Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Aziza Ally ateuliwa kuwa mbunge viti maalum CCM

Aziza Ally (14).jpeg Aziza Ally ateuliwa kuwa mbunge viti maalum CCM

Sat, 4 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imemteua Aziza Ally kuwa Mbunge wa Viti Maalum wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapunduzi (CCM).

Aziza anateuliwa kushika wadhifa huo, ulioachwa wazi na Bahati Ndingo ambaye kwa sasa ni mbunge wa Jimbo la Mbarali mkoani Mbeya.

Bahati alijiuzulu nafasi ya ubunge wa viti maalum Agosti 17, mwaka huu ili kwenda kuwania ubunge katika jimbo hilo mkoani Mbeya.

Nafasi ya ubunge katika jimbo hilo ilikuwa wazi baada ya aliyekuwa na wadhifa huo, Francis Mtega kufariki dunia Julai 1, mwaka huu kwa ajali ya pikipiki iliyogongana na Powertiller.

Uteuzi huo umetangazwa leo, Jumamosi Novemba 3, 2023 kupitia taarifa kwa umma iliyotiwa saini na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Ramadhan Kailima.

“Uteuzi huo umefanyika baada ya tume kupokea barua yenye kumbukumbu namba CEA.137/400/02a/22 ya tarehe 19, Agosti 2023 kutoka kwa Spika wa Bunge (Dk Tulia Ackson) ikitaarifu tume juu ya uwepo wa nafasi iliyopo wazi ya ubunge wa viti maalum,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Kulingana na taarifa hiyo, uteuzi umefanyika kwa mujibu wa Ibara ya 78(4), ya Katiba ya Tanzania ikisomwa pamoja na kifungu cha 86A (6) na (8) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi sura ya 343.

Hii si mara ya kwanza kwa Aziza kushika nafasi hiyo, amewahi kuwa mbunge wa viti maalum tangu 2005 hadi 2010, aliposhindwa kutetea nafasi yake katika mchakato wa ndani wa chama chake.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: