Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

MenuMichezo
Golf

Gulam Dewji na gofu damdamu

Gulam Dewji.jpeg Gulam Dewji na gofu damdamu

Tue, 13 Jun 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Zipo familia ambazo zimekuwa zikiipa kipaumbele kikubwa sekta ya michezo iwe kwa kushiriki kwa kucheza au kusapoti kwa kutoa fedha za kusaidia nyanja hiyo ipige hatua.

Lakini huwa ni nadra kuona familia moja inahusika moja kwa moja katika mambo hayo mawili kwenye michezo kwa maana ya kusapoti kwa fedha pamoja na kucheza.

Miongoni mwa familia chache ambazo zimeonyesha damu ya kupenda michezo kwa kusapoti kwa fedha, kuwemo katika uongozi lakini pia hata kucheza ni ile ya Dewji ambayo miongoni mwa wanaoiunda ni Mfanyabiashara tajiri zaidi Tanzania kwa mujibu wa mtandao wa Forbes, Mohammed Dewji 'MO'.

Hata hivyo wengi wanaitazama zaidi familia ya Dewji katika soka hasa pengine kwa kuwa mpira wa miguu ni mchezo ambao umekuwa ukifuatiliwa na kundi kubwa la watu nchini lakini pia ushabiki na sapoti yao ambayo wamekuwa wakiitoa kwa Simba ambayo ni miongoni mwa timu mbili kubwa za soka hapa nchini.

Chimbuko la familia ya Dewji kujikita katika soka hapana shaka ni kazi kubwa iliyofanywa na Mzee Gulamabbas Dewji ambaye ni baba mzazi wa MO Dewji ambaye ni miongoni mwa watu walioisapoti kwa kiasi kikubwa kifedha timu hiyo hasa katika miaka ya 1990.

Baadaye ni kama watoto wake walirithi ambapo MO Dewji akaja kuwa mfadhili na baadaye mwekezaji wa Simba wakati huo binti yake Fatema Dewji akawa mlezi wa timu ya wanawake ya Simba 'Simba Queens'. Lakini wakati wengi wakiifahamu zaidi familia ya Dewji kupitia soka, gofu ni mchezo mwingine ambao familia hiyo imekuwa ikishiriki tena kwa kucheza na imeonekana kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali. Mzee Gulam licha ya umri wake wa miaka 75 hivi sasa, ni miongoni mwa wacheza gofu ambao wamekuwa wakifanya vizuri katika mashindano mbalimbali ya mchezo huo akiwa ni mwanachama wa klabu ya Gymkhana iliyopo Dar es Salaam. Gazeti hili lilifunga safari hadi kwa Mzee Gulam ili kupata fursa ya kuhabarisha umma jinsi Mfanyabiashara huyo alivyo kiongozi wa mfano kwa wanafamilia wake katika ushiriki wao kwenye mchezo huo.

ALIKOANZIA GOFU Mzee Gulam anafichua, alianza kucheza gofu tangu alipokuwa kijana na hadi sasa anaendelea huku akisisitiza kuwa anafurahia kuufahamu.

"Nilianza kucheza gofu zamani kidogo lakini kipindi fulani hivi niliamua kuacha. Sijui hata nini kilinishawishi kufanya hivyo na nakiri kwamba nilifanya kosa kuacha kucheza.

"Niligundua nimefanya makosa kuacha nikaamua kurudi kucheza na nimeanza tena kucheza kama miaka 10 iliyopita," anafafanua Gulam.

Anasema kwamba jitihada zake ndio zilifanya auelewe mapema mchezo huo. "Nilianza kujifunza kwa kwenda 'range' na kisha 'course'. Na Mbwana Juma ndio mwalimu wangu wa kwanza kunifundisha," anafichua Mzee Gulam.

KILICHOMSHAWISHI Mzee Gulam Dewji anafichua sababu zilizopelekea aamue kucheza gofu tofauti na michezo mingine. "Sababu kuu iliyonishawishi kupenda na kucheza gofu ni kwamba ni mchezo 'safe' (salama) kucheza. Kuumia unapocheza gofu ni nadra sana. Na jambo la kufurahisha ni hata wazee wanacheza.

