Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

CHADEMA, polisi wapimana ubavu

Lissu Mnyika Mbeya CHADEMA, polisi wapimana ubavu

Mon, 12 Aug 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetunishia msuli Jeshi la Polisi na Msajili wa Vyama vya Siasa, kikisisitiza kitafanya kongamano la maadhimisho ya Siku ya Vijana licha ya kuwapo zuio.

Chama hicho kimepanga kufanya maandamano ya amani mkoani Mbeya na kufanya mkutano katika Uwanja wa Ruanda Nzovwe, jijini Mbeya, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani.

Hata hivyo, taarifa iliyotolewa jana na Jeshi la Polisi nchini kupitia kwa Kamishna wa Operesheni na Mafunzo, Kamishna wa Polisi Awadh Haji na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, zilipiga marufuku mkutano wa chama hicho.

Akizungumza na Nipashe jana, Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika, alisema pamoja na makatazo hayo, wataendelea na shughuli yao kama walivyopanga na hawako tayari kuahirisha kongamano hilo ambalo wamefanya maandalizi kwa muda mrefu.

"Katazo la Msajili na Jeshi la Polisi ni ukiukwaji wa sheria za nchi. Kwa hiyo, sisi tunaendelea na maandalizi na kesho (leo) tutaendelea na maadhimisho yetu ya Siku ya Vijana Duniani kama ambavyo tumepanga," alisema Mnyika.

Katibu Mwenezi wa Umoja wa Vijana wa Chama hicho (BAVICHA), Twaha Mwaipaya, alisema wanaendelea na maandalizi na watahakikisha maadhimisho hayo yatafanyika kwa mafanikio kama ambavyo wamepanga.

Alisema kauli zilizonukuliwa na Jeshi la Polisi ni za kwake na kwamba kauli hazina ukomo na hivyo haziwezi kusababisha kongamano kuahirishwa.

"Kama nilifanya makosa kutoa kauli hizo zilizonukuliwa na Jeshi la Polisi na Msajili wa Vyama vya Siasa, basi wangenishikilia mimi lakini si kutumia mwanya huo kuzuia kongamano, kama litaahirishwa basi tutakuwa tumeahirisha sisi lakini si kauli hizo," alisema Twaha.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Mbeya jana, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, CP Awadh Haji alisema jeshi hilo liliamua kupiga marufuku mkutano huo kutokana na matamko yanayotolewa na viongozi wa chama hicho kuashiria uvunjifu wa amani.

Alisema mbali na kupiga marufuku maandamano hayo, pia limezuia mikutano na mikusanyiko ya ndani na nje ya vijana wa chama hicho na kwamba wakikaidi amri hiyo, watashughulikiwa kwa mujibu wa sheria za nchi.

Alisema baadhi ya matamko ya viongozi wa vijana wa CHADEMA yanaashiria kuwa wanataka kufanya vurugu kama ambavyo ilitokea hivi karibuni Kenya ambako vijana walifanya maandamano na fujo katika maeneo mbalimbali.

Alisema kauli zilizotolewa na Katibu Mwenezi wa BAVICHA, Mwaipaya, ziliashiria kuhamasisha vijana kufanya fujo na ndio maana waliamua kuzuia.

"Moja kati ya kauli zilizotolewa na Mwaipaya ni 'kama kijana yeyote unaipenda nchi yako ya Tanzania, umeshalia miaka yako yote, siku ya tarehe 12/08/2024 tunakwenda kuweka hatima ya taifa letu la Tanzania mkoani Mbeya, kwa hiyo kijana yeyote popote Tanzania, njoo Uwanja wa Ruanda Nzovwe Mbeya'. Kauli hizi zinaashiria nia ovu," alisema Kamishna Haji.

Kauli nyingine ambazo zinadaiwa kutolewa na Mwaipaya alinukuu CP Awadh kuwa "Tupo serious sana na jambo hili, kwa hiyo vijana wote CHADEMA kama ambavyo vijana wa Kenya wamejitambua, siku ya tarehe 12/08/2024 tunakwenda kuacha uteja kwa serikali, vijana wa kitanzania na kuweka maazimio makubwa ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu mwaka 2025’.

Kamishna huyo alisema jeshi hilo linashauri vijana wa CHADEMA wa mikoa mbalimbali wanaopanga kwenda mkoani Mbeya kushiriki maadhimisho hayo kuahirisha ili kuepuka alichokiita "kushughulikiwa".

