Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

MenuMichezo
Golf

Viwanja vya gofu ni balaa

Golf Viwanja vya gofu ni balaa

Tue, 3 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kwenye gofu bhana kuna vionjo tofauti kabisa na ni mchezo wenye vitu vya kuvutia, ukielezewa viwanja tu vitakufurahisha na kukufanya utamani kuucheza mchezo huo.

Ukifika kwa mara ya kwanza kwenye viwanja hivyo unaweza ukajiuliza vinatumikaje, kutokana na vitu ambavyo utakutana navyo.

Ili viitwe viwanja vya gofu ambavyo vinaweza vikatumika kwa kuchezea michuano mbalimbali lazima kuwepo na saini ya watu maalumu ambao wanatambulika na Chama cha Gofu cha Dunia.

Kwenye harakati za Mzuka wa Gofu, Mwanaspoti linakuchambulia kila maeneo ili kukufahamisha mchezo huo ulivyo, awamu hii imekuja na vijue viwanja vya gofu.

SIFA ZA KIWANJA

Kwanza sifa kubwa ya kiwanja cha gofu lazima kiwe na mashimo 18 mfano kuna baadhi ya viwanja vina mashimo tisa ambayo kisheria kwenye mashindano unatakiwa kurudia mara mbili ili kupata idadi ya mashimo 18.

Kiwanja cha gofu ambacho kitatumika katika mashindano lazima kikaguliwe na wachezaji wa kulipwa wa nchi husika ambao wakiridhika nacho watasaini kisha kupeleka ripoti kwenye chama cha dunia.

Mahojiano yaliyofanyika hivi karibuni baina ya Mwanaspoti na mchezaji wa kulipwa nchini, Rodrick John anaeleza.

“Mfano Tanzania ili kiwanja kitumike lazima wachezaji wote wa kulipwa tukikague, kisha tunasaini ndipo chama cha dunia kipitishe nje na hapo, mashindano hayawezi kufanyika kwenye kiwanja hicho,” anasema.

Je, unataka kujua kila shimo lina mita ngapi? Kiwanja namba moja kina mita 173, namba mbili mita 450, namba tatu 438, namba nne ni mita 309, namba tano ni mita 119, namba sita 408, namba saba ni mita 298, namba nane ni mita ni 432, namba tisa ni mita 169.

Namba 10 ni mita 175, namba 11 ni mita 344, namba 12 ni mita 336, namba 13 ni mita 361, namba 14 ni mita 331, namba 15 ni mita 198, namba 16 ni mita 391, namba 17 ni mita 395 na namba 18 ni mita 353.

VIZUIZI KWENYE VIWANJA

Kama hujawahi kufika kwenye viwanja vya gofu kwa mara ya kwanza unaweza ukadhani upo porini hivi, lakini itakuwa inakushangaza kuona viwanja ndani yake ambavyo ni visafi sana.

Je, unataka kujua miti ina kazi gani ndani ya viwanja vya gofu? kazi yake inataka mchezaji atumie akili kuupiga mpira kwenda kwenye shimo husika, kuhakikisha mpira haugusi miti, ambapo wakati mwingine mchezaji asipokuwa makini mpira unapotea.

Vizuizi vingine ni bunker (shimo la michanga), mifereji, kubwa zaidi kama kiwanja kina wanyama hawatakiwi kubugudhiwa, zaidi ya mchezaji kuwaepuka.

John anasema: “Mfano kuna viwanja vinaweza vikawa na ngedere wakichukua mpira huwezi kuwakimbiza unaacha kwani wamekutwa humo, vipo vingine watu wanakutana na chatu inabidi apishwe na siyo kumuua.”

Anaongeza: “Mchezaji anajua kiwanja gani ni dume, mfano kwa hapa Tanzania kiwanja kigumu ni cha Kili Gofu Arusha kile kina miti mingi, maji, lazima ubebe mipira mingi maana upigaji wako kama siyo makini unaweza ukaipoteza na usimalize mashindano na unakuwa umejiondoa mwenyewe.”

VIBENDERA VINA MAANA GANI

Huko kwenye gofu ni tofauti na soka kabisa, ambako vibendera vinaonyesha mwisho wa uwanja na pia pembeni yake mchezji anaweza akapiga penalti.

Kwenye gofu vibendera vinakupa ishara ya shimo lililopo, mfano ukikiona kibendera cheupe kinaonyesha shimo lipo mwanzoni kama anavyoendelea kusimulia John.

“Ukiona kibendera cha njano basi kinaonyesha shimo lipo kati, hivyo unakuwa unajua utumie fimbo gani ambayo inaweza ikafikia umbali huo na kibendera chekundu kinaonyesha shimo lipo mwisho, hivyo vibendera hivyo vina maana kubwa na vinatoa mwelekeo wa upigaji na wakati mwingine kujua utumie fimbo gani,” anasema.

KUNA AINA TATU ZA VIWANJA

Anavitaja kuna pale ambapo hadi mpira ufike shimoni inatakiwa upigwe mara tatu, ingawa watalamu zaidi wanaweza wakapiga mara mbili ndio wanaoingia kwenye rekodi za kipekee za dunia.

“Kuna par 4 hicho kiwanja mchezaji anatakiwa apige mara nne mpira kuingia shimon, hivyo hivyo na par 5 lazima ipigwe mipira mitano kuingia shimoni,” anasema.

Mchezaji Rajabu Idd Pembe ambaye ni nahodha wa gofu wa kulipwa nchini, anasema uwepo wa vikwazo uwanjani vinaleta akili kwa namna ya kufanya vizuri zaidi.

“Ndio maana duniani kuna wachezaji wenye rekodi za aina yake baada ya kuvuka vikwazo hivyo na wengine kupiga mipira chini ya malengo ya shimo, mfano par 5 unaweza ukakuta mtu kapiga mipira mitatu,” anasema.

Chanzo: Mwanaspoti