vya habari yanaratibiwa na Katibu wa Halmshauri Kuu ya CCM Taifa, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Ndugu Amos Gabriel Makalla hivyo awasiliane naye na akampa namba ya simu ya mkononi ya Ndugu Makalla.

Kwa sababu ambazo Odemba anaweza kuzieleza mwenyewe, katika kipindi cha takriban wiki tatu, hakufanya mawasiliano au kumtafuta Ndugu Makalla kama alivyoelekezwa na kushauriwa na Katibu Mkuu Balozi Nchimbi.

Baada ya kuhisi kwamba nafasi ya Katibu Mkuu inaweza kuwa ngumu kupatikana kutokana na majukumu yake ya kazi za chama, Ndugu Odemba alimtafuta tena Balozi Nchimbi akiomba amuandae mwakilishi huku matangazo ya mdahalo huo yakiendelea kumtaja Katibu Mkuu wa CCM kuwa ndiye atakayeshiriki. Badala yake Katibu Mkuu alimwelekeza Ndugu Odemba kutofanya lolote kabla ya kupata mawasiliano na Sekretarieti ya Chama.

Kimsingi Ndugu Odemba alitaka wananchi wadanganywe kuwa CCM kupitia kwa Katibu Mkuu ilikuwa imethibitisha kushiriki katika mdahalo huo jambo ambalo si sahihi.

Katika mazingira ya kustaajabisha tumeshangazwa na machozi ya Ndugu Odemba aliyotoa jana akielekeza lawama kwa CCM na kwa Katibu Mkuu wakati alijua bayana kwamba alikuwa hajapata uthibitisho wowote wa CCM kushiriki ikiwa ni pamoja na ukweli kwamba yeye mwenyewe alishajua kwamba alikuwa akiendelea kutangaza kuhusu mdahalo huo kama "promo" pasipo kupata ridhaa ya CCM.

Katibu Mkuu wa CCM ndiye Mwenyekiti wa Sekretarieti na siku nzima ya jana ambayo ndiyo siku Odemba alipanga kufanyika kwa mdahalo huo, kulikuwa na vikao vya maandalizi ya Kamati Kuu Maalum ambayo inafanyika leo tarehe 01 Septemba 2024, jambo ambalo kwa namna yoyote Katibu Mkuu asingeweza kuwapo katika mdahalo huo hata kama angekuwa amethibitisha awali.

Kushiriki kwenye mdahalo kunahitaji mashauriano na maafikiano kati ya waandaji na waalikwa.

Tunaweza kutamka bayana na kwa uhakika kwamba Katibu Mkuu hakuwa ametoa uthibitisho wa kuhudhuria mdahalo huo. Hakukuwa na makubaliano yoyote rasmi ya yeye au mwakilishi wake kuhudhuria katika shughuli hiyo.

Mwisho, Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Nchimbi yupo tayari kwa midahalo, majadiliano na makongamano yanayolenga kujenga umoja wa kitaifa na maridhiano ya kisiasa kadiri ya taratibu zilizopo na ratiba yake ya kazi inavyoruhusu.

KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI

Chanzo: www.tanzaniaweb.live