Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bila cheo Msigwa habaki Chadema

Msigwaaa 017 Mchungaji Peter Msigwa

Mon, 1 Jul 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mchungaji Peter Msigwa, mwenyekiti wa zamani wa Chadema, Kanda ya Nyasa, amechefukwa. Hali ya afya yake kimwili ni njema isipokuwa anapotembea anajisikia kutapika.

Hadi sasa ametapika kiasi bado anasumbuliwa na kichefuchefu. Tunasubiri atapike zaidi, na kwa mtu mwenye kichefuchefu anapotapika na hasa kama ametapika nyongo ndipo hupona, akili na mwili vinakuwa huru.

Kichefuchefu kwa kawaida hutokana na matatizo ya tumbo na hisia za kutaka kutapika. Huenda hali hii ikadumu kwa muda mfupi kisha kurejea mara kwa mara, au ikadumu kwa muda mrefu.

Hali hii huweza kuchochewa na mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na baadhi ya vyakula au harufu, maambukizi ya mfumo wa utumbo, vidonda vya tumbo, aina tofauti za dawa, kula chakula kingi, msongo wa akili, mzio wa vyakula na mengineyo.

Kwa Msigwa, kilichomsababishia kichefuchefu ni msongo wa akili. Anajiuliza hapati majibu ya maana. Ameangushwaje na Joseph Mbilinyi “Sugu” katika uchaguzi wa nafasi ya mwenyekiti Kanda ya Nyasa? Sugu ana umaarufu gani kumshinda yeye? Majibu ya maswali haya ni muhimu ili aweze kuwa na utulivu wa moyo.

Msigwa amepata majibu kwamba ameshindwa kutokana na taratibu za uchaguzi kukiukwa. Baada ya kujiridhisha akakusanya ushahidi wake akakata rufaa kwenye Kamati Kuu ya Chadema.

Hata hatua hiyo haikuweza kuzuia kichefuchefu. Baada ya kukata rufaa kikarudi upya ndipo akaita vyombo vya habari vishuhudie anavyotapika. Kwanza, akatishia ikiwa chama kitashindwa kufanyia kazi rufaa yake, Chadema itakuwa imeshindwa kujitofautisha na chama tawala katika suala la uminyaji wa demokrasia na haki.

Pili, akamrukia mwenyekiti wake Freeman Mbowe, kwamba hawezi kuruhusu kila siku awe anafukuza watu na kubaki yeye. Msigwa anasema ameiona nguvu ya Mbowe katika miaka 20 iliyopita hivyo sasa haimtishi?

Haya yote yamekuja baada ya kuangushwa, tena kwa tofauti ya kura mbili tu; 54 za Sugu na 52 zake. Msigwa angetangazwa mshindi asingepata kichefuchefu. Sasa analalamikia taratibu za uchaguzi, anapinga matokeo, anakishutumu chama na mwisho anatamba amejipanga kupambana na Mbowe katika kinyang’anyiro cha uenyekiti taifa.

Mbowe alichaguliwa kwa mara ya kwanza kushika wadhifa huo, katika uchaguzi wa mwaka 2004 akichukua kijiti kutoka kwa Bob Makani na ndiye ameiweka Chadema katika ramani ya ushindani na CCM.

“Bado naendelea kupokea maoni ya baadhi ya wanachama, viongozi na marafiki zangu. Naamini kwamba Chadema inahitaji mabadiliko makubwa kwa sasa, ili kukabiliana na CCM, katika chaguzi zinazokuja,” anasema.

Msigwa amesema, “Nimeshakomaa. Nimekuwa ndani ya Chadema kwa miaka zaidi ya miaka 20, nikianzia chini kabisa kwenye jimbo. Nimekuwa mbunge, waziri kivuli wa Mambo ya Nje, na Maliasili na Utaalii. Nimekuwa Kamishena wa Bunge na mwenyekiti wa Kanda. Unahitaji uzoefu gani hapo? Mimi ni mwanasiasa  mzoefu na mbobezi na ninayejiamini na misimamo iliyonyooka.”

Msigwa aliyeshindwa uchaguzi wa Kanda anajiona anaweza kushinda ngazi ya taifa. Anakwenda mbali zaidi na kusema hawezi kulamba viatu vya Mbowe. Baada ya kichefuchefu kutulia alionekana kwenye jukwaa la makamu mwenyekiti Tundu Lissu mkoani Singida.

Je, alikwenda kushtaki kwa Lissu ambaye, kikatiba ni mwenyekiti wa nidhamu? Inafahamika katika uchaguzi wa Kanda kulikuwa na makundi na kundi moja ndilo lililompatia Lissu habari kwamba kuna fedha zimemwagwa kuvuruga uchaguzi. Kwa kukimbilia kwa Lissu, anataka kutuambia upande wa waliopokea fedha ndio wameshinda?

