Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

MenuMichezo
Golf

Tanzania mguu sawa uenyeji Gofu Afrika

Gofu Pic Tanzania mguu sawa uenyeji Gofu Afrika

Sat, 20 Aug 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Kwa mara ya kwanza Tanzania itakuwa mwenyeji wa mashindano ya Gofu Afrika kwa wanawake'All Africa Challenge Trophy' yatakayofanyika nchini kwa siku tatu kuanzia Septemba 6.

Mashindano hayo yatashirikisha zaidi ya wachezaji 300 kutoka mataifa 24 ya Afrika, Tanzania ikiwakilishwa na bingwa mtetezi, Madina Iddi, Hawa Wanyence, Neema Olomi na Angel Eaton.

Rais wa Chama cha Gofu cha wanawake nchini (TLGU), Sophia Viggo amesema hii ni mara ya kwanza Tanzania kupata fursa ya kuwa mwenyeji wa mashindano hayo makubwa Afrika ambayo yatafanyika kwenye viwanja vya klabu ya Gymkhana, Dar es Salaam.

"Kupitia wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo na Baraza la Michezo (BMT), tumemuomba Rais Samia Suluhu Hassan kuwa mgeni rasmi, tunamtarajia kutufungulia mashindano haya," alisema Viggo.

Nchi zitakazochuana ni pamoja na Tanzania, Nigeria, Botswana, Malawi, Uganda, Togo, Rwanda, Zimbabwe, Afrika Kusini, Kenya, Namibia, Senegal, Ghana, Burkina Faso, Morocco, Tunisia, Mali, Zambia, Ivory Coast, Mauritius, Gabon, Misri, Sierra Leone na Cameroon.

Amesema wadhamini mbalimbali kama Serengeti Breweries Limited (SBL), Great Lakes, Pepsi, Oryx, Prima Afro, National Internet Data Centre (NIDC), Garda World, Mohamed Enterprises Tanzania Limited (METL), Wadsworth, Freight & Transport, Capital Finance Ltd, Cornerstone Solutions Ltd na Savvy Fm wamejitokeza kufanikisha mashindano hayo, ingawa bado wana uhitaji zaidi wa udhamini.

"Tunapaswa kuzigharamia timu shiriki, malazi, usafiri na chakula, hivyo tunahitaji sapoti zaidi, lakini pia timu yetu ambayo itaingia kambini mapema wiki ijayo na itafanya mazoezi kwa siku 10 chini ya makocha wawili, Rajabu Iddi na Geofrey," amesema.

Amesema washiriki kutoka nje ya nchi wanatarajiwa kuanza kuwasili Septemba 2, na watapata siku mbili za mazoezi kabla ya ufunguzi jioni ya Septemba 5.

“Tunatarajia kutetea kombe hili ambalo tulishinda katika mashindano yaliyopita yaliyofanyika nchini Ghana mwaka 2018 ambapo mwenzetu, Madina Idi, ambaye ni Katibu wa TLGU alikuwa mshindi wa jumla,” alisema na kuongeza kuwa mwaka 2020 mashindano hayo yalitakiwa kufanyika nchini Namibia lakini haikuwezekana kwa sababu ya uviko-19.

Katika hatua nyingine, Viggo amesema mara baada ya mashindano hayo, wamepanga kufanya mashindano mengine ya Tanzania Ladies Open yatakayofanyika Septemba, 10, 11 na 12, 2022 na yatatanguliwa na mazoezi Septemba 9, 2022.

“Haya ni mashindano ya Kitaifa lakini tuliamua kuunganisha na All Afrifa Challenge Trophy ili kuruhusu washiriki pia waweze kushindana katika Tanzania Ladies Open,” alisema na kuongeza kuwa itakuwa wiki nzima ya gofu,"

Chanzo: Mwanaspoti