"Mimi nina miaka 75 na kuna wazee hadi wenye umri wa miaka 90 ambao wanacheza vizuri tu bila shida yoyote. Hakuna mchezo mwingine wowote tofauti na riadha ambao mtu anaweza kucheza akiwa hadi na miaka 85," anasema Mzee Gulam.

Mzee Dewji anaongezea kwa kutaja mahusiano mazuri na watu kama sababu nyingine iliyochangia kumshawishi acheze gofu.

"Inasaidia kujuana na watu tofauti, mnabadilishana mawazo na kufungua fursa nyingine. Hii ni kwa sababu kwenye gofu kuna muda wa kuzungumza tofauti na michezo mingine ambayo haikupi nafasi ya kuzungumza ukiwa unacheza," alisema Mzee Gulam.

Dewji anasema kwamba ushawishi huo ndio umepelekea hata wanafamilia wake wote wacheze gofu. "Namshukuru Mungu watoto na wajukuu wangu wote wamefuata nyayo kwa kucheza gofu. Ni mchezo mzuri na tuna furaha kuucheza," anasema.

MCHEZO WA KITAJIRI? Kumekuwa na dhana kwamba gofu ni mchezo unaochezwa na watu wenye uwezo kifedha na wale wanaotoka katika familia za kimasikini na duni hauwahusu. Hata hivyo, Mzee Gulam anawatoa wasiwasi watu wenye nia ya kucheza gofu na kuwataka wajifunze na ikiwezekana washiriki mashindano ya kimataifa.

"Nchi za nje huu ni mchezo wa matajiri lakini kwa hapa Tanzania haiko hivyo. Mtu akiwa na nia ya kucheza kuna msaada mkubwa wa kumuendeleza na naamini miaka mitano ijayo tutakuwa mbali zaidi.

"Na katika hili nitoe pongezi nyingi kwa klabu ya Lugalo. Wanasaidia sana vijana wasio na hela kucheza gofu. Wana program nzuri ya kusaidia vijana.

"Sapoti imekuwa kubwa na hata hizi timu ambazo zimekuwa zikienda kuiwakilisha nchi sio kama wana hela bali wanasapotiwa," alisema Mzee Gulam.

MATAJI KAMA YOTE Mzee Gulam anasema kwamba kucheza kwake mchezo huo kumemfanya apate mataji mengi ya mchezo huo jambo ambalo anasema ni la kufurahisha na linalompa heshima.

"Nimeshinda makombe yanafikia 40 kwa nyakati tofauti. Nimeyaweka nyumbani na hata ukihitaji naweza kukutumia picha au hata uje kuyaona," alisema Mzee Gulam.

CHANGAMOTO Gofu ni mchezo unaokabiliwa na changamoto kadhaa hapa nchini na Mzee Gulam anataja changamoto ambayo ikifanyiwa kazi itafanya mchezo huo kuipa heshima kubwa nchi.

"Changamoto kubwa ni kwamba tuna 'golf courses' (viwanja vya gofu) kidogo na vilivyopo havipo kwenye ubora ule unahitajika. Hata hivyo hilo halitukatishi tamaa," anasema Mzee Dewji.

MWANGA UNAONEKANA Mzee Gulam anatabiri kuwa Tanzania itafanya vyema zaidi katika mchezo huo kutokana na umahiri wa makocha na ujenzi wa viwanja.

"Vijana wengi wanaocheza gofu hivi sasa wanapata 'coaching' (mafunzo) nzuri na makocha wanajitolea sana kufundisha bila hata kutaka fedha nyingi. Fikra yangu tutakuwa na hali nzuri ya gofu siku za usoni.

"Jambo lingine la kufurahisha na kupongeza ni Rais wetu, Mama Samia Suluhu Hassan kuhimiza gofu kuchezwa. Chini yake serikali imepanga kujenga uwanja wa kisasa wa gofu kule Chamwino, Dodoma na Mbugani Serengeti. Hii inasaidia kuendeleza gofu na naamini baada ya miaka mitano tutakuwa mbali sana," anamalizia Mzee Dewji.

Chanzo: Mwanaspoti