"Kufuatia kauli hizo na matamko mbalimbali yanayotolewa na viongozi hao, Jeshi la Polisi limeamua kupiga marufuku maandamano na mikusanyiko ya aina yoyote ile ya ndani au nje inayotaka kufanyika kwa mwamvuli wa kuadhimisha Siku ya Vijana Duniani, inalenga kuleta uvunjifu wa amani Mkoa wa Mbeya na maeneo mengine yoyote katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

"Hivyo basi, Jeshi la Polisi nchini linatoa onyo kali na katazo kwa mtu au kikundi cha watu kinachojipanga kufanya maandamano na mikusanyiko, kuacha mara moja kwani Jeshi la Polisi lipo imara na limejipanga vizuri kuhakikisha ulinzi, usalama, amani na utulivu vinatawala nchini na lipo tayari kuzuia na kupambana na viashiria vyovyote vya uvunjifu wa amani, na halitasita kuchukua hatua kali kwa mujibu wa sheria kwa mtu yeyote atakayekiuka katazo hili," alisema CP Awadhi katika taarifa yake hiyo.

IRINGA  Mkoani Iringa jana, zaidi ya viijana 150 wa CHADEMA walizuiwa na kuwekwa kizuizini kwa saa kadhaa katika Kituo Kikuu cha Polisi mjini Iringa wakiwa njiani kwenda jijini Mbeya kwa ajili ya kushiriki kongamano la vijana lililoambatana na maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani.

 Vijana hao wa BAVICHA kutoka Kanda ya Kaskazini katika mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro walizuiwa baada ya kuwasili mkoani Iringa eneo la Kihesa, Kilolo, Manispaa ya Iringa kwa kile kinachodaiwa ni maelekezo kutoka juu yaliyolitaka jeshi hilo kuzuia safari ya vijana hao baada ya kubaini kuwapo hali ya hatarishi kwa usalama wa raia.

 Baadhi ya viongozi wa vijana hao, akiwamo Emma Kimambo, walidai wako safarini kwenda mkoani Mbeya kwa ajili ya maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani, lakini walizuiwa kwa madai ya kufanyiwa mahojiano na Jeshi la Polisi na kutakiwa kwenda kituo cha polisi.

 "Sisi tupo safarini kuelekea jijini Mbeya kama vijana wa CHADEMA, sisi siyo wahalifu, bali ni vijana wazalendo tunaelekea kwenye maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani, lakini tumefika Iringa tumezuiwa na Jeshi la Polisi, hatukatai kama kuna changamoto tuambiwe sheria ichukue mkondo wake, tumejaribu kuuliza tumeambiwa ni maelekezo kutoka juu tunatakiwa kwenda kituo cha polisi kuhojiwa," alisema Kimambo.

 Nipashe ilimtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, SACP Allan Bukumbi kutaka kupata taarifa zaidi kuhusu suala hilo bila mafanikio baada ya simu yake kutopatikana.   LISSU, MSAJILI Katika ukurasa wake wa X, Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Tundu Lissu alisema kinachofanyika kuzuia kongamano hilo si sawa kwa kuwa Siku ya Vijana Duniani inasherehekewa duniani kote, akihoji sababu za polisi kuweka zuio.

Jana Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa Tanzania, Sisty Nyahoza, aliwataka viongozi wa CHADEMA kusitisha kongamano hilo.

Barua ya Msajili kwenda kwa Katibu Mkuu wa CHADEMA, Mnyika, inaeleza kuwa kauli zilizotolewa na Katibu Mwenezi wa BAVICHA, Mwaipaya ni ukiukwaji wa Sheria ya Vyama vya Siasa.

“Msajili anawaasa viongozi wa CHADEMA kusitisha shughuli yoyote mliyopanga kufanya siku ya Agosti 12, 2024 Mbeya au mahali popote nchini, ambayo mnajua itasababisha uvunjifu wa sheria, amani na utulivu.

“Maelezo ya Katibu Mwenezi wa BAVICHA katika video hiyo yanakiuka Sheria ya Vyama vya Siasa na yanaashiria mkusanyiko huo unaweza kutumika kuhamasisha vijana kufanya vitendo vya uvunjifu wa sheria kama ilivyotokea Kenya," alisema.

Msajili pia ameelekeza Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe, Katibu Mkuu wake, Mnyika na Mwenyekiti wa BAVICHA, John Pambalu kufika Ofisi ya Msajili, jijini Dar es Salaam kesho Agosti 13,2024 saa 5:00 asubuhi kueleza kuhusu suala hilo. 

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: