Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Prof. Janabi ataja sababu wanaoshindwa kufunga mlo

Profesa Janabi Muhimbili Prof. Mohamed Janabi.

Tue, 20 Aug 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Tofauti za miili kati ya mtu mmoja na mwingine, ni moja ya sababu zisizoweza kuwalinganisha hasa inapotokea suala la kufunga kula huku mwingine akistahimili na mwingine kushindwa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Prof. Mohamed Janabi, anasema miili inatofautiana namna inavyofanya kazi kutokana na namna ilivyoundwa (jenetiki).

Bingwa huyo katika magonjwa ya moyo, anafafanua hayo katika kitabu chake ‘Mtindo wa Maisha na Afya Yako, akieleza sababu sita kwa nini wengine wanashindwa kufunga.

Anasema tofauti hizo za miili pia na mazingira mtu anapoishi, hali ya hewa, aina ya kazi unayofanya na aina ya chakula na mapokeo yake katika mwili ni sababu za wengine kushindwa kufunga.

“Matokeo ya afua kama za kufunga yatakuwa tofauti hata kama watu wawili watafanya afua moja kwa usahihi wa asilimia mia moja. Kuna watu ambao huchakata hifadhi ya chakula kwa haraka na wale wanaochakata taratibu.

“Ni vyema kujifunza mwili wako ni wa aina gani na ni matokeo gani ungeyataka. Wako watu wanaojaribu kufunga lakini kutokana na sababu mbalimbali zinazotokana na utaratibu wa ufungaji, hujikuta wakishindwa kuendelea kufunga, hivyo huacha,” alisema bingwa huyo wa tiba ya moyo.

Alitaja sababu zingine za kushindwa kufunga kuwa ni pamoja na kupungua uzito kupita kiasi. Anasema wako wanaopoteza uzito kwa kiasi kikubwa, hivyo huona kuwa hayakuwa malengo yao kuwa wembamba hivyo.

“Kwa hiyo wanakuwa na wasiwasi, wanaacha kuendelea na utaratibu wa kufunga. Hawa pia huenda ni kundi lile la wale wanaochakata mfumo wa chakula kwa haraka.

“Yaani kwa jitihada ndogo wanaweza kupungua kwa kasi sana. Pia ikumbukwe kuwa kupungua uzito kuliko inavyotakiwa kunasababisha utapiamlo ambao nao ni ugonjwa,” anasema.

Prof. Janabi anataja sababu nyingine ya watu wengine kushindwa kufunga kuwa ni kutopungua uzito. Anasema kwa watu ambao matarajio yao hayafikiwi, kwa maana ya muda ambao walidhani wangekuwa wamepunguza uzito wa mwili, lakini matokeo yanakuwa kinyume chake.

“Mara nyingi kundi hili ni la wale ambao wako kwenye shinikizo la makundi kama kwenye mitandao ya jamii kwamba kuna uwezekano wa kupunguza uzito ndani ya muda mfupi. Sasa wanapoona kwamba matarajio yao hayakufikiwa, wanakata tamaa na kuacha kuendelea kufunga,” anaongeza.

Sababu nyingine, kwa mujibu wa Prof. Janabi, ni uzito kupungua kwa taratibu mno. Anasema wako watu ambao matokeo ya kupungua uzito hutokea taratibu sana.

“Hali hiyo huwakatisha tamaa kwa kuwa walitarajia matokeo ya haraka ya kupunguza uzito. Wanapoona hali hiyo, hupoteza uvumilivu na hivyo kuachana na utaratibu wa kufunga. Aina hii huenda ni wale wanaochakata taratibu na wanahitaji muda na jitihada zaidi kufikia lengo,” anabainisha.

Prof. Janabi pia anasema kupanda na kushuka kwa uzito ni sababu za baadhi kushindwa kufunga, wakiwamo watu ambao kutokana na kufunga, wanapata hali mchanganyiko ya kupungua na kuongezeka uzito.

“Hali hii inawakatisha tamaa kwa sababu wanaona malengo yao ya kufunga hayafikiwi, hivyo huamua kuacha kuendelea na utaratibu wa kufunga.

“Kama nilivyosema awali, mwili unayo namna ya kujisahihisha. Afua ya kufunga ikizoeleka, mwili unaweza kutafuta namna ya kujilinda na kujirejesha katika hali iliyojizoesha ndio maana kufunga kwa vipindi na sio moja kwa moja ni muhimu zaidi kama afua ya afya,” anasema na kuongeza kuwa mwili pia unaweza kushindwa kuhimili madhara ya kufunga.

“Binadamu wanatofautiana jinsi miili yao inavyopokea hali ya kufunga. Wapo wanaopata madhara kama ya kuumwa tumbo, kutapika, au kuumwa kichwa na mengine.

Kutokana na hali hii, kufunga kwao kunageuka kuwa kero na kuwaharibia utulivu wa maisha na afya zao. Hawa nao huamua kuachana na utaratibu wa kufunga. Pia anasema watu hao hushindwa kuhimili njaa kali, akisema hiyo ni dhahiri kufunga kula huambatana na njaa na hisia za zinapokuja mwili unatoa ishara ya kutaka chakula.

“Sasa wako watu ambao hawahimili kukaa na njaa au kuwa na njaa kali sana kiasi cha kuwafanya washindwe kuivumilia. Matokeo yake huona kuendelea kufunga ni kama adhabu ambayo haina maana kwao. Hivyo, watu hawa huacha kufunga na kuendelea na utaratibu wa kawaida,” anasema.

Prof. Janabi aanasema wataalamu wanapozungumza kuhusu ulaji bora wenye afya, haimaanishi kukataza watu kula.

“Tunasema katika utaratibu wa ulaji wako ndio unasababisha kuwa na kiwango cha juu au cha chini cha insulini mvwilini. Kama ambavyo tumeona, ongezeko insulin ndiyo kichocheo cha kuongezeka kwa uzito wa mwili. Katika utaratibu wa ulaji wa chakula tunapaswa kujua vitu muhimu.

“Unakula mara ngapi kwa siku; Unakula mchanganyiko gani wa chakula?; Unakula saa ngapi na kiasi gani?; Unakula muunganiko na mgawanyiko wa aina gani ya chakula kama wanga, protini, au mafuta,” anasema.

Mambo haya, anasema ndiyo yanaamua kama insulin mwilini itakuwa nyingi au la kulingana na kasi ya kuwapo chakula tumboni, kama ulaji ni wa mara kwa mara basi insulin nayo inakuwa nyingi na kubadili chakula hicho kuwa mafuta ili kihifadhiwe.

“Katika mchakato wa kuzalishwa kwa insulin nyingi kutoka kwenye kongosho, kunasababisha hali va ukinzani wa insulini ambao husababisha uzito wa mwili huongezeka.

Kisayansi, binadamu amepitia hatua mbalimbali za mabadiliko. Mabadiliko mbalimbali tuliyopitia mpaka sasa, matokeo yake binadamu wa zamani hawakuwa na tatizo la uzito. Uzito umeletwa na mabadiliko ya tabia ya ulaji,” anasema Prof. Janabi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live