Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ummy aanika sababu ya uhaba mkubwa watumishi afya vijijini

Ummy 7c676d638 Ummy aanika sababu ya uhaba mkubwa watumishi afya vijijini

Tue, 30 Jul 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, amesema kuna uhaba wa watumishi wa afya kwa zaidi ya asilimia 50, huku maeneo mengi yakiwa ni ya pembezoni, ambako watumishi wengi wanaomba na wanahitaji kubaki mijini.

Alisema hayo jana wakati akifungua kongamano la siku tatu la kumbukizi ya Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, lililoandaliwa na Taasisi ya Benjamin Mkapa (BMF) na kukutanisha wadau kutoka sekta ya umma, binafsi na mashirika yasiyo ya kiserikali.

Wadau hao wamekutana kujadili kwa pamoja changamoto zilizoko katika sekta hiyo na mafanikio waliyonayo katika utoaji wa huduma.

Waziri Ummy alisema kupitia kongamano hilo, pia wanategemea kupata maoni na ushauri wa wadau katika kutengeneza Mkakati wa Sita wa Taifa wa Sekta ya Afya 2026/31 huku ukiendana na kukamilika kwa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Alisema changamoto kubwa hivi sasa wanayokabiliana nayo katika sekta hiyo ni rasilimali watu ya watumishi na suala la ugharamiaji wa huduma za afya.

“Hali ya watumishi wa afya, tunauhaba wa watumishi wa afya zaidi ya asilimia 50. Mnaweza kusema Waziri mbona kila siku (takwimu) inapanda haipungui.

“Hii ni kwa sababu tumejenga sana zahanati, vituo vya afya, hospitali za wilaya na kuanzisha huduma za kibingwa kwa hiyo naona uhaba wa watumishi wa afya ipo zaidi ya asilimia 50 kwa sasa na changamoto kubwa ipo ngazi za chini katika zahanati, vituo vya afya na hospitali za wilaya,” alisema.

Ummy alisema wanamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan ambaye kila mwaka amekuwa akitoa vibali vya kuajiri na sasa wizara hiyo pamoja na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma (UTUMISHI), wametangaza nafasi za ajira ambazo idadi yake hakuitaja.

Alisema changamoto wanayokutana nayo ni kwamba uhaba uko mikoa ya pembezoni na watumishi wanaoomba na wanawahitaji wengi kubaki maeneo kama Dar es Salaam, Mwanza, Arusha na Dodoma.

“Ni changamoto tunayopambana nayo na nimeongea na Waziri mwenzangu Mohamed Mchengerwa kwamba, tutasema wewe unapaswa kwenda Halmashauri ya Uvinza ambako kuna uhaba mkubwa wa watumishi. “Tumejifunza hili kupitia Taasisi ya Benjamin Mkapa Foundation wanapeleka watumishi Uvinza. Mazingira ni mazuri na miundombinu imeboreshwa.

“Niwatoe wasiwasi watumishi kutoogopa kufanya kazi maeneo ya pembezoni kwa kuwa huduma zote muhimu zipo na TAMISEMI wamekwenda mbali sasa wanajenga huko mpaka shule za mchepuo wa Kiingereza zikiwamo halmashauri za vijijini,” alisema.

Kuhusu mchango wa Hayati Mkapa katika sekta hiyo, Waziri Ummy alisema alikuwa mmoja wa vinara wa kuhakikisha Watanzania wanapata huduma bora na mambo mengi ya sekta hiyo yalianzia kwake ikiwamo Sheria ya Bima ya Mfuko wa Taifa wa Afya (NHIF) iliyoasisiwa na kubuniwa mwaka 2000 na sasa inahudumia mamia ya watu.

Pia alisema kwa sasa NHIF imekuwa chanzo kikubwa cha mapato ya hospitali za umma na binafsi ana takriban asilimia 50 yanayotokana na huduma zinazofadhiliwa na mfuko huo.

Kuhusu Taasisi ya Benjamin Mkapa Foundation, waziri huyo alisema moja ya kazi kubwa inayofanya ni masuala ya rasilimali watu katika afya na kusaidia kuajiri wataalamu wa afya hususani maeneo ya pembezoni.

Pia alisema wamekuwa wakitoa mkataba wa miaka mitatu kwa wataalamu ambao baada ya muda wanapozoea mazingira husika, serikali kuwaingiza katika ajira rasmi.

Mkurugenzi wa Programu na Ukuaji wa Taasisi hiyo, Rahel Sheiza, alisema yako mambo mengi sekta mtambuka yanayoathiri ukuaji, upatikanaji na utendaji wa watumishi.

Pia alisema kupitia kongamano hilo pamoja na mambo mengine wanajadili ukuaji wa teknolojia, mabadiliko ya tabianchi, uhusishwaji wa sekta binafsi, haja ya utendaji na uwajibikaji.

Alisema katika sekta ya rasilimali watu pamoja na kuangalia uhaba wa zaidi ya asilimia 50 ya watumishi, kuna uhaba zaidi wa kinadharia na kuendana na mabadiliko ya kitaifa na kimataifa ili kupata watumishi wenye tija, stahiki na wavumilivu.

Alisema taasisi hiyo kwa zaidi ya miaka 18 imejikita kuongeza nguvu kwa kuhakikisha kuna upatikanaji wa watumishi wa afya ambao si tu kwa namba bali pia, sifa na utendaji kazi.

Alisema hadi sasa wameajiri watumishi 5,200 katika maeneo yenye changamoto, kujenga nyumba 480, kutoa mafunzo na kuongeza nguvu ya rasilimali fedha.

Katika kongamano hilo baadhi ya washiriki wakimamo mabalozi, wameeleza umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa na uwekezaji katika bima ya afya, ili kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi na matumizi ya teknolojia katika kutoa huduma.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live