Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Lissu anavyogeuka panga la kukodi kuiumiza Chadema

Tundulissupic Lissu anavyogeuka panga la kukodi kuiumiza Chadema

Wed, 21 Aug 2024 Chanzo: mwanachidigital

Thirty-Six Stratagems ni andiko ndani ya Kitabu cha Qi (Book of Qi) au kwa Kichina hutamkwa Qi Shu, ambacho maudhui yake ni historia ya tawala za ukoo China. Qi Shu ni cha Kusini ya China, hivyo kilipoandikwa kitabu cha historia Kaskazini ya China (Northern Qi), Qi Shu hutambulika zaidi kama Southern Qi.

Southern Qi ni utawala wa ukoo Kusini ya China kuanzia mwaka 479 mpaka 502. Mfalme Xiao Daocheng ‘Gao’, maarufu Mfalme Gao ndiye mtawala wa kwanza wa Southern Qi. Wang Jingze alikuwa jenerali wa vikosi vya ulinzi na usalama vya Southern Qi.

Baada ya Mfalme Gao kufariki dunia, alifuata mjukuu wake, Mfalme Xiao Zhaoye ambaye alimteua Xiao Luan (mjomba wake) kuwa Waziri Mkuu. Xiao Luan alimpindua Mfalme Xiao Zhaoye (mpwa wake) na kumuua kwa hoja kuwa alikuwa hatoshi ufalme.

Xiao Luan ndiye Mfalme Ming ambaye baada ya kujitangaza Mfalme wa Southern Qi, alianza kuua watu ambao walikuwa ni ndugu damu ya moja kwa moja kutoka kwa Mfalme Xiao Zhaoye mpaka Mfalme Gao. Alitaka kukifuta kizazi chote ili abaki salama.

Wang Jingze alipoona mnyororo wa vifo, alijua naye zamu yake ya kuuawa imewadia, ndipo alipozama chini kuandika mkakati wenye mbinu chafu za kumwondoa madarakani Mfalme Ming. Mkakati huo ndiyo Thirty-Six Stratagems na ndiyo ambao nautumia hapa kuonesha jinsi nadharia zake zinavyofanana na hali iliyopo baina ya Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tanzania Bara, Tundu Lissu, dhidi ya chama chake.

Sura ya Kwanza, somo ni Ushindi wa Mbinu Chafu (Winning Stratagems), sehemu ya tatu katika sura hiyo inafundishwa “kuua kwa upanga wa kuazima”. Naam, matamshi ya Lissu, yanaiweka Chadema njiapanda. Lissu amekuwa mshereheshaji wa mashambulizi dhidi ya Chadema, yanayorushwa na kiongozi mwenzao wa zamani, Peter Msigwa.

Tafsiri; Upanga wa kuazima ni hali ya kushawishi nguvu nyingine kubwa imkabili adui unayemkusudia ili kumdhoofisha au ndani ya adui yako, unampata mtu, unamtengeneza ili aasi na kugeuka msaliti, mwisho ndani ya adui yako kunakuwa na mvurugano wa ndani kwa ndani ambao unamdhoofisha kwa maslahi yako.

Ndani ya Chadema, Lissu inawezekana amedhamiria au anatenda pasipo kujua. Hata hivyo, jinsi anavyotokeza na kutaka chama chake kitoe ufafanuzi wa tuhuma ambazo Msigwa anazitoa, wakati huohuo akikiri kwamba ameumizwa Msigwa kuhamia CCM, ni dhahiri inajenga picha ambayo siyo nzuri.

Mei 2024, Msigwa akiwa bado yupo Chadema, Lissu alikwenda Iringa, akashusha tuhuma nzito. Lissu alisema, kuna fedha nyingi zilitembea kwenye uchaguzi. Alidai fedha zilitoka CCM. Aliyasema hayo kwenye mkutano ambao uliandaliwa na Msigwa, ambaye wakati huo alikuwa Mwenyekiti wa Chadema, Kanda ya Nyasa.

Maneno ya Lissu, moja kwa moja yalitafsiriwa kama shambulizi kwa mbunge wa Mbeya Mjini 2010-2020, Joseph Mbilinyi “Sugu”, ambaye alikuwa anawania uenyekiti wa Kanda ya Nyasa, akichuana na Msigwa. Maneno ya Lissu, dhahiri yalikishambulia na kukifunga magoli chama chake. Magoli ya kisiasa.

