Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Haya ndiyo yaliyomo kwenye kanuni za uchaguzi serikali za mitaa

Kura Kura Tanzania Haya ndiyo yaliyomo kwenye kanuni za uchaguzi serikali za mitaa

Fri, 14 Jun 2024 Chanzo: Mwananchi

Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) imetoa rasimu ya kanuni za uchaguzi wa serikali katika mamlaka za serikali za mitaa 2024.

Rasimu hizo ni kwa ajili ya kanuni za uchaguzi wa mwenyekiti wa kitongoji katika mamlaka za miji midogo za mwaka 2024, na ya kanuni za uchaguzi wa mwenyekiti wa mtaa na wajumbe wa kamati ya mtaa, 2024.

Zingine ni rasimu ya kanuni za uchaguzi wa serikali za mitaa katika mamlaka za wilaya 2024 na rasimu ya kanuni za uchaguzi wa serikali katika mamlaka za miji 2024.

Rasimu hizo zimechapishwa Juni 12, 2024 katika tovuti ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).

Kanuni hizo zinaeleza masharti na utangulizi, tangazo la uchaguzi, maelekezo ya uchaguzi, uteuzi wa wagombea, utaratibu wa kushughulikia mapingamizi na rufaa, kampeni za uchaguzi, taratibu za kupiga kura, kuhesabu na kutangaza matokeo, nafasi wazi za uchaguzi mdogo, utaratibu wa kuapishwa, makosa na adhabu.

Kanuni zimempa waziri husika mamlaka ya kutoa tangazo kwa umma kuhusu kuwapo uchaguzi katika magazeti ya Kiswahili na Kiingereza yanayosambazwa nchi nzima na katika vyombo vya habari si chini ya siku 90 kabla ya siku ya uchaguzi.

“Tangazo litakalotolewa na waziri litaelekeza ratiba ya uchaguzi na shughuli zinazohusika, na masharti muhimu ya uchaguzi kwa mujibu wa sheria na kanuni hizi,” inaelekezwa katika rasimu hizo.

Wasimamizi wa uchaguzi

Rasimu ya kanuni hizo zinasema kutakuwa na msimamizi wa uchaguzi, msimamizi msaidizi wa uchaguzi, na msimamizi wa kituo atakayeteuliwa kusimamia uchaguzi.

Inaelezwa kiongozi wa chama cha siasa, mgombea, hakimu au jaji, kiongozi wa dini, askari au ofisa yeyote wa chombo cha ulinzi na usalama, katibu tawala wa wilaya, katibu tawala wa mkoa, mkuu wa wilaya au mkuu wa mkoa, hawataruhusiwa kusimamia uchaguzi.

Wapigakura

Kanuni zinasema kutakuwa na orodha ya wapigakura kwa ajili ya uchaguzi huo.

“Uandikishaji na uandaaji wa orodha ya wapigakura utaanza siku ya 47 kabla ya siku ya uchaguzi na utafanyika kwa siku 10 kwenye majengo ya umma na pale ambako hakuna jengo la umma, uandikishaji utafanyika kwenye sehemu ambayo msimamizi msaidizi wa uchaguzi atakuwa amekubaliana na viongozi wa vyama vya siasa.

Wagombea

Kanuni zinawataka wanaoataka kugombea kuchukua fomu ya uteuzi wa kugombea nafasi husika siku zisizopungua 26, kabla ya siku ya uchaguzi kwa kadri itakavyoelekezwa na msimamizi wa uchaguzi.

Mtu aliyechukua fomu atatakiwa kuirejesha ndani ya muda wa siku saba tangu siku ya kwanza ya uchukuaji wa fomu iliyotangazwa na msimamizi wa uchaguzi.

Kanuni zinasema endapo mgombea hakuridhika na uamuzi uliotolewa na msimamizi msaidizi wa uchaguzi au anapinga uteuzi wa mgombea yeyote, anaweza kuwasilisha pingamizi na kumwomba msimamizi msaidizi wa uchaguzi kupitia upya uamuzi uliofanyika ili amteue kuwa mgombea au atengue uteuzi anaoupinga na msimamizi msaidizi wa uchaguzi, baada ya kupitia pingamizi husika, anaweza kukubali au kulikataa pingamizi hilo.

“Mwombaji au mgombea ambaye hataridhika na uamuzi wa msimamizi msaidizi wa uchaguzi, atakuwa na haki ya kukata rufaa kwenye kamati ya rufani iliyoanzishwa chini ya kanuni ya 24 katika muda usiozidi siku nne kuanzia tarehe ya uamuzi wa msimamizi msaidizi wa uchaguzi,” inaelezwa katika rasimu hizo.

Kampeni

Rasimu za kanuni zimetoa siku saba za kampeni kabla ya uchaguzi na kila chama cha siasa kinachoshiriki uchaguzi kitawasilisha ratiba yake ya mikutano ya kampeni ya uchaguzi kwa msimamizi wa uchaguzi, si chini ya siku saba kabla ya kuanza kwa kampeni.

Chanzo: Mwananchi