Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Zilikuwa kampeni kwelikweli Monduli, Ukonga

17459 Kampeni+pic TanzaniaWeb

Sun, 16 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mshikemshike wa kampeni za ubunge katika majimbo ya Ukonga na Monduli unahitimishwa leo huku wagombea wa vyama vya siasa walioshiriki wakisubiri kesho kuvuna walichopanda.

Wagombea hao, wakiwamo wa CCM na Chadema walioonyesha kuwa na nguvu zaidi, wamekuwa katika mchuano mkali, wakifanya kampeni za kukamiana ili kunyakua majimbo hayo.

Ushindani wa wagombea hao umeongezwa nguvu na hoja kwamba wale wanaogombea kupitia CCM katika majimbo hayo, Julius Kalanga (Monduli) na Mwita Waitara (Ukonga), walikuwa wabunge wa majimbo hayo kupitia Chadema, wakajizulu na kuhama chama, kisha wakateuliwa kuwania tena ubunge.

Kutokana na mazingira hayo, CCM inapania kunyakua majimbo hayo huku Chadema nayo ikinuia kuyachukua tena na ndiyo maana kampeni zilikuwa za nguvu kila upande.

Pamoja na kuwapo vyama vingine kadhaa, CCM na Chadema ndivyo vinavyoonekana kuwa na nguvu na ambavyo vimetumia rasilimali watu na fedha katika kampeni ili kuongeza idadi ya kura kibindoni.

Ili kufanikisha nia yake, kila chama kimewatumia vigogo wake maarufu wakiwamo mawaziri wakuu wastaafu, Edward Lowassa na Frederick Sumaye kwa Chadema na Mizengo Pinda kwa CCM. Pia mawaziri kadhaa, wabunge na viongozi wengine wameshiriki kampeni hizo.

Monduli

Wakati CCM imewatumia mawaziri sita na wabunge zaidi ya 12 kusaka ushindi, Chadema kimewatumia viongozi wake wa kitaifa, Edward Lowassa na kiongozi wa vijana wa chama hicho (Bavicha), Patrick ole Sosopi.

Pia Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, Naibu Katibu mkuu (Zanzibar), Salimu Mwalimu na baadhi ya wabunge pia wameungana nao katuika wiki ya mwisho kuongeza nguvu.

Kampeni za CCM zilizinduliwa na makamu Mwenyekiti wa Taifa, Philip Mangula na kuendelezwa na timu ya kampeni iliyoongozwa na Naibu Waziri wa Elimu, William Ole Nasha.

Miongoni mwa mawaziri waliosaidia kampeni ni Jafo wa Tamisemi, Waziri wa Ardhi, William Lukuvi,

Waziri wa Nishati, Medard Kalemani, Naibu Waziri Mazingira, Mussa Sima na Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Jumaa Aweso.

Katika kampeni za Monduli hoja kubwa ambazo kila chama kilitaja kama kipaumbele ni kutatua migogoro ya ardhi na shida ya maji na pengine ndio maana ilibidi mawaziri husika wafike kutoa ufafanuzi wa hoja au kueleza mipango iliyopo.

Lakini pia vyama vya upinzani vilikuwa na hoja nyingine ya uminyaji demokrasia na pinga sababu za kurejea uchaguzi huo, vikisema ni kupoteza fedha za umma.

Vyama hivyo vya upinzani vikiongozwa na Chadema vilieleza kuwa kitendo cha Kalanga kujiuzulu ubunge na kujiunga na CCM na kugombea tena ni mchezo mchafu.

Lowassa katika kampeni zake alimtuhumu Kalanga kuwa alihama Chadema ili asaidiwe kulipa mkopo wa Sh600 milioni, madai ambayo Kalanga aliyakanusha na kufafanua kuwa alijiuzulu ili kulinda maslahi mapana ya Monduli kutowatenga wananchi na Serikali yao.

Katika kampeni yaliibuliwa madai kuwa Lowassa alikuwa mbioni kuhamia CCM, ambayo yalisababisha mtoto wa Lowassa, Fred apande jukwaani kuyajibu.