Kuaminika kwake Kwanza, Msigwa alikaririwa akisema kushindwa kwake ni sehemu ya demokrasia na hizo ni nafasi za kubadilishana. “Nawashukuru sana viongozi wote wa mkutano huu, kura ndizo zimeamua hivyo mmepata mlichokitaka na nikupongeze Sugu kwa kupata nafasi hiyo, mimi sikuja kwenye chama hiki ili kutaka cheo.”

Pili, aliahidi kutoa ushirikiano. Sasa huyu Msigwa ambaye anapinga matokeo ya uchaguzi huo ni yupi? Sawa, ikiwa kuna taratibu zilikiukwa kupinga matokeo ni sehemu ya demokrasia, lakini huyu Msigwa anayerusha makombora dhidi ya chama hata kabla hakijafanyia kazi malalamiko yake ni yupi?

Sawa, inawezekana ni katika juhudi za kutoa tahadhari, lakini Msigwa anayesema sasa atapambana na mwenyekiti wake Mbowe na hawezi kulamba viatu ni yupi?

Msigwa anataka kutuambia baada ya kukosa uenyekiti ndipo amegundua hakuna demokrasia? Mbona wakati baadhi ya wabunge waliohama wakilalamikia ukosefu wa demokrasia; kukatwa mishahara, kutumika kingono, fedha za ruzuku kutofanya kazi iliyokusudiwa alikuwa kimya?

Mwaka 2017 mshindani wake Patrick Sosopi aliondolewa na Kamati Kuu baada ya mashauriano, hivyo Msigwa alibaki mgombea pekee. Mwaka 2019 mpinzani wake Boniface Mwabukusi alilalamika kuwa Msigwa hakushinda kihalali akahama chama. Kwa kuwa Msigwa “alibebwa” aliona uchaguzi ni huru na haki.

Duniani kote huwezi kutangaza mapambano dhidi ya mwenyekiti wako ukabaki salama. Ni mawili ama utajiuzulu au utafukuzwa. Hajui yaliyomkuta Spika wa Bunge Job Ndugai? Hajui yaliyowakuta wana CCM wengi waliokwenda kinyume na matakwa ya mwenyekiti wao katika uchaguzi mkuu wa 2015?

Baadhi walisimamishwa wengine walifukuzwa; walirejeshwa baada ya kuomba radhi. Kundi lililohamia Chadema likimfuata Edward Lowassa, baada ya kukosa ushindi lilirudi CCM pamoja na kiongozi huyo.

Wana-Chadema walipotaka kurudi CCM ‘waligeuka miba’ kama ya Msigwa. Cecil David Mwambe, mbunge huyo wa zamani Jimbo la Ndanda (Chadema) alipotaka kuondoka alitangaza kupambana na Mbowe. Novemba 26, 2019, alisema anagombea nafasi ya juu ya chama hicho ili kumsaidia mwenyekiti, Freeman Mbowe “ambaye kama binadamu amechoka”.

Baada ya kushindwa Februari 15, 2020 alirudi CCM akidai vyama vya upinzani nchini vina safari ndefu ya kujenga demokrasia ya kweli. Kwamba aliona atakuwa anajidanganya na kuwadanganya wapiga kura wake kubaki katika vyama vya namna hiyo wakati bado anatamani kuwatumikia wananchi wa Ndanda.

Nimkumbushe Msigwa. Katikati ya mwaka 1995, viongozi wa NCCR-Mageuzi ya Augustine Mrema (mwenyekiti) na Mabere Marando (katibu mkuu), walimfuata Mwalimu Julius Nyerere kupata maoni kuhusu uchaguzi mkuu uliotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka ule, naye aliwajibu; “I Can not let my country go to the dogs” (siwezi kuiacha nchi yangu kwa watu wasiofaa).

Nyerere alimpigia debe Benjamin Mkapa hadi akashinda. Bila shaka Mbowe aliyekulia ndani ya Chadema hawezi kukiacha chama katika mikono ya watu wenye kichefuchefu, waliopoteza msimamo wa kimageuzi; mamluki, mapandikizi na walio radhi chama kivunjike wagawane mbao.

Kwa hiyo, Msigwa anaposema hawezi kulamba viatu vya Mbowe maana yake aliyofanya ni sahihi na hawezi kuomba radhi. Wote waliotoa kauli za dharau dhidi ya Mbowe na Chadema – Mwambe, Dk. Vincent Mashinji, Frederick Sumaye, David Silinde na wengineo – walikuwa wamejiandaa kutimkia CCM. Sasa ni zamu yako Msigwa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live