Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wastaafu tunateseka kupata matibabu

Picha Wazee Data Wastaafu tunateseka kupata matibabu

Tue, 6 Aug 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Licha ya utumishi uliotukuka serikalini, wastaafu wengi hawapati matibabu kwa kuwa hakuna utaratibu maalum uliowekwa.

Licha ya baadhi yao kupata bima za matibabu, wengi wao wanakosa hiyo haki, jambo ambalo ni mateso hasa kwa wazee ambao mara nyingi hukumbwa na magonjwa yasiyo ya kuambukizwa kama shinikizo la damu, kiharusi na kisukari.

Kuna wafanyakazi wachache wenye bahati ya kuishi miaka mingi baada ya kustaafu, kutokana na utunzwaji mwema kutoka kwa familia zao. Matibabu ni gharama kubwa na kwa wakati huo hawana kipato, achilia mbali malipo madogo ya pensheni wanayopata wakiwa wamestaafu.

Matokeo yake jamii imekuwa ikibeba mzigo mzito wa kulea wazee na kama jamii hiyo ni masikini basi, mzigo unakuwa mzito. Mtumishi aliyestaafu ni sawa na aliyekuwa mtumishi wa mfalme ambaye anaendelea kujivunia hadhi hiyo hadi mwisho wa maisha yake kwamba alikuwa na hadhi na heshima aliyokuwa akiipata na ndivyo watumishi wa umma wanapaswa kuwa hivyo.

Faraja aliyokuwa akiipata mstaafu wa mfalme anapomaliza muda wake ni kupewa mali kama ng’ombe, mali na mashamba na endapo atapungukiwa, mfalme angeweza kumwongeza. Kwa watumishi wa umma, wanachokipata ni mafao ya kustaafu kwa mkupuo na baadaye atapewa kidogo kidogo.

Pensheni hii imesaidia sana hasa wakati wa kupumzika, lakini inategemea na mshahara uliokuwa ukiupata. Kama ulikuwa mdogo ni wazi kwamba pensheni yako itakuwa ndogo na isiyoweza kukidhi mahitaji muhimu ya kimaisha kama vile angekuwa akipokea mshahara zamani.

Kama nilivyoeleza kuwa matibabu yanayohusisha vipimo, dawa na ushauri ni gharama kubwa, hivyo hata yale malipo ya kidogo kidogo yanaweza yasitoshe kuwatibu wastaafu.

Hapa ndipo kunakuwa na umuhimu wa kuwafikiria wastaafu na utaratibu wa matibabu, ambao utaandaliwa na kupitishwa kama sheria bungeni ili wanapostaafu wawe na uhakika wa matibabu.

Kwa nchi kama Marekani, Uingereza na Ujerumani wana utaratibu wa kufuatilia hali za kiuchumi za wastafau na kuwaboreshea maisha yao hasa huduma za matibabu. Kwa nini hili linashindikana kwa Tanzania, hasa ikizingatiwa kuwa watumishi hawa walikuwa wakikatwa fedha zao ambazo zilitumika kwenye uwekezaji.

Katika nchi hizo, kada ya ustawi wa jamii ambayo ina jukumu la kuangalia ustawi wa jamii wa wazee, inafuatilia matatizo ya kijamii na kuangalia jinsi ya utatuzi wa matatizo ya wastaafu.

Uzeeni kuna matatizo mengi, aliyekuwa katika utumishi hupaswi kukaa chini muda mwingi bila kazi maalumu na hapaswi kuwa mpweke kwa kukosa marafiki, matokeo yake huishia kuwa na msongo wa mawazo na hatimaye kujijengea mazingira ya vifo vya haraka.

Kuna haja ya Serikali kufikiria upya kuhusu wazee hawa na kuwawekea mpango maalum wa kiafya. Hata hivyo, hilo nalo ni funzo kwa wafanyakazi wengine kuanza kujiandaa na kustaafu.

Haya matatizo hayaji ghafla, kwani kila mfanyakazi anajua kwamba ipo siku atastaafu. Hivyo ni muhimu kujipanga kwa kujiunga na bima za jamii au kuweka akiba maalum itakayomwezesha kupata matibabu siku za usoni.

Kwa wafanyakazi waliojiajiri au wafanyabiashara, hilo nalo wanapaswa kulizingatia, kwani kila mtu ni lazima azeeke na kila mtu atakufa. Ni lazima tutayarishe kesho yetu, sio kwenye matibabu tu, bali pia kwenye miradi ya maendeleo kwa kuwekeza kidogo kidogo.

Wastaafu pia wajiunge kwenye vikundi vya uzalishaji mali ambavyo wanaweza kusaidiana wao kwa wao na kutiana moyo ili kuepuka msongo wa mawazo. Wafanyakazi nao ama wazazi na walezi wanapaswa kuitayarisha jamii ili wanapostaafu iwe rahisi kuhudumiwa. Walee watoto kwa kuwapa elimu na maarifa.

Jamii nayo inapaswa kupokea jukumu la kuwatunza wazee kwa kuwapa matibabu. Kuwe na utaratibu wa wanafamilia kuchangishana au kuwaweka wastaafu katika idadi ya wategemezi katika bima za afya.

Kama ni semina, mikutano na taratibu nyingine vimeshafanyika sana kuhusu uboreshaji wa afya kwa watumishi wa umma ambao ni wastaafu.

Lakini mpaka sasa sioni utekelezaji wowote. Kama tulivyowajali waipokuwa watumishi hodari kazini, tuwakumbuke na sasa walipo nje ya utumishi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live