Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

MenuMichezo
Golf

Sauzi wapindua meza Gofu Afrika, Tanzania yapiga hesabu fainali

Tanzania Golf Sauzi wapindua meza Gofu Afrika, Tanzania yapiga hesabu fainali

Thu, 8 Sep 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Wakati Afrika Kusini ikipindua meza na kuwa kinara katika mechi za raundi ya pili kwa mchezaji mmoja mmoja kwenye mashindano ya gofu ya wanawake ya All Africa Challenge Trophy 'AACT', Tanzania inapiga hesabu ya kubadili upepo huo katika mechi za raundi ya mwisho kesho.

Nyota wa Afrika Kusini, Gabrielle Venter ndiye amekuwa kinara katika raundi hiyo kwa kupiga mikwaju 72 akifuatiwa na 'ndugu' yake, Bobbi Brown aliyepiga 73 mchana huu.

Kwa mikwaju hiyo sasa, Afrika Kusini imepanda hadi nafasi ya kwanza kwenye msimamo huku Kenya ikiporomoka hadi nafasi ya tatu kwenye matokeo ya jumla.

Wenyeji Tanzania katika raundi hiyo imeongozwa na Angel Eaton aliyepiga mikwaju 75 sawa na Abir Taibi wa Morocco aliyemaliza kwenye nafasi ya nne nyuma ya 'ndugu' yake Rich Intisar aliyepiga mikwaju 74.

Hata hivyo, Morocco haijapanda kuipiku Tanzania katika matokeo ya jumla kutokana na rekodi ya matokeo yao ya raundi ya kwanza jana.

Mbali na Eaton ambaye katika raundi ya kwanza alipiga mikwaju 80, Mtanzania mwingine, Madina Iddi amemaliza wa saba akipiga mikwaju 78.

Nahodha wa Tanzania, Hawa Wanyenche katika raundi ya pili hakuwa na mchezo bora kama alivyocheza raundi ya kwanza alipokuwa kinara kwa kupiga mikwaji 69.

Katika raundi ya pili, Wanyenche amepiga mikwaju 79 na kumaliza wa 11 kwenye msimamo.

Kocha wa timu hiyo, Geofrey Leverian amesema wamepoteza shot tano kwa Afrika Kusini, lakini bado wana fursa ya kuwa bingwa wa mashindano hayo yanayoshirikisha mataifa 21.

"Tunajipanga kwenye mechi za mwisho kesho, tulianza vizuri raundi ya kwanza kwa kuongoza, kwenye raundi ya pili Afrika Kusini wametufunga shot tano na sasa wao ndiyo wanaongoza.

"Sisi pia tumewafunga Kenya shot tano na kuwashusha hadi nafasi ya tatu, lakini bado tuna nafasi kubwa ya kufanya vizuri kesho na kuwa mabingwa," amesema nahodha huyo wa zamani wa timu ya taifa.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz