Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simulizi maduka dawa kuuza bidhaa zilizoishia muda mtaani

Pharmacy Duka La Dawa Simulizi maduka dawa kuuza bidhaa zilizoishia muda mtaani

Thu, 30 May 2024 Chanzo: Nipashe

Kukosekana elimu ya kutambua bidhaa ya dawa za binadamu zilizokwisha muda wake wa matumizi hasa za kumeza, kunalalamikiwa kusababisha watumiaji kuwa hatarini kiafya na kupata ugonjwa sugu, wahanga wakubwa ni wanawake na watoto.

Dawa zinazotolewa kwa njia ya sindano pia si salama kuzitumia baada ya kuisha muda kwani zinaweza kusababisha madhara makubwa kwani vijidudu kama fangasi na bakteria, huweza kuota kwenye dawa hizo zenye asili ya majimaji na kuleta madhara makubwa zaidi endapo wataingia mwilini.

Kutokana na ukubwa wa tatizo hilo, Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), imekuwa ikifanya ukaguzi wa kila mara katika maduka ya dawa za binadamu, lengo ni kudhibiti dawa zilizokwisha muda wake wa matumizi zisiendelee kusambaa mitaani na wanaobainika kuuza, wanachukuliwa hatua za kisheria.

Katika Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, ,wakazi walikuwa wakilalamika kuuziwa dawa katika moja ya duka la dawa lakini walikuwa hawaponi magonjwa wanayoumwa, hatua iliyowafanya kupaza sauti mpaka TMDA ilipofika na kubaini kuwepo dawa zilizokwisha muda wa matumizi.

Mkaguzi wa TMDA, Venancy Burushi anasema wamekuwa wakifanya ukaguzi wa maduka ya dawa mara kwa mara ili kupambana na dawa zilizokwisha muda zisiendelee kutumiwa kwani zinamadhara makubwa na zinasababisha mpaka kifo.

Anasema, kuuza dawa zilizokwisha muda wake wa matumizi ni kwenda kinyume na Kifungu Namba 76 cha Sheria ya Dawa na Vifaa Tiba na kuna baadhi ya dawa kama kundo la antibaiotiki, hugeuka kila bada aya muda wake wa matumizi kuisha na kusababisha matatizo kwenye figo.

Burushi anasema, dawa mara nyingi hubaki na uimara wake inapotunzwa sehemu salama hasa kwenye ukavu, yenye ubaridi baridi na mbali na joto au mwanga wa jua, zinapotunzwa nje ya mazingira hayo zinaharibika na kutengeneza sumu ndio sababu yakuwa wanakagua mara kwa mara maduka.

Burushi anasimulia atika mtaa wa Mwine Manispaa ya Kahama wamemkamata mfanyabiashara (jina tunalo) akiuza dawa za binadamu zilizokwisha muda wa matumizi na kujipatia fedha pasipo halali, huku wananchi wakilalamika kutopona wakitumia dawa hizo.

Anazitaja dawa hizo kuwa ni pamoja na Tinidazole, Good Morning na Cafenol, zilizokuwa zimekwisha muda wake wa matumizi, lakini mmiliki wa duka akaendelea kuwauzia wananchi, huku akijua ni kosa kisheria.

"Dawa zote hizi tulizozikamata zimeghushiwa muda wa matumizi, ambazo zipo zinaoonesha zimekwisha matumizi Desemba mwaka 2023 na zingine zimeongezwa muda wa matumizi na ambazo zinatakiwa kwsha Septemba 24 mwaka huu, ila zimeongezwa muda hadi Oktoba Mwaka 2025,” anasimulia Burushi.

Meneja wa TMDA Kanda ya Ziwa Magharibi Dk. Edgar Mahundi, anasema dawa zote zilizokamatwa zimethaminishwa na gharama yake ni Sh. Milioni tano na kama zingeuzwa kwa binadamu zingeleta madhara makubwa, ikiwamo kupata tatizo la usugu wa dawa mwilini.

Aidha, anasema watamfungulia mtuhimiwa waliomkamata, mmiliki wa duka hilo, kwa kukiuka sheria za uuzaji dawa za binadamu, kwani kitendo cha kuuza dawa bandia au zilizokwisha muda wake ni kinyume cha sheria, akisisitiza madhara yalivyo, mtumiaji anaweza kupata madhara usugu wa dawa mwili, kupooza viungo au kifo.

Mahundi anatoa onyo kali kwa wafanyabiashara wa dawa za binadamu kuacha udanganyifu kwa kucheza na maisha ya binadamu kwa kuuza dawa zilizokwisha matumizi na TMDA haitawavumia.

Hapo anaahidi atahakikisha wanafikishwa mahakamani wote watakaobainika, akiwataka wananchi kuangalia muda wa matumizi wa bidhaa wanayonunua.

MAONI WANANCHI

Mkazi wa Mtaa wa Mwime Hassan Said anasema, kutokuwa na elimu ya kutambua bidhaa zilizokwisha muda wake wa matumizi hasa dawa za binadamu zinasababisha kuwa na usugu wa maradhi wanayoumwa mara kwa mara na wamekuwa wakigundua pale wanapofika vituo vya afya na hospitali na kuonyesha dawa walizotumia.

Anasema, baadhi yao wanalazimika kukimbilia kwa waganga wa jadi kupata matibabu kiasili, huku wakiwa hawatambui kuwa wanahatarisha usalama wa maisha yao kwani ugonjwa wa malaria na hautibiwi kwa wakunga jadi, hali inayowasababisha wanatumia dawa za kizungu lakini hawaponi wala kupata unafuu wowote.

Saidi anasema, wiki mbili zilizopita ndugu yake alidhurika kwa kupewa dawa katika maduka mtaani na ilipofuatiliwa, muuzaji katika duka la dawa alikuwa mkali, lililowaumiza na kutoa taarifa kwa Mwenyekiti wa Serikali Mtaa, kwa hatua zaidi.

Aika Samweli, anasimulia “Mwezi wa Kwanza mwaka huu (Januari), niliugua sana na mara baada ya kupima nilibainika kuuzwa malaria na UTI. Nilitumia dawa ndani ya wiki nzima sikuweza kupata unafuu wowote...”

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mwime, Dogo Mhenziwa, anasema ofisi yake imekuwa ikipokea malalamiko ya wananchi kuuziwa dawa zilizokwisha muda na wanazitambua, kwa malalamiko ya watu kutopata nafuu au kupona.

Sasa anaiomba serikali kutoa elimu ya namna ya kuzifahamu bidhaa zilizokwisha muda wake wa matumizi ili kuondoa madhara yasiyo na ulazima.

Anasema, wamekuwa wakishuhudia makundi maalumu mbalimbali yakipewa elimu ya kutambua bidhaa kama fedha bandia, hivyo basi nguvu kama hiyo ifikie wananchi kwa kuelimishwa na kutambua bidhaa feki kupitia vyombo vya habari na mikutano ya hadhara inayofanyika.

Mhenziwa anaeleza, mtaani kwake kunamiliki wa duka mmoja amekuwa akikamatwa na polisi mara kwa mara kwa tuhuma za kuuza dawa zilizokwisha muda wake wa matumizi lakini amekuwa akifika kituo na kuachia na ninadhani ni kwa sababu hata polisi hawana elimu ya kuzitambua bidhaa hizo.

Chanzo: Nipashe