Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Maeneo haya hatari kwa afya yako

Mwili Afya.jpeg Maeneo haya hatari kwa afya yako

Fri, 12 Jul 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mtaalam wa Usikivu, Kizunguzungu, Matamshi na Lugha Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Fikiri Idd, ametoa tahadhari kwa wananchi wanaoishi katika maeneo yenye kelele, akiwataka kuvaa vifaa maalum ili kupunguza athari za usikivu.

Katika mazungumzo na Nipashe jana katika banda la MNH kwenye Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam (DITF), maarufu Sabasaba, mtaalamu huyo alibainisha umuhimu na uwezo wa sikio katika usikivu unavyopungua kadri umri unavyosonga.

Alishauri wanaotembelea maeneo kama Soko Kuu la Kimataifa Kariakoo, jijini Dar es Salama na maeneo mengine yenye kelele, wavae vifaa maalum alivyovitaja kwa jina la 'ear plug na ear muffs’ ili kupunguza athari.

Mtaalamu huyo pia alieleza umuhimu wa kiungo sikio kuwa ni miongoni mwa milango mitano ya fahamu, ikisaidia mwili kuwa na uwiano, kuimarisha matamshi, lugha pamoja na kuzuia mtu kuondokana kutokana na kizunguzungu.

Alisema katika maonesho hayo wanatambulisha huduma mpya ya kuwafanyia uchunguzi watoto tangu siku ya kwanza hadi mwezi mmoja, ili kubaini wenye changamoto waanze kupata tiba.

Idd alisema wazazi na walezi walio na watoto wenye changamoto ya usikivu huwafikisha hospitalini hapo wakiwa katika hatua ya juu ambayo ni nadra kurejesha usikivu wao.

"Kama ana shida ya usikivu, tukimgundua mapema tutamwekea kipandikizi, ambacho kitamsaidia kuwa na usikivu kwa asilimia 90. Changamoto ni kwamba watoto wanaletwa wakiwa na miaka sita au saba anakuwa ameishi na tatizo hili miaka yote hiyo.

"Tumegundua kwamba kama hospitali, kukabili changamoto ni kusaidia jamii kuanza uchunguzi wa mtoto anapozaliwa tu," alisema. Idd alisema matibabu ya usikivu ni ghali na vifaa huagizwa nje ambapo kifaa kimoja hufikia hadi Sh. milioni 70. Serikali huchangia gharama za matibabu hayo.

"Serikali imechangia Sh. bilioni 2.6 kwa ajili ya vifaa hivyo. Lakini fedha hizo ni kwa ajili ya kuleta kifaa, bado matibabu ya kukiweka kwa mtoto, ni lazima mtu achangie," alisema Idd.

Mtaalamu huyo alisema kuwa watoto wanaochunguzwa kabla ya kufikisha miaka mitano, husaidia kuondokana na ukubwa wa tatizo kama vile kushindwa kutamka maneno na sauti isiyo na mawimbi.

Idd alishauri jamii kujenga utamaduni wa kufanya uchunguzi angalau mara moja au mbili kwa mwaka kwa kuwa kiwango cha tatizo la usikivu kinakua. Alisema katika kliniki ya Muhimbili, kila siku hospitali hiyo imekuwa inapokea takriban watu 20 wenye matatizo hayo.

"Takwimu za mwaka 2023, utafiti unaonesha watu milioni 432 walipata tatizo la usikivu duniani kote na kati yao, milioni 34 ni watoto," alisema na kubainisha kuwa kundi kubwa ni watu wazima kwa kuwa hupuuzia jambo hilo.

"Hutakiwi kuingiza chochote masikioni hata pamba. Ndani ya sikio kuna nta inayozalishwa maalum kwa ajili ya kusafisha. Inaposogea nje ndio utumie kitambaa kujisafisha.

"Ear phone (spika za masikioni) ni sababu kubwa. Mfano, mtu kapanda daladala au bodaboda, kavaa ‘ear phone’ na ili asikie lazima aweke sauti kuzidi mngurumo wa chombo alichopanda au redio iliyoko ndani ya gari.

"Nenda Kariakoo, utagundua ghorofa moja kila duka kuna jenereta lake, bado muuzaji wa sumu ya panya ana spika yake, mwuzaji viwanja ana spika yake, mpigadebe hivyohivyo. Ukipima kiwango cha kelele pale ni kikubwa, huwezi kugundua ila utaathirika taratibu.

"Mfano, mwingine hapa tulipo (Sabasaba), hatuko  mbali sana na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), lakini ndege ngapi zimepita na haujazisikia milio yake? Kwa sababu hapa kuna kiwango kikubwa cha kelele ndio maana hausikii chochote," alifafanua mtaalamu huyo.

Idd alisema ili kuepuka hali hiyo, vipo vifaa ambavyo watu wanaweza kuvitumia kupunguza kiwango cha kelele na kuondokana na athari zake.

Alisema Shirika la Afya Duniani (WHO) linakadiria kuwa, ifikapo 2050, watu bilioni 2.5, wengi wao (bilioni moja ni vijana) watapoteza usikivu. Kati yao, milioni 700 ni kutoka kusini mwa Jangwa la Sahara. Wanahitaji huduma ya utengefu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live