Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Profesa Janabi aibuka na walaji wa nyama choma

Profesa Janabi Muhimbili A06091 Profesa Janabi

Fri, 28 Jun 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Matumizi ya chumvi yaliyopitiliza yametajwa kuwa chanzo cha magonjwa yasiyoambukiza kwa wananchi wengi wa Mkoa wa Arusha, ikiwemo kiharusi, shinikizo la juu la damu, figo, na magonjwa ya moyo.

Mkoa huo umetakiwa kuchukua hatua za haraka kudhibiti kiwango kikubwa cha shinikizo la juu la damu linalowakabili wananchi wengi.

Hayo yamesemwa jana Alhamisi, Juni 27, 2024, na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Profesa Mohamed Janabi, alipozungumza na wananchi waliojitokeza katika viwanja vya Sheikh Amri Abeid, kwenye kambi maalumu ya madaktari inayoendelea.

Profesa Janabi amesema amefika mkoani Arusha kwa nyakati tofauti katika Hospitali za Selian, Hospitali ya Rufaa ya Mount Meru, na sasa kwenye kambi hiyo ambako wagonjwa waliopimwa shinikizo la damu wana matokeo ya 180 kwa 110.

Amesisitiza umuhimu wa kushirikiana na mganga mkuu wa mkoa huo kuhusu suala hilo.

“Presha za Arusha ni 180/110, na nafikiri nitashauriana na mganga mkuu wa mkoa. Hisia yangu ni kuwa mnatumia chumvi nyingi sana kwenye nyama,” amesema na kuongeza:

“Chumvi inatoa maji yaliyokuwa ndani na kuyaingiza kwenye mzunguko wa damu na hivyo kusababisha presha kupanda. Presha za Arusha zinatia wasiwasi; kama hatutachukua hatua za makusudi, magonjwa ya moyo, kiharusi, na figo yatakuwa makubwa,” amesema Janabi.

Mkurugenzi huyo amesisitiza umuhimu wa chakula bora, akieleza kuwa kinaweza kumjenga mtu au kuwa chanzo cha maradhi.

Ameitaka jamii kuepuka kula hovyo na kupunguza matumizi ya pombe, ambayo yanachangia vifo vingi kutokana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza.

“Ukila vibaya chakula kitakupeleka kubaya. Kwa mfano, mtu amekunywa chai asubuhi, lakini akifika hapa uwanjani akimuona mtu anakula karanga atanunua. Ikifika saa saba ataenda kula, hata kama hana njaa,” amesema Profesa Janabi.

Ameongeza kuwa watu wakirudi kwenye nidhamu ya kula, chakulak itawasaidia kuepuka magonjwa hayo.

“Anza taratibu, kula asubuhi, kisha katikati kunywa maji, njoo ule mchana na ule jioni. Hii itakinga afya yako. Ukifanya kinyume chake, utapata kitambi na siku moja utashangaa una presha na tatizo la moyo. Hii ni nidhamu ya chakula, hakuna kitu kingine,” amesema.

Kwa upande wake, Mratibu wa Tiba Mkoa wa Arusha, Charles Migunga, amesema wamepokea madaktari 50 kutoka mikoa ya Dodoma, Singida, Manyara, na Kilimanjaro.

Amesema Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, amewasiliana na mganga mkuu wa Serikali kumuomba kuongeza madaktari katika mkoa huo na tayari wameshafika.

"Kulingana na idadi ya watu inayoongezeka kila siku, ili tuweze kuwahudumia vizuri, tuliomba kuongezewa madaktari na tayari wameshafika na kuanza kutoa huduma. Mwitikio bado ni mkubwa na tumeongeza mahema matano kwa ajili ya kutolea huduma," amesema Migunga.

"Tunaamini huduma itaendelea kwa kasi ukilinganisha na siku zilizopita. Wananchi waendelee kujitokeza na tutawahudumia vizuri hadi kuhakikisha wanapata dawa."

Chanzo: www.tanzaniaweb.live