Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

MenuMichezo
Golf

Huyu hapa nguli wa gofu Bongo

Nguli Gofu Huyu hapa nguli wa gofu Bongo

Thu, 5 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Alianza kucheza kabla ya Uhuru wa Tanganyika (sasa Tanzania Bara), hadi sasa bado anacheza japo si kwa kasi ile ile.

Enzi zake, ingekuwa ni kwenye soka, tungemfananisha na nyota kama Sunday Manara’Computer’ au Juma Pondamali ‘Mensah’ enzi wakiwa wamoto uwanjani, Salum Manyenza, nyota wa gofu nchini mwenye rekodi yake.

Japo mtaani, jina lake sio maarufu sana, lakini ukienda kwenye viunga vya klabu za gofu, hasa klabu yake ya muda mrefu ya Gymkana Dar es Salaam, utahadithiwa namna ‘kijana huyo wa zamani’ alivyo hatari kwenye gofu.

Anasema alianza kuipenda gofu akiwa mdogo kwa kuona kwa wakoloni, wakati ule nyumbani kwao ilikuwa ni jirani na klabu ya gofu ya Tanga.

Mwaka 1956 akiwa darasa la kwanza mkoani Tanga, alijikita kwenye gofu, lakini wakati huo akiwa ni mbeba begi (kedi) hapo ndipo safari yake ya kucheza gofu ilianzia.

MIAKA 80 BADO ANACHEZA

Licha ya umri mkubwa, legendari huyo ambaye ana miaka 80 mpaka sasa bado anacheza gofu, akiwa mmoja wa wanachama wa Klabu ya Gymkhana tangu katikati ya miaka ya 1970.

“Nilianza kama mbeba mabegi nikiwa kijana mdogo sana huko kwetu Tanga, wakati huo nipo darasa la kwanza na kiwanja hakikuwa mbali na nyumbani,” anasema Mwanyenza na kuongeza;

“Kila nilipotoka shule, nilikwenda moja kwa moja uwanjani na kuwabebea Wazungu mabegi kisha wananilipa na wazazi wangu hawakushangaa kuniona narudi na pesa.”

UJIRA WA SH 1.5

Japo leo hii, pesa hiyo haiwezi kununua chochote, Mwanyenza anasema akiwa kedi, alipenda tu kuwabebea Wazungu mabegi wakati wakicheza, hakuifanya bure kazi hiyo.

“Walinilipa shilingi moja na nusu wakati huo ilikuwa pesa nyingi ambayo inaweza kununua vitu vingi kama nyama, maziwa, chai na andazi.”

Anasema, alipohitimu masomo yake ya sekondari katika Shule ya Karimjee mkoani humo mwaka 1967 alikwenda Dar es Salaam kufanya kazi serikalini kama mkaguzi mwaka 1969 na ikawa rahisi kwake na kujiunga na klabu ya Gymkana 1970 akiendelea kuwa kedi.

“Wakati huo, kiingilio katika klabu hiyo ilikuwa Sh 100 na kila mwezi mwanachama alikuwa akilipa Sh 25 ambapo mwenyeji wake alikuwa baba yake mdogo.

“Mwaka 1977 nilianza kucheza klabuni hapo kama profesheni mpaka leo na wakati huo huo alikuwa akifundisha baadhi ya wachezaji.

REKODI ZAKE

Kama ingekuwa kwa mataifa yaliyoendelea duniani basi mkongwe huyo angejengewa sanamu lake mahali kwani ameweka rekodi kubwa nchini.

Mwaka 1983 Mwanyenza aliweka rekodi ya pekee kwa kupata grosi 57 katika kiwanja kilichokuwa katika saizi ya uwanja ‘lever’ 69 wakati huo na sehemu ya kumalizia ilikuwa ni ya mchanga ‘brown’.

Rekodi hiyo mpaka sasa haijawahi kufikiwa na mcheza gofu yeyote nchini.

Mkongwe huyo anasema katika maisha yake ya gofu hawezi kuisahahu rekodi hiyo kwenye Uwanja wa Dar Gymkhana.

“Kama ningepata grosi 56, naamini kuwa ningewekwa kwenye kumbukumbu ya Kitabu cha Guiness duniani,” anasema Mwanyenza na kuongeza;

“Kwa kweli nilihuzunika sana kucheza kwa kuharibu sehemu moja na kama ningecheza vizuri ningepata grosi 56, ambayo ingenifanya niwe mmoja wa watu mashuhuri walioingizwa kwenye kitabu hicho.”

REKODI YA MAMILIONI

Kwenye mashindano makubwa, rekodi kama hizi zinawekewa zawadi ya gari ya mamilioni ya pesa, japo kwa Mwanyenza, licha ya kuifikia rekodi hiyo mara nne, anasema wakati huo haikuwa na zawadi kama hizo.

“Ni zamani kidogo, hamasa kama hiyo haikuwepo,” anasema nyota huyo ambaye ana rekodi ya kupiga mpira na kuingia moja kwa moja kwenye shimo.

