Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hospitali yenye viwango vya kidunia kujengwa Tanzania

MWIGULU ME Hospitali yenye viwango vya kidunia kujengwa Tanzania

Tue, 6 Aug 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Tanzania inatarajiwa kuwa miongoni mwa nchi tano za Afrika zitakazonufaika na ujenzi wa mradi mkubwa wa hospitali itakayokuwa na viwango vya dunia vya utoaji huduma za matibabu (African Medical Center of Excellence (AMCE).

Mradi huo unatekelezwa kupitia mradi unaotekelezwa na African Export-Import Bank (Afreximbank) kwa kushirikiana na Hospitali ya Chuo Kikuu cha King ya London, nchini Uingereza.

Taarifa ya Wizara ya Fedha ya Tanzania iliyotolewa jana Jumatatu, Agosti 5, 2024 imeeleza hayo yamesemwa na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kituo cha Umahili cha Kimatibabu, Abuja, Brian Deaver, wakati Waziri wa Fedha wa Tanzania, Dk Mwigulu Nchemba alipoongoza ujumbe wa Tanzania kutembelea ujenzi wa mradi wa aina hiyo, nje kidogo ya mji wa Abuja, nchini Nigeria.

Deaver amesema hospitali hiyo itakayokuwa na uwezo wa kulaza wagonjwa 500 kwa wakati mmoja, itatumia teknolojia ya kisasa ambayo haijawahi kutumika katika Bara la Afrika kwa ajili ya kutibu magonjwa ya saratani ya damu na selimundu.

Amesema hospitali hiyo pamoja na hospitali nyingine zitakazojengwa nchini Ghana, Kenya na Tanzania, zitatoa huduma mtambuka, ikiwemo uchunguzi, matibabu, tiba kwa njia ya nyuklia, upasuaji, huduma baada ya upasuaji na huduma nyingine zinazojulikana kitaalamu kama oncology, haematology na magonjwa ya moyo.

“Tunapotekeleza mradi huu tunalenga kutoa huduma bora za afya, kutoa mafunzo kwa wataalamu wa afya, kufanya utafiti, kutoa ajira, kudhibiti mahitaji ya matumizi ya fedha za kigeni hususani dola na kukuza utalii wa kimatibabu kwa nchi za Afrika,” amesema Deaver.

Wakizungumza baada ya kutembelea mradi huo unaotarajiwa kugharimu zaidi ya dola milioni 260 za Marekani, Waziri Mwigulu na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dk Natu Elmaanry Mwamba wamesema mradi huo wa mfano si tu utasaidia huduma za kimatibabu kwa wananchi, bali pia itakuwa sehemu ya utalii wa kimatibabu kwa watu kutembelea na kupata huduma hizo kutoka nje ya Tanzania.

Kwa upande wake, Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Nigeria, Judica Nagunwa amesema jitihada zinazofanywa na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan katika sekta ya uchumi na matibabu, umelenga kuimarisha afya za Watanzania na ubalozi wake utatumia kila fursa kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa manufaa ya Watanzania.

Afreximbank ni taasisi ya fedha ya kimataifa (Pan-African multilateral financial institution) yenye majukumu ya kutoa fedha na kuendeleza biashara kwenye nchi za Afrika.

Dk Nchemba ameongoza ujumbe wa Tanzania, akiwemo Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Dk Natu El-maamry Mwamba na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-Fedha na Mipango-Zanzibar, Aboud Hassan Mwinyi ambao wanashiriki mikutano ya nchi za Afrika (African Caucus Meetings), uliowashirikisha Mawaziri wa Fedha na Magavana wa Benki Kuu kutoka nchi wanachama wa Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).

Chanzo: www.tanzaniaweb.live