Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

MenuMichezo
Various Sports

Kiatu cha milioni 3.7 kumbeba Geay Boston

Gabriel Geay Kiatu cha milioni 3.7 kumbeba Geay Boston

Mon, 15 Apr 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mbio za Boston Marathon zinatazamiwa kutimua vumbi leo, Aprili 15 nchini Marekani, huku mwanariadha wa kimataifa wa Tanzania, Gabriel Geay akiwa ni miongoni mwa nyota ambao wanapewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri, akitumia kiatu chenye thamani ya Sh3.7 milioni kukimbilia.

Mbio hizo zitaanza saa 10 jioni kwa saa za Afrika Mashariki, Geay akiwa na kumbukumbu nzuri ya kushika nafasi ya pili mwaka 2023 akitumia saa 2:06:04 nyuma ya Mkenya Evans Chebet aliyeongoza kwa 2:05:54.

Katika kuhakikisha anaendeleza pale alipoishia mwaka jana, nyota huyo ambaye anashikilia rekodi ya taifa ya mbio ndefu kwa muda wa saa 2:03:00 amepanga kuvaa kiatu hicho akiamini ubora wake utamfanya kuendelea kuwatimulia vumbi nyota wenye rekodi za dunia akiwemo Eliud Kipchoge wa Kenya.

Adidas dizero Adios Pro Evo 1, rangi nyeupe yenye michirizi nyeusi ambayo inauzwa Dola 1,474 za Marekani (sawa na takriban Sh3.7 milioni) ndicho kiatu ambacho Geay atavaa.

Akizungumza na Mwanaspoti moja kwa moja kutoka Marekani, nyota huyo amesema maandalizi yake yamekamilika na hakuna tatizo la hali ya hewa, hivyo kilichobaki ni kufanya kile ambacho amekuwa akikifanya mara zote kwa maana ya kushinda na kuipeperusha vyema bendera ya nchi.

"Kila kitu kiko sawa kuanzia kwenye maandalizi na mazingira kwa ujumla. Hata ukiangalia kiatu ambacho nitakitumia cha mdhamini wangu kina ubora mkubwa, naamini nitafanya vizuri," amesema mwanariadha huyo.

"Ili kushinda mbio kubwa unahitaji kuwa na vitu ambavyo vinakuongezea morali mwenyewe mwanariadha ikiwemo viatu vyenye ubora wa kukimbilia. Natarajia nitakimbia vyema japo siwezi kusema nitashinda moja kwa moja, kwani sijui wapinzani wangu wamejiandaa vipi lakini nimefanya maandalizi ya kutosha kufanya hivyo.”

Mwanariadha huyo ambaye alimaliza wa saba katika mashindano ya dunia 2022, ameongeza kuwa kama mambo yatakwenda vizuri jinsi ambavyo amepanga anaamini leo ataipeperusha vyema bendera ya Tanzania kimataifa kwa kuongoza na kuwashinda wababe wa mbio hizo.

“Natambua kutakuwa na upinzani mkubwa kutoka kwa wanariadha wengine, hivyo nimefanya maandalizi ya kutosha kuja kumalizia pale ambapo niliishia mwaka jana," amesisitiza.

Geay ambaye alianza na mbio ndefu za viwanjani (mita 5000 na 10000), baada ya kumaliza Boston Marathon akili na nguvu zote ataelekeza katika marathoni za Olimpiki zitakazofanyika Paris, Ufaransa, Julai, mwaka huu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live