Lissu, kiongozi namba mbili Chadema. Kama kuna matatizo ya rushwa kwenye chama, ana nafasi nzuri kabisa ya kuyashughulikia bila kupayuka kwenye mikutano ya hadhara. Wapo walioamini kuwa kauli za Lissu ni kuyumba kiuongozi. Wengine walidhani Lissu kwa uelewa wake wa mambo, hakubahatisha, isipokuwa alipiga shambulio dhidi ya Sugu ili kumsaidia Msigwa.

Rushwa ni kitu kibaya mno. Mapambano yake hayafai kutekelezwa kwa kelele za majukwaani, bali kwa hatua stahiki. Lissu kwa nafasi yake ya Makamu Mwenyekiti, kama kweli alishajua kuhusu uwepo wa vitendo vya rushwa, alipaswa kuchukua hatua au kushauri mamlaka husika za chama kufanyia kazi.

Kitendo cha kuzungumza jukwaani siyo tu kinagawa chama, bali kinadhihirisha udhaifu wa mifumo Chadema. Kwanza, inaonesha Chadema hawana uwezo wa kupambana na rushwa. Ikiwa fedha zinatembea, viongozi wa juu hawachukui hatua, bali wanalalamika majukwaani, je, wakikabidhiwa nchi wataweza kuzikabili rushwa kubwa?

Moja ya majanga makubwa ambayo yanaipeleka Tanzania kubaya ni rushwa. Watanzania wangependa kuona vyama mbadala vya siasa vyenye kujipambanua waziwazi kukabiliana na rushwa ili viwape matumaini na waviamini. Chama ambacho viongozi wake wa juu wanalalamikia rushwa dhidi ya wao kwa wao, kinaweza vipi kujenga kuaminika?

Matamshi ya Lissu Iringa, yalitosha kuunda muktadha hasi dhidi ya Chadema, kwamba chama hicho kimeshindwa kutibu janga la rushwa ndani, je, kitaweza kuyamudu madudu ambayo yanaikabili nchi katika mtandao mpana? Hapa ndipo kwenye tafsri ya Lissu kuishambulia na kuifunga Chadema magoli ya kisiasa.

Msigwa aliondoka Chadema kwa kinyongo. Alitoka kushindwa uenyekiti Kanda ya Nyasa na Sugu. Awali, alikubali matokeo, lakini baadaye akawa mbogo. Akarusha mashambulizi mfululizo dhidi ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe. Malalamiko ya Msigwa ni kwamba nyuma ya kushindwa kwake yupo Mbowe.

Msigwa, kabla hajahamia CCM, alitoa kauli tata kuhusu kuwania uenyekiti Chadema taifa. Alisema, kama ilivyokuwa kwake yeye na Sugu Nyasa, basi na uchaguzi wa Chadema taifa, lazima kuwe na wagombea wawili wenye nguvu na washindane kwa mdahalo. Moja kwa moja, alikusudia kufikisha ujumbe kwamba Mbowe lazima apimwe dhidi ya mtu imara katika uchaguzi ujao ndani ya chama.

Baada ya kuhamia CCM, Msigwa alirusha kombora kwa Mbowe, aliposema kuwa kila nafasi anataka yeye, uenyekiti hadi kugombea urais. Mbowe alikuwa mgombea urais wa Chadema Uchaguzi Mkuu 2005. Mwaka 2010, alisimama Dk Willibrod Slaa. Mwaka 2015, ilikuwa zamu ya Edward Lowassa. Mwaka 2020, alikuwa Lissu. Hata hivyo, zipo fununu lakini ni sahihi kwa asilimia kubwa kwamba Mbowe anataka kuwania urais 2025.

Mtu anayeomba kuwa mgombea urais baada ya miaka 20, unawezaje kusema “anataka yeye tu kugombea urais?” Kuna mahali inatafutwa sababu na kisingizo. Mbowe amekuwa kisingizio cha kila anayehama chama hicho. Msigwa ameendeleza utamaduni.

Lissu anapotokeza na kutaka hoja za Msigwa zijibiwe kwa ushahidi, ni dhahiri anakuwa anamgusa Mbowe, ambaye ndiye mtajwa mkuu. Vipi Mbowe naye akitokeza na kumkabili Lissu? Chama kitabaki salama? Kwa vyovyote, CCM watanufaika kwa mkorogano wa Mbowe na Lissu. Na hayo yatakuwa matunda ya panga la kukodi.

Chanzo: mwanachidigital