Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

CCM wamchangia Lissu Mil. 5 atengeneze gari - VIDEO

CCM Wamchangia Lissu Mil. 5 Atengeneze Gari.png CCM wamchangia Lissu Mil. 5 atengeneze gari

Fri, 16 Aug 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Maelfu ya Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), waliokuwa sehemu ya mkutano mkubwa wa hadhara uliohutubiwa na Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, wamemchangia Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Ndugu Tundu Lissu mamilioni ya fedha ili amudu kutengeneza gari yake anayotumia kwenye shughuli zake mbalimbali.

Hatua hiyo imekuja baada ya kuwepo kwa taarifa mbalimbali, ambazo pia zimewahi kumnukuu yeye mwenyewe Lissu akilalamika kuwa hatendewi haki na anadhalilishwa ndani ya Chama chake hicho kwa yeye kutumia gari moja mbovu, inayombeba pamoja na walinzi wake wanane, huku Mwenyekiti wake Freeman Mbowe akiwa na msululu wa magari 15 ardhini na helkopta angani.

Mchango huo uliofikia shilingi milioni tano, umekusanywa kwenye mkutano huo wa hadhara uliofanyika katika Viwanja vya Furahisha, jijini Mwanza, leo Agosti 15, 2024, ukiwa ni hitimisho la ziara ya siku mbili ya Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Nchimbi, katika Mkoa wa Mwanza, akiwa pia amehitimisha ziara ndefu aliyoanzia Mkoa wa Kigoma, kisha Kagera, Geita na hatimae Mwanza.

Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa (NEC), Ndugu Amos Gabriel Makalla, aliyeendesha shughuli hiyo ya kuchangisha mchango huo, alitangaza kiasi kilichopatikana kuwa ni Sh. 5,320,000, na akaongeza kusema fedha hizo taslimu zitawekwa kwenye akaunti ya benki ya mwanasiasa huyo, baada ya Mchungaji Msigwa kuthibitisha kuwa anayo akaunti hiyo.

Katika ziara hiyo, ambayo pia mafanikio yake imekuwa ni pamoja na kuendelea kurejesha na kuvuna wanachama wa vyama vingine, wanaorejea kujiunga CCM kutokana na kazi nzuri zinazogusa wananchi zinazofanywa na Serikali ya CCM, inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Balozi Nchimbi aliambatana na Katibu wa NEC - Oganaizesheni, Ndugu Issa Haji Usi Gavu, Ndugu Makalla (Mwenezi) na Katibu wa NEC - Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Ndugu Rabia Hamid Abdalla.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live