Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

MenuMichezo
Golf

Asota miaka 16 akitafuta kuitwa timu ya Taifa

Miaka 16 Asota miaka 16 akitafuta kuitwa timu ya Taifa

Thu, 16 Nov 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Haikuwa rahisi kwa Victoria Elias siku ya kwanza alipoingia uwanjani kucheza na Balozi Erick Angaye. Anasema alipata hofu, lakini kiu na uchu wa kutaka kufanikiwa ndivyo vilimpa ujasiri.

“Nilipata hofu kucheza na balozi uwanja mmoja, lakini kwa kuwa gofu ni mchezo wa kirafiki unakukutanisha na mtu yeyote ile ilinipa ujasiri,” anasema mchezaji huyo.

Anasema kwenye gofu, imewahi kutokea amepangwa kucheza na watu bila kuwafahamu, lakini baada ya mashindano akaambiwa mpinzani wake uwanjani ni kiongozi mkubwa wa nchi hiyo.

“Imewahi kunitokea mara kadhaa, lakini kwa kuwa mnakutana na kukaa pamoja inakujengea ujasiri. Gofu ni mchezo ambao unakukutanisha na watu tofauti,” anasema.

ALIVYOKUTANA NA BRIGEDIA JENERALI ANGAYE

Vick kama ambavyo amezoeleka kuitwa uwanjani, anasema mara ya kwanza walikutana kwenye klabu za gofu na alipopangwa kucheza naye alipata hofu wakati huo akimfahamu kama balozi wa Nigeria nchini.

“Alikuwa ni balozi, baadaye ndipo akaja kuwa brigedia jenerali nchini kwao. Siyo huyo tu hata aliyewahi kuwa balozi wa Malawi hapa nchini, Kalino (Kondwa) naye nimecheza naye mara nyingi kwenye mashindano ya mwisho wa mwezi na mara nyingi mimi ndiye niliwafunga.”

MIAKA 16 AKISAKA NAFASI TIMU YA TAIFA

Miaka 16 ni umri wa mtoto kuzaliwa, kuanza elimu ya msingi hadi kuhitimu na kujiunga na sekondari. Kipindi chote hicho Vick anasema alikitumia kutafuta nafasi ya kuitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa.

“Ilikuwa ni 2007 katikati ambapo nilianza kuwa na ndoto ya kuwa mchezaji wa timu ya taifa. Nilipata maono hayo nikiwa kedi wa nyota wa Kenya, Dismas Indiza ambaye sasa anacheza profesheno,” anasema.

Anasema kuwa alikuwa kedi wake kwenye mashindano yaliyofanyika jijini Arusha mwanzoni mwa 2007 na kujikuta wakigombana na mchezaji huyo katikati ya mchezo na kuacha kuendelea kumkedi. “Niliacha begi lake na kuondoka. Baadaye jioni alinifuata klabuni na kuniomba msamaha. Kuanzia pale ndipo nilipata wazo la kuwa mchezaji tena wa timu ya taifa,” anasema.

Vick anasema, walitofautiana na mchezaji huyo baada ya kumpa maelekezo ambayo aliyapuuza na akapata shoti tofauti na alivyocheza awali.

“Ukiwa kedi kuna muda nawe unaweza kumuelekeza mtu unayemkedi. Niliona kuna vitu anakosea, nilimuelekeza hakuelewa, nikapata hasira na kuacha kumkedi.

“Nilimwambia tumeongoza mashindano yote. Siku ya mwisho namuelekeza ananipuuza na kapata shoti. Nilikuwa niko sahihi naye alijua alikosea na baadaye tulizungumza yakaisha, lakini alinipa wazo la kuwa mchezaji, sababu aliamini naweza.

“Nilitoka Arusha kuja Dar es Salaam kuanza maisha. Nilikwenda Klabu ya Lugalo kufanya kazi ya u-kedi, lakini nikiwa na lengo la kuwa mchezaji tu, hiyo ilikuwa ni katikati ya 2007,” anasema.

Nyota huyo anasema alitumia muda wake wa asubuhi kujifua katika mazoezi binafsi na mchana aliendelea na kibarua cha u-kedi klabuni hapo.

