Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

CHADEMA yaitwisha mzigo polisi lawama utekaji nchini

Kigaila ED Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA Bara, Benson Kigaila

Thu, 18 Jul 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Siku chache baada ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) Camilius Wambura kukanusha madai ya jeshi hilo kuhusika na kuteka watu, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimeendelea kusisitiza kuwa linahusika.

Jana Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA Bara, Benson Kigaila alinyooshea kidole jeshi hilo kuwa linahusika na utekaji mwanachama wao, Kombo Mbwana (29), aliyetekwa Juni 15, mwaka huu.

Kijana huyo alipotea kwa siku 29 mkoani Tanga, huku ndugu zake pamoja na viongozi wa chama hicho wakimtafuta katika vituo mbalimbali vya polisi bila mafanikio.

Pia alimtaka IGP Wambura kujibu maswali aliyoulizwa katika mkutano wa waandishi wa habari mkoani Tanga, ili kuhakikishia Watanzania jeshi hilo halikuhusika na kutekwa kwa kijana huyo.

"Inawezekanaje Jeshi la Polisi kushikilia mtuhumiwa kwa kosa la matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii bila kufikishwa mahakamani ndani ya siku zote hizo? Na toka mwanzo jeshi lilikataa kuwa halijamkamata mtu huyo.

"Baada ya kukataa, siku 29 baadaye ndipo wanakuja kukubali kuwa mtu huyo wanaye kituoni wanamshikilia kwa kosa hilo. Je, ni sheria gani ya Jeshi la Polisi au Sheria ya Tanzania inayosema hivyo?" alihoji.

IGP Wambura, akiwa ziarani mkoani Simiyu hivi karibuni, alisema kazi ya jeshi hilo ni kulinda na kuimarisha usalama wa raia na mali zao na wala si matendo hayo ambayo limekuwa likihusishwa nayo mara kwa mara.

"Lakini jambo hili limekuwa likielezwa na makamanda wa polisi katika maeneo ambayo ripoti hizo zimekuwa zikitolewa. Kwanza, ifahamike kuwa hatuhusiki na shughuli hizo za utekaji watu.

"Sisi ni jeshi linalolinda usalama wa raia na mali zao. Kwa hiyo, wanaoleta tuhuma za namna hiyo kwetu ni vitendo vya kutukosea adabu," alisema IGP Wambura. Julai 15, mwaka huu, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Zacharia Benard, alithibitisha kushikiliwa kwa mtu huyo na kueleza kuwa anakabiliwa na tuhuma za matumizi mabaya ya mtandao.

Alisema mtuhumiwa huyo anashikiliwa na jeshi kwa tuhuma za kutumia vibaya mitandao ya kijamii katika mikoa mbalimbali nchini na vifaa vya kielektroniki pamoja na laini za simu za mitandao mbalimbali zisizokuwa na usajili wake katika kutekeleza uhalifu huo kinyume cha sheria za nchi.

Alisema upelelezi wa matukio hayo umefika hatua nzuri na mshtakiwa atafikishwa mahakamani, akitoa wito kwa raia kuacha kujihusisha na matumizi mabaya ya mitandao badala yake kuitumia vizuri kwa manufaa yao na  taifa kwa ujumla.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live