Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Demokrasia bila nidhamu ni fujo, nidhamu bila Demokrasia ni Udikteta

Mbowe Musomaa Demokrasia bila nidhamu ni fujo, nidhamu bila demokrasia ni udikteta

Tue, 15 Aug 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Hayati Rais wa awamu ya tatu, Benjamin William Mkapa aliwahi kusema: “Kazi ya uongozi ni kuonyesha njia na watu wanakufuata si kwa sababu wanakuogopa ila kwa sababu wanakuamini na imani ya kweli haitokani na maneno bali matendo”.

Serikali ya Awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan imesimama mstari wa mbele kuleta maendeleo makubwa katika sekta ya uchukuzi nchini kwa kuweka mazingira bora ya uwekezaji ili kuongeza mapato.

Hali hiyo imeiwezesha serikali kuja na mipango mbalimbali kuhakikisha sekta hiyo inakuwa na mafanikio lukuki hususan eneo la bandari ambalo limekuwa na muhimu kwa uchumi wa nchi kutokana na mipango mikubwa iliyowekwa na serikali ndani eneo hilo.

Toka serikali ilipoingia makubaliano kati yake na Dubai maneno yalikuwa mengi kutokana na makubaliano hayo yaliyolenga kukuza uchumi wa nchi na kuleta mpinduzi makubwa katika sekta hiyo ambayo imekuwa na mchango mkubwa katika kukuza uchumi na pato la taifa.

Kujitokeza kwa mawakili na wananchi kupinga mkataba huo na kufungua kesi Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya ilikuwa ni jambo bora linalokwenda kujibu maswali ya ubishani wa Mkataba wa Uwekezaji wa Bandari ya Dar es Salaam baina ya Tanzania na Kampuni ya DP World ya Dubai kuwa ni sahihi au lah.

Nionavyo, lilikuwa jambo bora na kuonyesha nidhamu kubwa ya demokrasia iliopo kwa taifa pale jamii inaposhindwa kutatua matatizo yao basi eneo moja kubwa la kutatua ubishi ni mahakamani, hivyo kufunguliwa kwa kesi ni daraja kubwa la wananchi kupewa uelewa wa kutambua umuhimu na ubora wa mkataba husika.

Mahakama ni mhimili bora na wenye kutoa majibu ya mambo mengi magumu wanayokutana nayo ili kuweza kupata tafsiri kamili ya masuala hayo kama ilivyojitokeza katika suala la Bandari ambalo Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya kutoa hukumu na kusema mkataba huo ni halali.

Mahakama hiyo ilitoa hukumu yenye kurasa 91 na kusomwa na Mwenyekiti wa Jopo la Majaji watatu wakiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru pamoja wenziwe wakiwemo Mustafa Ismail na Abdi Kagomba kuwa Mahakama imeona mkataba wa Ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kati ya Serikali ya Tanzania na Dubai (IGA) hauna tatizo.

Pia, ilisema pingamizi lililowekwa na walalamikaji waliofungua kesi hiyo halina mashiko kwa kuwa imebaini kwamba mkataba huo haukukiuka vifungu vya katiba na sheria mbalimbali za nchi, ilitangaza kutupilia mbali hoja za upande wa waleta maombi kuwa mkataba huo ulipoka uhuru wa Tanzania kumiliki na kutumia rasilimali asilia bila kuingilia na nchi yoyote.

Kesi hiyo namba 5 ya mwaka 2023, ilifunguliwa katika mahakama hiyo na wananchi wanne ambao ni Alfonce Lusako, Wakili Emmanuel Chengula, Raphael Ngonde na Frank Nyalusi ambapo walifungua kesi dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Wengine waliofunguliwa kesi hiyo mbali ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ni Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, ambapo serikali iliwakilishwa na mawakili wanne wakiongozwa Wakili Mkuu wa Serikali, Mark Mulwambo.

Kwa upande wa walalamikaji au waleta maombi waliongozwa na mawakili wanne wa kujitegemea wakiongozwa na Boniface Mwabukusi ambapo waliwasilisha hoja tisa za kupinga mkataba huo.

Miongoni mwa hoja hizo ni wanasheria hao walidai makubaliano hayo wakidai kuwa ni batili kwa kuwa masharti ya baadhi ya Ibara zake yanakiuka Sheria za Nchi za Ulinzi wa Raslimali na Maliasili za Nchi na Katiba ya Nchi.

Vile vile, wanadai kwamba yanahatarisha mamlaka ya Nchi na usalama wa Taifa na kwamba yaliridhiwa na Bunge kinyume cha utaratibu bila kuwapa nafasi ya kutosha wananchi kutoa maoni yao ambapo hukumu imetoa njia bora na mwafaka ya kueleza ukweli wa jambo hilo na kutoa nafasi kwa mtu asiyeridhika na hukumu basi waende nafasi ya juu.

