Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Zitto kaandika barua Benki ya Dunia ajibiwe kwa barua

98002 Zitto+pic Zitto kaandika barua Benki ya Dunia ajibiwe kwa barua

Fri, 6 Mar 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Naamini wapo Watanzania tena wengi tu ambao hawakupendezwa na hawakuunga mkono uamuzi wa Kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe kuandika barua Benki ya Dunia (WB) akitaka Tanzania isitishiwe mkopo wa masharti nafuu wa Dola 500 milioni zaidi ya Sh1.2 trilioni za Tanzania.

Pia naamini wapo wengine wengi tu ambao wanaamini uamuzi wa Zitto ambaye pia ni mbunge wa Kigoma Mjini ni sahihi na wa kuungwa mkono. Kwa wanaompinga wanalazimika kukubali jambo moja kwamba kwa uamuzi huo, Zitto hajafanya kosa lolote la jinai, ametumia uhuru wake wa kuamua jambo aliloona ni sahihi na halivunji sheria za nchi.

Hoja kinzani katika dunia ya sasa ni jambo lisiloepukika na kwa kuwa Zitto aliamua kuandika barua basi ingekuwa rahisi kwa wanaompinga nao kuandika barua kujibu hoja zake.

Taasisi aliyoiandikia barua Zitto inajulikana, watu aliowaandikia pia wanajulikana na hata hoja za barua yake zinajulikana, sasa ugumu wa kuijibu barua hiyo unatoka wapi? Inashangaza kwamba baadhi ya watu badala ya kujibu barua kwa barua au hoja kwa hoja wakaona njia sahihi ni kutoa vitisho.

Kibaya zaidi ni kwamba vitisho vinavyotolewa vimekwenda mbali kwa baadhi yao kumtishia uhai wake. Huku ni kushindwa kwa kiwango cha juu hasa katika demokrasia ya vyama vingi. Ikiwa kila anayetoa hoja ambayo haiungwi mkono na upande wa pili suluhisho lake ni kumtisha basi tutaingia katika dunia ya ajabu kwamba watu wote tuwe na fikra na misimamo inayofanana.

Zitto si kwamba anapinga Tanzania kupewa mkopo bali katika mkopo huo hataki matumizi yake yawabague watoto wa kike wanaopata ujauzito wakiwa shule. Hii hoja ya Zitto inajibika kwa maandishi na si vitisho.

Habari zinazohusiana na hii

Advertisement
Kwake hilo anaona ni ubaguzi, sasa ambaye haungani naye katika hoja hiyo alitakiwa kumpinga kuanzia hapo, iwe ni kwa kuandika barua kama alivyofanya Zitto au kutumia uwanja wowote kuonyesha jinsi gani hakubaliani na hoja za Zitto badala ya kumtisha kwa kauli ambazo zinaashiria kuishiwa hoja. Kuna wakati ni muhimu watu kutofautiana, kwani katika kutofautiana huko zinapotolewa hoja kinzani husaidia kupanua mawazo ya watu wengine lakini hilo litawezekana iwapo hoja zitajibiwa kwa hoja na si kama hivi tunavyoona hoja inajibiwa kwa watu kutishwa.

Sitaki kuamini kuwa hoja za Zitto hazijibiki au katika CCM hakuna watu wenye uwezo wa kumjibu Zitto lakini inashangaza baadhi ya watu ndani ya CCM kuamini kwamba njia sahihi ya kumjibu Zitto si kuandika barua na kuzichambua hoja zake kwa namna yoyote ile bali ni kumtisha. Pamoja na changamoto nyingi katika sekta ya elimu, Watanzania bila shaka wanatambua juhudi za Serikali, na katika hilo namba ziko wazi, haziongopi. Ukifuatilia takwimu za hivi karibuni za wanafunzi wanaomaliza darasa la saba na kujiunga na kidato cha kwanza utaliona hilo. Mfano wanafunzi waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza mwaka 2019, kati ya 733,103 waliofaulu, 133,747 walishindwa kuanza moja kwa moja kidato cha kwanza kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa. Kwa waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza mwaka 2020, kati ya 701,038 waliofaulu, 58,699 ndio waliokosa nafasi ya kuendelea kidato cha kwanza kutokana na upungufu wa vyumba vya madarasa.

Kwa hiyo idadi ya wanaokosa nafasi kwa uhaba wa madarasa imekuwa ikipungua kutoka 133,747 wa mwaka 2019 hadi 58,699 wa mwaka 2020.

Pengine fedha za WB zingeweza kulifanya tatizo la uhaba wa madarasa kuwa historia nchini pamoja na kupunguza changamoto nyingine na labda ndio maana kuna watu wamekuwa wakali kwa Zitto lakini hoja ya Zitto pia ni katika hiyo hiyo elimu, anataka hata wale wanaopata ujauzito nao wanakuwa huru kuendelea na masomo bila kubaguliwa. Ni haki ya kila Mtanzania kuamua kumpinga au kukubaliana na Zitto lakini tatizo ni pale mpingaji badala ya kuja na hoja anaona njia sahihi ni ya vitisho. Hapa ndipo tatizo linapoanzia. Ni kama ambavyo mimi siungi mkono hatua ya Zitto kuandika barua WB lakini naamini kwa uamuzi huo, Zitto hajavunja sheria yoyote kiasi cha kufikia hatua ya kutishwa. Kwangu nilidhani ingependeza mjadala wa watoto kupata mimba na kubaguliwa ungekuwa wa ndani, iwe bungeni au maeneo mengine na zaidi ya hilo ni kama ambavyo nimewahi kusema kwamba ingependeza zaidi kujadili msingi wa tatizo badala ya matokeo.

Msingi wa tatizo ni watoto wa shule kupata mimba, tunahitaji kutumia nguvu nyingi kuhakikisha watoto hawapati mimba, ikiwezekana hata kujifunza katika nchi ambazo tatizo hili ama halipo au lipo kwa kiwango kidogo.

Nasema hivyo kwa sababu watoto wa kike wanapopata mimba wengi hukata tamaa na kupoteza matumaini ya kuendelea na masomo lakini kibaya zaidi ni hata baadhi ya watu huwabagua, ubaguzi huanzia katika jamii zinazowazunguka kabla ya serikalini.

Desemba mwaka jana ofisa elimu mkoa wa Dodoma, Maria Lyimo akiwasilisha taarifa ya elimu kwa kamati ya ushauri mkoa alisema kwamba wanafunzi 304 wa shule za msingi na sekondari walipata mimba na kuacha masomo kuanzia Januari hadi Desemba 2019. Sitaki kuamini kwamba wanafunzi wote hawa watarudi darasa kuendelea na masomo kukiwa na fursa bali naamini wengi wao wameshachukua maamuzi mengine. Kwangu naona watu hawa kwanza nguvu inahitajika kuwapa matumaini ya kesho yao, kuhakikisha hawatengwi na jamii lakini pia kuhakikisha wanafunzi wengine hawapati mimba. Kwa mantiki hiyo WB watoe fedha wasitoe fedha tatizo la mimba kwa wanafunzi ni mzigo ambao unatakiwa kumalizwa na Watanzania wenyewe, aliyeandika barua WB na ambaye hajapenda kuandikwa kwa barua hiyo.

Nguvu nyingi zitumike katika tatizo hili, kwa walioamua kumtisha Zitto ni vyema sasa wakatumia nguvu hizo kuwatisha wanaume wanaowapa wanafunzi mimba ili waogope kwani hao ndio msingi wa tatizo.

Columnist: mwananchi.co.tz