Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

MenuMichezo
Golf

Timu ya taifa gofu hata miaka 50 freshi tu

Taifa Golf Timu ya taifa gofu hata miaka 50 freshi tu

Tue, 21 Nov 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Inahitajika mchakato maalumu wa kuwaandaa vijana wa kuitumikia timu ya taifa ya gofu, ambao watanyakua mataji ya mashindano mbalimbali yanayofanyika kila mwaka nchi tofauti, kama wanavyozungumza wadau wa mchezo huo, wakitaka Tanzania iwe tishio dhidi ya wapinzani wao.

Kwa mara ya mwisho timu ya taifa ya wanaume kunyakua taji kubwa ilikuwa 2004 la mashindano ya Afrika Mashariki na Kati, yaliyofanyika jijini Arusha, iliundwa na wachezaji tisa kwa maana walikuwa wanatakiwa kucheza ni nane na mmoja wa akiba. Mwanaspoti kupitia Mzuka wa Gofu awamu hii limezungumza na wadau mbalimbali ili kujua kasi ya kunyakua mataji kwenye mchezo huo kwa timu ya wanaume upoje na mipango ya Shirikisho la Mchezo wa Gofu nchini (TGU) ipoje ya kuandaa timu za taifa zenye ushindani.

KIKOSI KILICHOCHUKUA UBINGWA 2004

Wachezaji ambao waliunda timu ya taifa ambayo ilichukua ubingwa huo 2004, nahodha mkuu alikuwa ni Adam Mohamza, msaidizi wake ni Shaban Omary, Orasi Morere, Mathias Julias, Emmanuel Juma, Hasara Vicent, Hassan Kadio, Philipo Mwakalobo na Fadhili Nkya, wakati kocha mkuu alikuwa ni Salim Mwanyenza na msaidizi wake alikuwa Mbwana Juma.

Kati ya hao walioendelea kucheza gofu hadi sasa ni Mohamza, Morere, Kadio na Nkya na siyo kucheza pekee na wanafundisha, wengine inaelezwa wamegeukia shughuli nyingine.

Mmoja wa wachezaji ambao walinyakua taji hiyo, Kadio anaeleza kwamba timu ya taifa ya gofu inachezwa na mchezaji wa umri wowote ili mradi awe na uwezo wa kuisaidia timu, ingawa anatamani Shirikisho la Gofu Tanzania (TGU), wawekeze zaidi kwa vijana kama zinavyofanya nchi zilizoendelea kama Afrika Kusini, Zimbabwe na kwingineko ambako wanawafundisha watoto tangu wakiwa shule.

“Timu ya taifa anaweza kucheza mchezaji hata wa miaka 50, ila kwa nchi za wenzetu ambao wanaendelea kwenye mchezo huo wanaandaa chipukizi ambao wanafanya vizuri, kutokana na maarifa wanayojengewa mfano Afrika Kusini kuna chuo cha mchezo huo ndio maana wapo juu, mtoto wa miaka 15 anaweza akamshinda hata Pro,” anasema na kuongeza;

“Kuna wakati tukikutana na timu ya taifa ya Afrika Kusini ya mwaka jana siyo ya mwaka huu tena wanakuwa na wachezaji chipukizi, sisi timu yetu wachezaji ndani ya miaka 10 ni wale wale, hivyo inaweza ikawa ngumu kunyakua mataji mengi, niliombe TGU kutafuta namna nzuri ya kuweka mfumo wa kuandaa timu ya taifa hasa kwa kukuza vipaji vya watoto.

“Angalau Lugalo naona inafanya bidii sana kwenye jambo hilo na Dar Gymkhana klabu, ambao kuna watu binafsi unaona wanawasaidia sana vijana kuinua vipaji vyao, ndio maana naona kuna haja TGU kuweka mfumo mahususi, naamini inawezekana na huko mbele Tanzania itakuwa tishio.” Anasema kwa sasa anacheza na kufundisha anatamani kuona vijana wengi wanafika mbali

“Ila pia ifahamike wachezaji wa ridhaa ndio wanaunda timu ya taifa na siyo maproo, hivyo nikitaka kuchezea inabidi niandike barua kwenye klabu ya kutani kurejea kwenye Amacha wao ndio watapeleka TGU, halafu unakaa mwaka mmoja nje bila kucheza mashindano kisha unarudishwa kucheza.”

Kwa upande wa Mwanyenza ambaye alifanikisha kikosi hicho kunyakua taji hilo anasema; “Najivunia kuwa na rekodi hiyo kwa nchi yangu, kati ya vijana waliokuwepo kwenye kikosi hicho ni Kadio na Nkya ambao bado wanacheza hilo ni jambo zuri zaidi, ila ninachoweza kusisitiza nguvu iwekwe kwa vijana ingawa ni mchezo usiyobagua umri.

“Anaweza akacheza hata mzee wa miaka 100 ili mradi awe na nguvu ya kutembea, kuona na uwezo wa kupiga na kuna mashindano kulingana na umri, ila jambo la msingi tunapaswa kuandaa vizazi vya gofu vya miaka ijayo.”

Anasema wakiandaliwa vijana wenye ujuzi anaamini wataleta mataji ya mashindano makubwa ya All African Game na ya duniani, kitu kikubwa ni elimu ya mchezo huo anatamani iendelee kutolewa kwa jamii, huku akilishukuru gazeti la Mwanaspoti kwa kuwa mstari wa mbele kuiandika mchezo huo.

“Niwaondoe hofu wazazi wapo wengi ambao wametoka familia za chini na sasa ni wachezaji wa gofu wazuri, wasizime ndoto za watoto kama wapo ambao wanapenda mchezo huo,” anasema. Mchezaji mwingine Pro ambaye alichangia kuhusiana na timu ya taifa Hamis Ally pia ni kocha, anasema alikuja kocha mzungu Charles Fallah ambaye kwa sasa ni marehemu alijaribu kuweka mfumo mzuri wa kuandaa vijana kwenye misingi mizuri.

“Matunda yake ni hao kina Victor Joseph (Dar Gymkhana) na Isihaka Daudi wa Lugalo hao ni zao la mzungu alianza kuwafundisha wakiwa wadogo sana na sasa ndio tegemeo la timu ya taifa na wanafanya vizuri sana,” anasema.Kwa upande wa Joseph anasema; “Tulifundishwa kwa kuingia darasani kisha tulipelekwa uwanjani kwa ajili ya vitendo, tulikuwa tukikosea tunachapwa fimbo, kwa mfumo ule angekuwa hadi sasa tungekuwa mbali na naamini tungekuwa na mataji mengi sana.”

RAIS WA TGU

Kwa upande wa Mwenyekiti wa TGU, Gilman Kasiga anasema nguvu kubwa ya chama hicho wanaipeleka kwa timu za vijana itakayofanya iweze kubeba mataji mengi.

Anasema mkakati waliouweka ni kuhakisha wanaanda timu mapema ya kushiriki mashindano ya ubingwa Afrika kwa timu za vijana nchini Afrika ya Kusini mwakani.

Anaongeza kuwa kupitia timu za vijana TGU inaweza ikapata timu ya gofu wakubwa itakayoweza kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa.

“Nchi za wenzetu kama Afrika Kusini imeendelea sana kwa upande wa vijana, mkakati wetu kama TGU ni kufanya mapinduzi makubwa kwa upande huo ili tupate wawakilishi wazuri mwakani,” anasema

Chanzo: Mwanaspoti