Hii inatokana na hukumu iliyotolewa na Jaji Ndunguru ilisema Mahakama imeona mkataba wa Ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kati ya Serikali ya Tanzania na Dubai (IGA) hauna tatizo hivyo pingamizi lililowekwa na walalamikaji waliofungua kesi hiyo halina mashiko.

Pia, alisema “Mahakama imekubali kuwa Dubai ina mamlaka ya kuingia mikataba kama hiyo. Walalamikaji hawajaeleza kama Dubai imezuiliwa kuingia mkataba wa ushirikiano wa uwekezaji kwani ni suala la ushahidi,”

Kuhusu kama IGA inakiuka kifungu cha 64 cha Sheria ya Manunuzi, Jaji Ndunguru alisema “Mahakama imeikataa hoja hiyo ikisema IGA ni mkataba wa kimataifa na kwamba katika mkataba huo hakuna manunuzi yaliyofanyika."

Aliongeza; "Kama walalamikaji wakiona TPA (Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari) iliingia katika manunuzi basi walipaswa kuiunganisha TPA katika kesi hii, kwa hiyo hoja nayo Mahakama imeikataa.”

Katika hukumu hiyo, mahakama pia ilijielekeza katika madai yaliyotolewa uamuzi ni pamoja na: Kama ibara ya 2,4 (2)... zinakiuka Ibara namba 1, 8 na 28(1) na (3) za Katiba ya nchi na pia kama IGA ni mkataba kwa muktadha wa Sheria ya Mikataba.

Katika madai hayo mahakama imesema IGA si mkataba unaoweza kusimamiwa na sheria ya mkataba.

Kuhusu kama umma uliarifiwa na kupewa muda wa kutosha kutoa maoni yao mahakama imesema: “mahakama inatambua Ibara ya 63 inaipa Bunge mamlaka ya kuridhia mikataba ya kimataifa kama ilivyo IGA. Mahakama haikubaliani na hoja za waleta maombi katika mazingira ya sasa, njia iliyotumiwa kutoa taarifa kwa mitandao ni sahihi.

“Msimamo wa mahakama ni kwamba Bunge halipaswi kuingiliwa katika utendaji wake wa kazi wa ndani, msimamo ambao umetokana na maamuzi ya kesi mbalimbali za nje.” alisisitiza Jaji Ndunguru katika uamuzi wa kesi hiyo.

Aliongeza “Na hitimisho letu kwamba, licha ya athari za utaratibu lakini tunajizuia kuona kama upungufu huo uliathiri mkataba huo. Mahakama inajizuia kuvuka mipaka yake. Hivyo hoja hii pia mahakama imekataa,”.

Aidha, Jaji Nduguru alisema; “Mahakama inakubali kwamba Ibara ya 20 (1) ya IGA inakiuka Sheria za Ulinzi wa Rasilimali maana inataka hata mikataba itakayosainiwa ya utekelezaji wa miradi migogoro ipelekwe nje."

Alisema "Tumeshangaa kwa nini uandishi huo wa Ibara hiyo. Hata hivyo Ibara ya 22 ya IGA inatoa nafasi ya kufanya marekebisho hivyo kasoro ndogo hiyo haiwezi kuufanya mkataba kuwa batili."

Aliongeza; “Kama baadhi ya ibara zinakiuka mamlaka ya hadhi ya nchi, tafsiri siyo sahihi. Kukiukwa ulinzi na usalama ni tafsiri isiyo sahihi maana Ibara ya 28 inahusu uvamizi wa kivita hivyo tunaikataa,” alisema.

Kwa ujumla, Mahakama iliamua kuwa malalamiko yaliyoletwa na walalamikaji hayana mashiko na tunayatupilia mbali. Kwa hiyo kwa uamuzi huo mkataba wa IGA ni halali. Hukumu hiyo imeweza kuonyesha ukweli halisi wa mkataba huo ambao umekuwa ukizungumzwa muda mrefu.

Sasa ni wakati wa kuwa moja na kuachana na chokochoko au kuleta viashiria vya uvunjifu wa amani kwa kuwa demokrasia bila nidhamu ni fujo, nidhamu bila demokrasia ni udikteta. Jamii inapaswa kuishi kwa kufuata taratibu bora na zenye kuleta mafanikio na maelewano.

Hivyo, onyo la Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP), Camilius Wambura dhidi ya kundi la watu wanaodai kuandaa maandamano nchi nzima, akiwataka kuacha mara moja kwa kuwa wanayotaka kufanya hayana afya kwa taifa katika kuleta maendeleo.

Credit: Hamis Shimye

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: