Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

MenuMichezo
Various Sports

Kenya, Ethiopia zapigana vikumbo riadha dunia

Kenyaaaa (600 X 556) Kenya, Ethiopia zapigana vikumbo riadha dunia

Thu, 21 Jul 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Wakati mashindano ya dunia ya riadha yakitimiza siku ya sita huko Marekani, Kenya na Ethiopia zinaendelea kukimbizana katika chati ya medali kwa wanamichezo wa nchi shiriki katika mashindano hayo.

Nchi hizo kila moja imekusanya medali sita hadi sasa zikishika nafasi ya pili na ya tatu nyuma ya Marekani inayoongoza kwa kuvuna jumla ya medali 16.

Licha ya kulingana kwa idadi ya jumla ya medali, Ethiopia iko nafasi ya pili hadi sasa ikibebwa na idadi kubwa ya medali za dhahabu ambazo imekusanya kati ya sita ilizonazo kulinganisha na Kenya ambayo hadi sasa ina medali moja tu ya dhahabu.

Medali tatu za dhahabu za Ethiopia katika mashindano hayo zimechukuliwa na Tamirat Tola aliyeshinda mbio za Marathoni Wanaume, Letesenbet Gidey aliyeibuka kinara wa mbio za Mita 10,000 wanawake na Gotytom Gebreslase aliyeongoza mbio za Marathoni Wanawake.

Mbali na hizo, Ethiopia pia imetwaa medali tatu za shaba baada ya wanariadha wake watatu kumaliza katika nafasi ya pili ambao ni Mosinet Geremew katika Marathoni Wanaume, Lamecha Girma, Mita 3000 kuruka vihunzi na Gudaf Tsegay katika mbio za mita 1500.

Upande wa Kenya, medali yao moja ya dhahabu wameipata kupitia kwa Faith Kipyegon aliyeibuka mshindi wa mita 1500 wanawake na tatu za shaba ambazo zimechukuliwa na wanariadha wake watatu ambao kila mmoja ameshika nafasi ya pili katika mbio alizoshiriki.

Wanariadha hao ambao wameipa Kenya, medali tatu za shaba ni Stanley Mburu, Mita 10,000 wanaume, Hellen Obiri, Mita 10,000 wanawake na Judith Korir katika mbio za Marathoni.

Kenya ina medali mbili za shaba ambazo zimevunwa na Conseslus Kipruto aliyeshika nafasi ya tatu katika mbio za mita 3000 kuruka vihunzi pamoja na Margaret Kipkemboi aliyeshika nafasi ya tatu ktatika mbio za mita 10,000 wanawake.

Uganda wana medali mbili ambazo moja ni ya dhahabu iliyochukuliwa na Joshua Cheptegei aliyeshinda mbio za Mita 10,000 wanaume na nyingine ya Jacob Kiplimo aliyeshika nafasi ya tatu katika mbio za mita 10,000 wanaume.

Nchi nyingine ya Afrika ambayo imepata medali hadi sasa ni Morocco ambayo ina moja ya dhahabu iliyochukuliwa na Soufiane El Bakkali aliyeshinda mbio za Mita 3000 kuruka vihunzi.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz