Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chadema yadai viongozi wao kupigwa, Polisi yajibu

Chademapxm Chadema yadai viongozi wao kupigwa, Polisi yajibu

Wed, 14 Aug 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Chama cha Demokrasia (Chadema) kimedai baadhi ya viongozi wake wakuu walishushiwa kipigo wakati wakikamatwa na Jeshi la Polisi jijini Mbeya kwa nyakati tofauti.

Hata hivyo, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Awadhi Juma Haji akizungumza na Mwananchi jana Jumanne Agosti 13 2024 juu ya tuhuma hizo amesema alishazungumzia mbele ya vyombo vya habari jana Jumatatu hivyo hawezi kuzungumzia tena.

“Siwezi kuzungumzia tena tukio hilo, yote nilishayazungumzia jana katika mkutano wangu na waandishi wa habari na kama kuna suala lingine basi wafuate utaratibu katika kuwasilisha,” amesema Kamanda Haji.

Kwa mujibu wa chama hicho, waliokumbwa na kadhia hiyo ni Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika, Makamu Mwenyekiti (bara), Tundu Lissu na Joseph Mbilinyi maarufu Sugu ambaye ni Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Nyasa.

Leo, Agosti 13, 2024 chama hicho kimedai viongozi hao wanapatiwa matibabu baada ya kufikishwa Dar es Salaam wakitokea mkoani Mbeya.

Hayo yameelezwa na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (bara), Benson Kigaila mbele ya wanahabari, jijini  Dar es Salaam wakati akitoa mrejesho baada ya viongozi wakuu akiwamo mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe na makada wengine kuachiwa huru na Jeshi la Polisi.

Mbowe, viongozi wengine wakuu na makada wa Chadema 520, walikamatwa na kuachiwa huru na Jeshi la Polisi kutokana na madai ya kukiuka zuio la kutofanyika kwa kongamano la maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani inayosheherekewa Agosti 12 ya kila mwaka.

Katika maelezo yake, Kigaila amedai Mnyika, Lissu na Sugu walipigwa wakati wakikamatwa, katika ofisi za Chadema kanda ya Nyasa.

“Walianza kumkamata Lissu waliomburuza na kumrusha katika gari, ndipo Mnyika akahoji kwa nini wanamburuza makamu mwenyekiti.

Amesema mnyika aliitwa na mmoja wa polisi aliyemnyang’anywa miwani yake iliyovunjwa kisha kushushiwa kipigo sambamba na Sugu, “sasa hivi wapo hospitali wakipatiwa matibabu.”

Pia, Kigaila amedai wakati viongozi na wanachama waliokuwa ofisi za kanda Mbeya wanakamatwa, kuna uharibifu ulifanyika ikiwamo wa kuvunja milango ya ofisi hizo na kuchukua simu zilizokuwa zikichajiwa, kompyuta mkapato moja na funguo ambazo hazijarejeshwa.

Kigaila amedai kamera tatu za waandishi wa Chadema Media, Jambo TV na Mwanzo Tv zilichukuliwa na kutaka vifaa hivyo virejeshwe kwa wahusika pasina masharti yoyote.

Kuzungumza Alhamisi Katika mkutano wake na waandishi wa habari, Kigaila amesema Alhamisi Agosti 15, 2024 viongozi hao wakuu watazungumza kwa kina na Watanzania kueleza kilichotokea mkoani Mbeya kisha chama hicho kitatoa msimamo wake na namna ya kusonga mbele.

Jana, Jumatatu Agosti 12, 2024, Kamishna Haji alitangaza kuachiwa huru kwa viongozi hao na baadhi ya makada.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live