Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

MenuMichezo
Golf

Huku kwenye gofu usipochomekea unalo

Gofu Gofu Huku kwenye gofu usipochomekea unalo

Tue, 10 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kama angekuwa anacheza gofu, basi winga nyota wa Yanga, Maxi Nzengeli angefunika sana na kuwa ‘mkali’ wao kwani asingehusika kwenye adhabu hii ya kutochomekea kabisa kwenye mchezo huo.

Huko kwenye soka ni wachezaji wachache wenye nidhamu ya kuchomekea jezi zao ndani ya bukta, huku Maxi akiwa ndiye kubwa lao la kuvaa smati muda wote wa dakika 90 za pambano analokuwa uwanjani. Ni kama alivyokuwa akifanya Stephen Sey Kwame aliyewahi kuwika na Singida United, Namungo na Dodoma Jiji ambaye kwa sasa anacheza soka la kulipwa huko Libya.

Wawili hao ilikuwa ngumu kuwakuta uwanjani wakiwa hawajachomekea, tofauti na wanasoka wengi ambao baada tu ya kipyenga kupulizwa, huchomoa jezi, lakini winga huyo hana mpango huo, mwanzo mwisho utamkuta amechomekea.

Sasa ni kwamba kwenye gofu kuchomekea ni moja ya sheria inayowaadhibu wasioitii, hususani wachezaji wa kiume.

“Kwenye gofu hii ni sheria, unapoingia uwanjani hakuna anayekukumbusha kuchomekea, lakini ukikanyaga tu kiwanja namba moja ukiwa haujachomekea hata kama hujaanza kucheza adhab inakuhusu,” anasema nyota wa zamani wa timu ya taifa, Godfrey Leverian.

Anasema kwenye gofu, wanaume kuchomekea ni lazima, japo sheria hiyo ya mavazi haiwalengi wanawake ambao ni ruksa kucheza bila kuchomekea.

Kwa Nzengeli, gofu inamhusu kutokana na anavyojiweka nadhifu muda wote akiwa uwanjani, japo anacheza kandanda, lakini kwake kuchomekea ndiyo mpango mzima.

ADHABU YAKE NI HII

“Kote duniani, mwanamume hawezi kuingia uwanjani hajachomekea, kuna adhabu zake na ukikanyaga tu kwenye kiwanja namba moja, hata kama hujaanza kupiga mpira, ukaonekana hujachomekea hiyo ni penalti,” anasema.

Anasema, hakuna mchezaji anayekumbushwa kufanya hivyo, kitakachomkumbusha ni penalti atakayopigwa, ingawa ni nadra sana kumkuta mcheza gofu hajachomekea.

“Wanawake pekee ndiyo wanaruhusiwa kuingia hivi, wanaume ni kosa na lina adhabu zake, unapoingia bila kuchomekea, kama ilikuwa upige short ya kwanza, utaongezewa stroke zako utaanza kupiga short ya pili,” anasema.

Ikumbukwe, kwenye gofu aliyepiga short chache ndiye anayefanya vizuri, unapoongezewa short ya pili maana yake unajipunguzia nafasi ya kufanya vizuri.

“Kuchomekea ni moja ya sheria za mchezo wa gofu kote duniani, ni sheria za kimataifa na hakuna mtu wa kukukumbusha kuchomekea, kama mchezaji mwenyewe unapaswa kuishi kwenye misingi hiyo.”

KWA NINI WANAWAKE TU?

Anasema wanawake wanaruhusiwa kucheza bila kuchomekea kutokana na aina ya mavazi yao na ni utaratibu ambao uliwekwa hivyo.

“Wanawake wana mavazi yao, tofauti na wanaume, kundi hili pekee ndilo linaruhusiwa kuingia uwanjani kucheza bila kuchomekea, lakini kwa wanaume, kama nilivyosema na ukiingia tu uwanjani, hata kama ujaanza kucheza, hiyo inahesabika huko kwenye mchezo, kama hujachomekea adhabu yake inaanzia hapo.

“Utapigwa penalti, kisha utachomekea na kuendelea na mchezo, kwani hauwezi kuruhusiwa kucheza kiwanja namba mbili na kuendelea hadi 18 bia kuchomekea, adhabu itaanzia kiwanja namba moja,” anasema.

KWA NINI WANACHOMEKEA

Anasema vazi lolote la gofu linapaswa kuchomekea, mchezo huo ni wa watu smati, hivyo kuchomekea ilipitishwa ili kuzidi kufanya uwe nadhifu zaidi.

“Unapovaa fulana bila kuchomekea kwa mwanamume hakukufanyi uwe nadhifu uwanjani, umaridadi unapungua na gofu kama nilivyosema ni mchezo wa watu smati, kama haujachomekea unaonekana si nadhifu,” anasema.

Chanzo: Mwanaspoti