Kupitia kampeni hizo, migogoro kadhaa ya ardhi imetatuliwa, tatizo la vijiji 61 kutopata umeme limefanyiwa kazi, pia tatizo la maji limepatiwa ufumbuzi baada ya Serikali kueleza itatoa 1.2 bilioni.

Wakati vyama viwili vikigangamala kufanya kampeni, vyama vingine vidogo vya upinzani vimeshindwa kufanya kampeni za kutosha, tatizo kubwa likitajwa ni ukata.

Ukonga

Katika Jimbo la Ukonga wagombea na vyama vyao walikuwa wanarushiana maneno katika kampeni za wazi na chinichini, kwa kutumia hoja mahususi za maendeleo, ukaribu wa mgombea na ‘fedha’ pamoja na tuhuma za kununuliwa na ukabila.

Ukabila

Katika hatua za awali za kampeni CCM na Chadema vilikuwa vikijinasibu kipi kinakubalika zaidi miongoni mwa Wakurya ambao inaaminika wako wengi jimboni humo, tofauti na Monduli ambako wagombea wa vyama hivyo wote ni Wamasai, wanatoka kata moja na wote walikuwa kuwa madiwani.

Wakati CCM ikitamba kwa kumpata Waitara wa kabila hilo na kuonyesha ngoma za kabila hilo mfano katika eneo la Bombambili, Kivule; Chadema imekuwa ikidai mgombea huyo amewasaliti Wakurya wenzake waliosimama kidete kulinda kura zake hivyo hafai kuaminiwa tena.

Kuchafua na kusafisha

Katika kampeni hizo jambo lingine lililoibuka mara kwa mara ni Waitara na timu yake kutumia muda mwingi kufafanua sababu za kujiondoa Chadema na kuhamia CCM akisema alikuwa anaandamwa na viongozi wa Chadema.

Hata hivyo, Chadema nao wametumia muda mwingi kukanusha madai hayo na kumlaumu Waitara wakimtuhumu kuwa amehama chama baada ya kununuliwa.

Kutatua changamoto

Hoja kuu ya Waitara ni kushindwa kutimiza majukumu ya msingi kama kiongozi wa upinzani kutokana na Chadema (chama alichokuwa awali), kumzuia kukutana na viongozi wa CCM ambao ndiyo wana fedha za maendeleo.

Mbali na hayo ndiyo chama chenye mawaziri wenye dhamana ya fedha hizo, wakiwamo wanaohusika na umeme, maji, elimu na afya.

Akiwa katika mkutano katika eneo la Msongola na kwingineko, Waitara amekuwa akisema mara kadhaa kuwa miongoni mwa shida alizokuwa anapata ni viongozi wa chama chake kutokubali kuwa John Magufuli ndiye Rais.

Alisema bila kumuunga mkono Magufuli maendeleo kwa wanaukonga ingebaki kuwa ndoto ndiyo maana ameamua kuhamia huko.

Alisema “Nilikuwa nakatazwa hata kuonana na Mkuu wa Wilaya Sophia Mjema, Mkuu wa Mkoa Paul Makonda na Mawaziri wenye dhamana ya maji, umeme na afya,” alisema na kuongeza.

“Na nikifanya hivyo nitawekewa kikao, nitaonywa na kuitwa msaliti. Nitawaletea vipi maendeleo bila kuonana na wenye fedha na ilani ya kuongoza nchini hii,” amekuwa akihoji Waitara kwenye mikutano yake ya kampeni.

Pia anasema: “Nilikataa kuwa kenge, wakati wenzangu kwenye majimbo yao kuna umeme, maji na vituo vya afya, kwangu kuna kila aina ya changamoto.

“Niliamua kujiongeza kwa sababu nilizuiwa kuonana na wanaoweza kunisaidia kutatua changamoto jimboni kwangu, niliamua kuungana nao, kuliko kuharibikiwa,” amesema mara kadhaa Waitara.

Kauli hizo za Waitara mbali na kujibiwa mara kwa mara na washindani wake, zilipingwa na wengi wakiwamo wasomi na hata wanasiasa, waidai kuwa alikuwa na uwezo wa kuchochea maendeleo akiwa nje ya CCM.

Wagombea wa vyama vya CUF na Chadema pia walipinga kauli hiyo wakidai kuwa alikwenda CCM kwa tamaa zake na si kwa lengo la kutatua kero za wananchi.

