Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

FRED LOWASSA: Nchimbi usiruhusu ya baba yajirudie

Fred Lowassa X Nchimbi FRED LOWASSA: Nchimbi usiruhusu ya baba yajirudie

Mon, 3 Jun 2024 Chanzo: Nipashe

Mbunge wa Monduli, Fred Lowassa, ameibua tena suala la kukatwa kwa jina la baba yake, Edward Lowassa, Waziri Mkuu wa zamani, katika mchakato wa kupata mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) mwaka 2015.

Safari hii Fred amepongeza msimamo uliooneshwa na Katibu Mkuu wa sasa wa CCM, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, ambaye alitamka wazi kutokukubaliana na uamuzi uliofanywa wakati huo dhidi ya Lowassa.

Akizungumza jana katika mkutano wa hadhara uliofanyika Makuyuni, wilayani Monduli, mkoani Arusha, Fred alisema kuwa Balozi Dk. Nchimbi alimtendea haki baba yake, Hayati Lowassa.

Mbunge huyo alisema hataona aibu kusema hilo na kama atakuwa amekosea basi asamehewe, akisisitiza kuwa Katibu Mkuu wao wa sasa Balozi Dk. Nchimbi anapaswa kuhakikisha kanuni hazivunjwi tena ndani ya chama chao.

"Siku ile ulitoka katika kikao cha Kamati Kuu kwa heshima, ukasema 'kwa kuwa kanuni za chama zimekanyangwa sitavumilia'. Wewe sasa ni Katibu Mkuu, ukasimamie (kanuni) zisikanyagwe tena," Fred alisema.

Makada 38 walijotosa kuwania kuteuliwa kupeperusha bendera ya CCM katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015. Hata hivyo, majina ya makada 33, akiwamo Lowassa, yalikatwa katika hatua ya awali. Yalibaki majina matano ya Bernard Membe, Dk. Asha Rose Migiro, January Makamba, Amina Salum Ali na Dk. John Magufuli, ambaye mwishowe alipitishwa kuwa mgombea wa chama hicho, Rais Samia Suluhu Hassan akiwa mgombea mwenza.

Hatua ya kukata jina la Lowassa aliyekuwa anapewa nafasi kubwa, haikufurahiwa na baadhi ya wajumbe wa vikao vya juu vya CCM.

Dk. Nchimbi alikuwa miongoni mwa wajumbe watatu wa Kamati Kuu ya CCM walioitisha mkutano na waandishi wa habari na kueleza kuwa wanapinga uamuzi huo kwa madai kikao kilichofanya uamuzi huo hakikifuata kanuni kwa kuwa majina machache yaliwasilishwa na hayakuhusisha mgombea anayekubalika.

Wajumbe wengine walioungana na Dk. Nchimbi kupinga uamuzi huo ni aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma, Adam Kimbisa na Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Sophia Simba.

Hata hivyo, Dk. Nchimbi na Sophia baadaye waliingizwa katika timu ya kampeni za ushindi wa Dk. Magufuli aliyepitishwa na Mkutano Mkuu wa CCM kuwa mgombea wao wa urais.

Baada ya jina lake kukatwa CCM, Lowassa alijiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) alikoteuliwa kuwa mgombea urais, akiungwa mkono na vyama vingine vya upinzani vilivyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).

Huko aliipa ushindani mkali CCM, akitangazwa kushika nafasi ya pili katika mbio za urais nyuma ya Dk. Magufuli huku akisaidia vyama vya upinzani kuwa na wabunge wengi katika Bunge la Tanzania.

Katika mkutano wa hadhara jimboni Monduli jana, Balozi Dk. Nchimbi, pasi na kujibu chochote kilichotokea mwaka 2015 kwa Lowassa, alisema, "wakulima waheshimu wafugaji, vivyohivyo kwa wafugaji. Tunategemeana unakula ugali na nyama. Ukiona mkulima anamdharau mfugaji, hajui wajibu wake, vivyohivyo kwa mfugaji."

Aliwashukuru wananchi kwa kujali polisi, walimu na manesi kwa kuwa ni kundi ambalo linahangaika usiku na mchana, hivyo changamoto za nyumba walizoeleza ni suala muhimu la kufanyiwa kazi.

Balozi Nchimbi alisema mwezi mmoja na nusu mbunge wa jimbo hilo alimtafuta, akaomba asaidiwe kusukuma suala la miradi miwili mikubwa ya maji inayotakiwa kutekelezwa na alimtafuta waziri mwenye dhamana na kumtaka aende kulishughulikia. Tayari mkataba umetiwa saini.

Alimpigia simu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, naye aliwaeleza wananchi kuwa mahitaji ya maji ni zaidi ya lita 300,000 jimboni humo na uwezo uliopo ni zaidi ya lita 100,000.

Alisema serikali imeshaagiza kujengwe mradi wa Sh. bilioni saba na tayari mradi umeshatiwa saini na mkandarasi anatafuta mabomba. Yeye (Aweso) atasimamia ukamilike kwa wakati.

Kuhusu kumalizia jengo la kulaza wagonjwa katika Hospitali ya Makuyuni, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa, akizungumza kwa njia ya simu, aliahidi watafika kwa ajili ya tathmini na kuhakikisha jengo hilo linajengwa na kuhudumia wananchi wa Monduli.

Balozi Dk. Nchimbi alisema kuwa kiongozi asiyeguswa na kero za wananchi hatoshi katika nafasi yake.

"Wananchi wote mliokuja kushirikiana nasi hapa, tunawashukuru sana, niwahakikishe CCM imeendelea kusimamia serikali zake kuona zinahudumia wananchi kwa upendo," alisema.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, alisema kuna changamoto ya ajira kwa vijana, ndio maana wanagusa sekta ya utalii ambayo sasa ina watalii wengi. Alisema yuko tayari kupokea maagizo yoyote halali ya chama na kuyatekeleza.

Katika mkutano huo, Balozi Nchimbi pia aliahidi kukabidhi pikipiki moja leo kwa mama aliyeomba msaada huo na Mkuu wa Mkoa huo. Makonda naye akaahidi kutoa pikipiki kwa kijana mwingine.

Akiwa mkoani Manyara juzi, Balozi Dk. Nchimbi alisema anavutiwa na aina ya wakuu wa mikoa ambao wanaposikia matatizo ya wananchi wanakwenda kuyatatua na si wakuu wa mikoa mabwana wakubwa ambao muda wote wanatamani kujionesha wao ni kina nani.

Chanzo: Nipashe