Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Baraza la vyama lampongeza Rais Samia anavyotekeleza 4R

4r Za Samia.png Baraza la vyama lampongeza Rais Samia anavyotekeleza 4R

Thu, 15 Aug 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa nchini Tanzania, Juma Ali Khatibu amesema kazi kubwa ya baraza hilo ni kuishauri Serikali katika mambo muhimu yanayohusu siasa na wananchi, huku akiishukuru Serikali kwa ushirikiano inaouonyesha.

Khatibu ameyasema hayo leo Alhamisi, Agosti 15, 2024 kwenye hafla iliyoandaliwa na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) ya kutoa tamko kuhusu uchaguzi wa Serikali za mitaa 2024.

Tukio hilo limehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa, Serikali akiwemo Naibu Msajili wa vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza huku mgeni rasmi akiwa ni Waziri wa Tamisemi, Mohamed Mchengerwa.

“Tumekuwa na ushirikiano mzuri na Serikali, tulifanya mkutano wetu na Rais Samia Suluhu Hassan alihudhuria kama mgeni rasmi na alipokea changamoto zetu, na mwisho wa siku kuliundwa kikosi kazi kilichofanya kazi kwa muda wa miezi 10.”

“Kuhudhuria mkutano ule na kutusikiliza inaonyesha utayari wa Rais katika kufanya siasa zenye tija kwa nchi yetu na baada ya tukio lile mambo mengi yamefanyika, mikutano ya hadhara ikaruhusiwa, maandamano na mengine yameshafanyiwa kazi,” amesema.

Khatibu katika maelezo yake amesema kitendo cha kuhudhuria viongozi na wajumbe wa baraza katika tukio hilo ni ishara wapo tayari kushiriki uchaguzi wa Serikali za mitaa.

“Tunampongeza Rais Samia kwa kuleta 4R, (4R Maridhiano, Mabadiliko, Ustahimilivu na Kujenga Upya.) tulibahatika kuwa watu wa mwanzo, alituletea wataalamu wakatupatia mafunzo na tunataka nyie watendaji wa Tamisemi nanyi mlipokee,” amesema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Wakuu wa Mikoa Tanzania na Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigella ameipongeza Serikali kwa kushirikisha mchakato huo huku akieleza hali hiyo inaonyesha kuimarika kwa demokrasia.

Shigella amesema katika utendaji kazi wao watazingatia maadili, 4R, sheria na taratibu huku akiwaomba viongozi wa vyama vya siasa kuendelea kuwa na imani nao kama wanaweza kutekeleza majukumu hayo bila tatizo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live