Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Lissu: Wanyimeni CCM kura mtokomeze Umasikini

Lissu Uchaguziiii Makamu wa Mwenyekiti wa Chadema (Bara), Tundu Lissu

Wed, 19 Jun 2024 Chanzo: Mwananchi

Makamu wa Mwenyekiti wa Chadema (Bara), Tundu Lissu amewataka wananchi wa Manyoni mkoani Singida kuikataa CCM katika chaguzi za Serikali za Mitaa, vijiji na vitongoji ili waondokane na ugumu wa maisha wanapaswa kumalizana na.

Amesema wananchi hao wakiikataa CCM katika ngazi ya vijiji na vitongoji, watakuwa wamekikata miguu na kukivunja nguvu chama hicho tawala nchini.

Lissu amefafanua kuwa wenyeviti wa vijiji na vitongoji ndiyo kila kitu katika uongozi wa chini, hivyo wakiwepo wa upinzani CCM hakitakuwa na nguvu katika maeneo husika.

Lissu ameeleza hayo jana Jumanne Juni 18, 2024 wakati akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika kijiji cha Mitundu wilayani Manyoni mkoani Singida, katika mwendelezo wa ziara yake iliyoingia siku 18 katika majimbo ya Mkoa wa Singida.

“Ukichagua, mwenyekiti wa kijiji, kitongoji na madiwani wote CCM mkipata matatizo hakuna anayeweza kuwasaidia, CCM haijawahi kuwaletea unafuu wa maisha, hakina manufaa zaidi ya kuendelea kuwapa umasikini wananchi,” amesema Lissu.

Lissu ambaye ni mbunge wa zamani wa Singida Mashariki, amesema licha ya umasikini wa Mkoa wa Singida kuwa nyuma kimaendeleo, bado wananchi wake wamekuwa mstari wa mbele kuipigia kura CCM kuanzia katika chaguzi za vijiji na vitongoji.

Hata hivyo, Lissu anasema ili kuondokana na changamoto mbalimbali ikiwemo tozo na michango wanapaswa kuikataa CCM mapema kuanzia kwenye uchaguzi ujao utakaofanyika Oktoba mwaka huu.

“Hilo linawashinda watu wa Mitundu? Kwa hiyo ndugu zangu tuna miezi minne kabla ya Oktoba itakayofanyika uchaguzi wa vijiji na vitongoji na halmashauri, tafuteni watu wa kweli, jasiri na wenye msimamo na haki kuwania nafasi za uongozi,” amesema Lissu.

Awali, Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), John Pambalu amesema majimbo ya Singida karibu yote na mkoa wa Dodoma yote yanatawaliwa na CCM tangu mfumo wa vyama vingi kuanza mwaka 1992.

“Dodoma yote haijawahi kuwa na mbunge wa upinzani, Singida nayo hivyo ukiondoa jimbo la Singida Magharibi hivi mtakuwa hivi hadi lini? amehoji.

Chanzo: Mwananchi