Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Muhimbili kuja na matibabu ya misuli kwa njia hii...

Muhimbili Langooo.jpeg Muhimbili kuja na matibabu ya misuli kwa njia hii...

Tue, 30 Apr 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila kwa kushirikiana na Chama cha Wataalamu wa Magonjwa ya Mishipa ya Fahamu imeandaa mafunzo ya siku mbili ya matibabu ya magonjwa ya fahamu yanayoathiri misuli kwa kutumia sindano maalumu (botox).

Akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili-Mloganzila, Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Upasuaji Mloganzila, Dkt. Godlove Mfuko amesema mafunzo hayo yanatolewa kwa mara ya kwanza hapa nchini na yamehusisha wataalamu wanaoshughulika na magonjwa hayo.

Dkt. Mfuko ameongeza kuwa mafunzo hayo yanatolewa na Mkufunzi Mbobezi kutoka Senegal ambapo baada ya mafunzo hayo kwa mara ya kwanza huduma hizo zitapatikana hapa nchini, hususani Hospitali ya Mloganzila.

“Mafunzo haya ni muhimu sana hapa kwetu kwa kuwa tunao wataalamu wa kada mbalimbali wenye weledi na utaalamu wa ubobezi kabisa duniani, vifaa tiba na mashine za uchunguzi zinazotumia teknolojia ya hali ya juu,” amebainisha Dkt. Mfuko

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Madaktari wa Mishipa ya Fahamu, Prof. Williama Matuja amesema matibabu hayo yanatolewa kwa kuchoma sindano ndogo (botox) mgonjwa mwenye changamoto za mishipa ya fahamu inayoathiri misuli, ambapo wameanza kwa kuwapa mafunzo wataalamu ikiwa ni maandalizi ya kutoa huduma hiyo nchini.

Mafunzo hayo yamehusisha madaktari bingwa wa mishipa ya fahamu, misuli na ubongo; madaktari wa magonjwa ya ndani na madktari wanafunzi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live