“Ni rekodi inayonipa heshima hadi sasa, nilipopiga mpira ukaingia moja kwa moja kwenye shimo “Hole- in one” ambao sio rahisi kwa mchezaji kufanya hivyo.

Anasema hakuishia kupiga mpira huo mara moja tu kwani aliendelea kufanya hivyo mara nne kwa miaka tofauti.

ALIANZA NA VIFAA VYA MITI

Anasema wakati wanaanza kuucheza mchezo huo walitumia fimbo za miti na hakukuwa na fimbo kama za sasa.

“Wenyewe Wazungu ndio walikuwa wanatumia fimbo za chuma sisi tulitumia miti kuupiga mpira na tulikuwa tunapatia tu kama wengine,” anasema mkongwe huyo.

Anaongeza hawakuwepo na wadhamani tofauti na sasa ambapo wadhamini wamekuwa wakijitokeza kudhamini mchezo wa gofu.

“Kuwepo kwa wadhamini nimeona idadi kubwa ya wachezaji kuongezeka na kadiri mashindano yanavyofanyika mabadiliko yanaonekana,” alisema Mwanyenza.

Hata hivyo, Mwanyenza aliupongeza uongozi wa chama cha gofu nchini (TGU) na wanawake (TLGU) kwa kazi kubwa wanayofanya ya kuendeleza mchezo huo hapa nchini.

KIMATAIFA YUMO

Sio tu nchini bali mkali huyo wa gofu aliwahi kutingisha sehemu mbalimbali na kuondoka na ushindi.

Ukiachana na mashindano ya Tanzania Open ambayo alishinda mara nne mfululizo mwaka 1972, 1973, 1974 na 1975.

Pia alishinda mashindano ya Kenya Open na kuondoka na makombe mara mbili mfululizo mwaka 1974/1975.

“Kipindi hicho watu walishangaa sana kubeba makombe yote hayo Kenya na hapa nchini na ni miongoni mwa mafanikio niliyoyapata,” anasema mwandamizi huyo

KUHUSU GOFU SENIOR

Alieleza namna gofu ilivyompa mashavu ya kutembea nchi mbalimbali ikiwemo Ufaransa na nyingine.

Alisema aliweza kufuzu kucheza mashindano ya gofu ya senior na kuwa mtanzania wa kwanza kushiriki mashindano ya British Open, kwenye viwanja vya Port Rush nchini Northern Highland mwaka 1998.

Anaongeza mashindano hayo yalifanyika Ufaransa katika maeneo ya Northern France ambayo yalishirikisha nchi mbalimbali ikiwemo Scotland.

“Nchi zilikuwa nyingi nakumbuka kulikuwa na England, Marekani, Norway, Japan, Sweden na Ufaransa.”

UBAGUZI

Wakati akiwa Sweden kwaajili ya mashindano ya Senior alitumiwa ujumbe na Balozi wa Tanzania nchini humo kuwa haruhusiwi kushiriki mashindano hayo.

Anasema baada ya kuletewa ujumbe huo hakushituka kwani kulikuwa na ubaguzi wa rangi uliokuwa unaendelea nchini humo.

Hata hivyo, anasema Tanzania ilikuwa haitakiwi kushiriki mashindano yoyote ambayo makaburu walishiriki jambo lilomfanya arudi nchini.

“Nilipoletewa ile memo sikushtuka kwasababu nilizisikia taarifa hizo za ubaguzi kwahiyo nilivyopewa ujumbe ule tu nikakusanya kila kilicho changu na kurudi zangu nchini,” anasema Mwanyenza

NI MTAALAMU WA VIWANJA

Mbali na kuwa na utaalamu wa kucheza gofu kwa muda mrefu lakini ni fundi wa kuelekeza kiwanja cha gofu kijengwe vipi.

Anasema kuna viwanja akatolea mfano Lugalo kilichopo Dar es Salaam alisaidia kuelekeza kijengwe vipi kuanzia kiwanja namba 1-9.

“Ukiachana na Lugalo kuna Serengeti, Dodoma na kimoja kipo Malawi nimewaelekeza namna ya kukijenga mfano kuanzia kiwanja namba 1-9 wakichongeje,” anasema mtalamu huyo.

FAMILIA

Mkongwe huyo ana watoto wanne wa kike wawili na wengine wa kiume wote hakuna hata mmoja aliyerithi kipaji chake. Hata hivyo baadhi ya wajukuu ndio wanapenda kucheza lakini bado hawajajaribu.

“Nilikuwa na mwanangu mmoja Mohamed alipenda soka lakini hakufanikiwa wajukuu zangu ndio wanapenda japo nao bado hawajajaribu,” anasema Mwanyenza.

GOFU YAMPA NYUMBA

Kupitia mchezo huo umemfanya ajenge nyumba iliyopo (Mwananyamala) na shamba lililopo Mkuranga.

USHAURI WAKE

Viongozi watengeneze viwanja ili wachezaji waongezeke. “Tanzania itapata wachezaji wengi watakaokuwa tegemeo kwa taifa la tofauti na sisi wakati tunacheza viwanja vilikuwa ni vichache,” anasema Mwanyenza.

Chanzo: Mwanaspoti