Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kigaila: Msigwa aje kulalamika vikaoni

Msigwa Mnjz Chadema Mchungaji Peter Msigwa.

Wed, 5 Jun 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Siku moja baada ya aliyekuwa mgombea uenyekiti wa Kanda ya Nyasa, Mchungaji Peter Msigwa kudai kuwa msimamizi wa uchaguzi huo, Benson Kigaila kushindwa kusimamia vema mchakato huo, mwenyewe amemjibu akimtaka awasilishe malalamiko yake katika vikao.

Kigaila aliyekuwa msimamizi mkuu wa uchaguzi huo uliofanyika Mei 29, 2024 Makambako mkoani Njombe, amesema Chadema haiwezi kujibizana na wanachama barabarani na kama kuna malalamiko yawasilishwe katika vikao chama biashara inaishia hapo.

Jana Jumatatu Juni 3, 2024 Mchungaji Msigwa alizungumza na wanahabari mkoani Iringa na kuwatuhumu wasimamizi wa uchaguzi wa Nyasa, Kigaila na John Mrema, msimamizi msaidizi, akidai ni miongoni mwa watu waliosababisha kwa namna moja au nyingine yeye kushindwa katika mchakato huo.

Katika uchaguzi huo Msigwa alishindwa kutetea nafasi yake mbele ya Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ kwa tofauti za kura mbili, zilizoamua matokeo hayo. Baada ya uchaguzi huo, Msigwa alikubali matokeo na kumpongeza Sugu kwa ushindi.

Hata hivyo, baada ya siku sita, Mchungaji Msigwa ameibuka akidai Mrema ambaye ni mkurugenzi wa mawasiliano, itifaki, ienezi na Mmambo ya nje wa Chadema, alishiriki kumpigia kampeni Sugu kinyume cha utaratibu.

Amedai alikuwa akiwaambia wajumbe kuwa ametumwa na mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliyetaka mpinzani wake mwenyekiti wa Nyasa.

“Mwanzo niliandika mmoja wa wasimamizi wa uchaguzi (John Mrema), angeondoka ili kupisha mchakato huo. Kama Chadema tulalamikia Serikali ya CCM kwamba wasimamizi wa uchaguzi hawatendi haki basi tulitakiwa tuwe mfano wa kuigwa, kwamba katika chaguzi zetu haki inatendeka,” alisema.

Kuhusu Kigaila ambaye ni naibu katibu mkuu wa Chadema, Bara, Msigwa amesema hakuchukua hatua baada ya watu kuanza kuleta vurugu mbele yake.

“Hali ile inaleta mashaka na ina harufu ya uvundo wa ukiukwaji mkubwa wa haki ndani ya Chadema,” alidai Msigwa.

Lakini leo Juni 4, 2024 Mwananchi lilimtafuta Kigaila kuhusu madai hayo ya Msigwa ambapo alijibu kuwa, “mimi sio aina ya viongozi wa kujibizana na wanachama barabarani, mwanachama mwenye malalamiko anajua njia za chama.

 “Huwezi kwenda barabarani ukataka nikujibu, siwezi kukujibu, sijibizani na wanachama barabarani isipokuwa katika vikao vya chama. Si amekata rufaa? Sasa ukikata rufaa unakwenda barabarani, hivi unakata rufaa barabarani au kwenye chama?” amehoji.

Kigaila amesema wakishaanza kujibizana barabarani na Msigwa hakutakuwa na uhalali wa rufaa iliyokatwa na mwenyekiti huyo wa zamani wa Kanda ya Nyasa inayounda mikoa ya Njombe, Iringa, Mbeya, Rukwa na Songwe.

Jana Msigwa alisema kutokana na kasoro hizo, ameamua kukata rufaa Kamati Kuu ya Chadema kwa madai ya kuwa ushindi alioupata ‘Sugu’ haukuwa halali.

 “Nimekata rufaa kwa chama changu kuwa makatibu watatu wa mabaraza walizuiliwa kupiga kura, ukiangalia kura zangu zilizoongezeka na kufikia sita lakini wajumbe watatu walizuiliwa, rufaa yangu imefafanua mambo mengi yaliyokiukwa katika uchaguzi,” alisema.

Katika hatua nyingine, mjumbe wa bodi ya wadhamini ya Chadema, Dk Azaveli Lwaitama amewataka makada wa chama hicho kama wana madukuduku kutokana na uchaguzi wakate rufaa ndani ya chama.

“Kama una dukuduku kutokana na uchaguzi anakataa rufaa ndani ya mahakama ya chama sio kwenye magazeti, nitashangaa, nikisikia unakwenda ‘mahakama ya magazeti’,” amesema Dk Lwaitama.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: