Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

MenuMichezo
Various Sports

Failuna atimuliwa kambi Madola

541a9062b825d5fee70d1ec08f5b977c Failuna Abdi

Mon, 30 May 2022 Chanzo: www.habarileo.co.tz

Mwanariadha wa kike nyota wa Tanzania wa marathoni, Failuna Abdi ameondolewa katika kambi ya maandalizi ya timu ya Jumuiya ya Madola iliyopo Arusha.

Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Silas Isagi alisema Dar es Salaam juzi kuwa Failuna ameondolewa kambini kwa utoro baada ya kuondoka bila ruhusa.

Alisema kuwa mwanariadha huyo baada ya kushiriki Mbeya Tulia Marathon Mei 2, 2022, hakurudi na kila akipigiwa simu, hapokei.

Isagi alisema kuwa uongozi wa RT ulipokea barua kutoka kwa Kocha Mkuu wa timu hiyo, Suleiman Nyambui kuwa mchezaji huyo hamtaki kwa sababu ya utoro, taarifa ambayo ilikubaliwa na RT.

Mbali na kuondolewa, Isagi alisema kuwa RT watakutana ili kujadili kwa kina suala hilo waone adhabu gani zaidi itatolewa kwa mwanaridha huyo kutokana na kutokuwa mzalendo.

Michezo ya Jumuiya ya Madola itafanyika Birmingham, Uingereza kuanzia Julai 28 hadi Agosti 8 na Tanzania mbali na riadha, inatarajia kupeleka michezo ya ngumi, judo na kuogelea.

Nyambui akizungumzia kambi hiyo alisema kuwa inaendelea vizuri na mwaka huu wanatarajia kupata angalau medali moja ya marathoni kutoka kwa Alphonce Simbu.

Alisema wanaishukuru serikali kwa kuigharamia kambi hiyo, ambapo wamekuwa wakipata posho na mahitaji mengine kwa wakati, hivyo hawana kisingizio.

Chanzo: www.habarileo.co.tz