Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Biteko: Serikali itaboresha matibabu ya saratani

Biteko Asikitishwa Na Kusuasua Ujenzi Wa Laini Ya Umeme Tabora   Urambo Biteko: Serikali itaboresha matibabu ya saratani

Fri, 3 May 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amesema serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya utoaji wa huduma za saratani na vifaa tiba ili kutanua wigo wa huduma hizo kupatikana kwa urahisi.

Dkt. Biteko amesema hayo jana Mei 2, 2024 wakati akimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika uzinduzi wa kituo cha matibabu ya saratani cha Aga Khan, Jijini Dar es Salaam.

“Serikali yetu imejipanga kuboresha huduma za afya na kupambana na magonjwa yasiyoambukiza na mfano wa juhudi hizi ni serikali kutenga eneo kilipojengwa kituo hiki ambacho kimepanga kuhudumia wagonjwa 100 kwa siku kwa matibabu ya mionzi, wagonjwa 25 kwa siku kwa tiba za kemikali na wagonjwa 25 kwa siku kwa uchunguzi wa saratani na huduma za chanjo,” amesema Dkt. Biteko

Ameupongeza Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan (AKDN) kupitia Taasisi ya Huduma za Afya ya Aga Khan Tanzania kwa ushirikiano na Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) pamoja na Kituo cha Tiba Bugando (BMC) kwa kubuni mradi shirikishi kati ya sekta ya umma na sekta binafsi uitwao Mradi Mtambuka wa Saratani Tanzania (TCCP) ambao unaunga mkono juhudi za serikali katika kupambana na saratani.

Pamoja na pongezi hizo, Dkt. Biteko ametoa wito kwa taasisi mbalimbali za afya nchini kuhakikisha zinajikita pia kwenye kuzuia ugonjwa wa saratani kwa njia mbalimbali ikiwemo kutoa elimu ya afya na lishe kwani wataalamu wanaamini kuwa magonjwa hayo yanaweza kuepukika na hivyo kuepusha gharama kubwa zinazotumika kwenye matibabu.

Awali, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema kuwa changamoto ya saratani nchini ni kubwa ambapo kila mwaka kuna wagojwa wapya 40,000 huku vifo 27,000 vikitokea kila mwaka na kwamba saratani inayoongoza ni ya mlango wa kizazi.

Amempongeza Rais Samia kwa kutoa fedha kwa ajili ya mapambano dhidi ya saratani ikiwemo kuboresha miundombinu, kununua vifaa tiba vya kisasa huku mwaka huu akitoa shilingi bilioni 10 kwa ajili ya kusomesha madaktari bingwa na madaktari wabobezi kwenye masuala ya saratani.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati Tendaji ya Taasisi ya Huduma za Afya Aga Khan, Bi. Zahra Aga Khan amesema kujengwa kwa kituo hicho ni ushahidi wa namna Tanzania inavyopiga hatua kwenye sekta ya afya

Chanzo: www.tanzaniaweb.live