“Sasa nimeachana kabisa na ukedi. Ndoto yangu ya kuwa mchezaji wa timu ya taifa imetimia baada ya miaka 16 kupita.”

Anasema alianza kucheza Lugalo Open na kushiriki mara kadhaa mashidano ya Ladies Open ya ndani na nje ya nchi, lakini kipindi chote hakupata nafasi ya kuitwa timu ya taifa kwa kuwa hakuwa na vigezo.

“Ili uitwe timu ya taifa ilikuwa ni lazima ufanye vizuri kwenye mashindano makubwa ya Tanzania Ladies Open au Lugalo, Gymkhana na Arusha. Kwa kipindi hicho sikuwahi kushinda na sikukata tamaa,” anasema.

Mchezaji huyo anasema kuna mwaka alishinda Morogoro Ladies Open, lakini ni kipindi ambacho timu ya taifa haikuchaguliwa. Hata hivyo aliendelea kupambana hadi hivi karibuni aliposhinda Tanzania Ladies Open.

“Nilikuwa mshindi wa jumla kwa wanawake wote. Mashindano yaliwashirikisha wachezaji gofu kutoka Kenya na Uganda pia. Kwa mara ya kwanza ndoto yangu ya kuitwa nation team (timu ya taifa) ikatimia,” anasema.

“Sihitaji kubweteka naendelea kujifua kwa kuwa mwakani kuna mashindano ya All African Challenge wachezaji watatu ndiyo wataiwakilisha nchi. Naendelea kujifua ili niwe kwenye kikosi kitakachopeperusha bendera ya taifa, hiyo ndiyo ndoto yangu kubwa kwa sasa.”

GOFU YAMPA MTAJI

Usiwachukulie poa wanawake wanaofanya shughuli mbalimbali za michezo lakini tofauti kwa sababu ni sehemu ya kuendesha maisha.

Vick anasema kupitia gofu alipata mtaji wa kuanzisha biashara ya mashuka ambayo inamuongezea kipato kingine nje ya mchezo huo.

Akiwatia moyo wanawake, anasema alithubutu kuingia kwenye mchezo huo ambao umeweza kubadili maisha yake ya kiuchumi.

Anasema ameshiriki mashindano mengi ya ndani na nje ambayo yamempa zaidi ya mataji 30 na kujinyakulia zawadi nyingi zingine za matumizi ya nyumbani.

“Baadhi ya zawadi ni simu ya mkononi iPhone 14, tiketi ya ndege, Tv, friji, meza, redio, seti za vyombo yaani hivyo ni baadhi tu na vimenisaidia kwa matumizi ya nyumbani,” anasema Vick.

Anasema kupitia gofu imemfanya atembelee nchi mbalimbali kama Kenya, Namibia, Uganda, Zambia, Malawi, Rwanda na zimbambwe alikokwenda kushiriki mashindano ya Ladies Open.

Vicy ambaye kwa sasa ana handcup 4, anasema nafasi ya gofu kwa wanawake kwa sasa imeanza kukua ingawa siyo kwa kasi, akitofautisha na awali ulivyokuwa unaonekana mchezo kuwa wa kiume zaidi. “Fursa zinatafutwa zikipatikana zinapambaniwa. Sisi wenyewe tulithubutu hatukutaka kukaa nyumbani na kuishia kulialia, ndio maana tukaanza ukedi na sasa tunacheza hadi na mabalozi wakubwa ambao wanatufunza maisha ni nini,” anasema mchezaji huyo.

Anasema amejuana na watu mbalimbali ndani na nje ambao wengine wanaishi kama ndugu na wanasaidiana kwenye shida na raha. “Ni mchezo unaounganisha watu wanaoweza kubadilisha maisha ya wengine.”

Vipi kuhusu kutani kuwa pro, anasema: “Bado sijafikia kiwango cha 0 ndio napambana kwani kwa handcup 4 siwezi kuwa pro.”

Je unataka kujua nje na gofu anajishughulisha na nini? Anafunguka kwamba: “Nauza mashuka gredi A pamoja na mashati ya kiume, yote hayo napambana ili nipate maendeleo ya maisha yangu.”

Chanzo: Mwanaspoti