Salama Masudi, mgombea CUF anasema endapo atapata ridhaa ya kuongoza wananchi wa Ukonga ataishinikiza Serikali kuleta maendeleo akiwa kulekule upinzani.

“Sitohama huku nilipo, nitashirikiana na Serikali nikiwa huku kuikumbusha kuwa wananchi wanataka maendeleo ambayo ni haki yao kwa sababu wanatozwa kodi.

“Kwangu hiyo ndiyo njia sahihi, sitawaacha njiani kwa tamaa ya chochote kile. Maendeleo ni haki yenu na inafahamika wazi,” anasema Masudi.

Mgombea huyo anasema ujenzi wa barabara, miradi ya umeme na maji, vyote vinafanyika kwa fedha ya kodi ya wananchi na siyo fedha za chama cha siasa, hivyo akiwa mbunge jukumu lake litakuwa ni kuwakumbusha wanaoshika madaraka kutekeleza miradi hiyo kadri awezavyo.

Kama ambavyo Masudi anafafanua, Waziri Mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye ambaye pia ni mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Pwani anasema Waitara akiwa CCM hawezi kuikosoa Serikali kwa lolote, bali lazima akubaliane nao.

Akimnadi mgombea wa Chadema, Asia Msangi Sumaye amesema mara kadhaa kuwa sehemu pekee ambayo mtu anaweza kuikosoa Serikali zaidi ya kuwa upande wa upinzani.

Sumaye anasema wanaohama upinzani kwa madai ya kwenda kuleta maendeleo, akiwamo Waitara si wakweli kwa sababu wakiwa CCM haitakuwa rahisi kwap kuibana Serikali.

Anafafanua kuwa duniani kote wapinzani ndiyo wanaichagiza Serikali kwaletea wananchi maendeleo, hivyo anayetoka huko kwa madai kama ya Waitara anawalaghai wananchi.

“Wananchi wa Ukonga kuweni makini na mtu huyu, anawalaghai, ameshindwa kuibana serikali akiwa upinzani akienda huko (CCM) ndiyo anazibwa mdomo kabisa,” anasema.

Lakini Katibu wa Itikadi na Uenezi wa (CCM) Humphrey Polepole anasisitiza kuwa Ukonga sasa “maendeleo yanakuja kama kukanyaga ganda la ndizi kwa sababu Waitara akipiga simu moja kwa Waziri mkuu inapokelewa.”

Mbali na Polepole, Mbunge wa Kisarawe na Waziri wa Tamisemi, Seleman Jafo amesema anamuhurumia Waitara kwa kushindwa kutatua changamoto za jimbo hilo kwa muda wa miaka miwili kutokana na kuwa “katika chama kisicho na ilani, amehamia CCM kupata maendeleo ya jimbo.”

Alijua akija CCM maendeleo yatakuwapo na kama mnavyoona tayari kuna vitu vimeanza kufanywa na bado baada ya uchaguzi huu barabara, madaraja na umeme yataanza kufanyiwa kazi kwa nguvu moja,” alisema Waziri Jafo.

Hoja hiyo ya kuwa karibu na ‘wenye fedha” inazungumzwa pia na Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde akisema matatizo ya wananchi wa Ukonga yatapata suluhisho iwapo watamchangua mbunge mwenye ‘connection’ (aliye karibu) na Serikali.

Kujiuzulu, kugombea tena

Hoja ya Waitara kujizulu ubunge na kuuwania tena nayo imekuwa sehemu ya kampeni, Ukonga na Monduli. Chadema inadai kuwa wananchi wanafanywa wajinga kwa kuletewa mtu waliyemchagua lakini akaamua kuachia ubunge mwenyewe, kisha anarudi kuomba kura.

CCM nao wamekuwa kuwa wananchi wanafanywa wajinga kwa sababu wanadanganywa kuwa changamoto zao zitatuliwa na watu wasiokuwa na dola, ambao hawana ilani ya chama wala fedha za kumaliza changamoto hizo.

Chama cha tatu hapo kinaibuka CUF, kinachosema wamezoea kuchezewa na vyama hivyo viwili, CCM na Chadema, kikitaka wananchi waviadhibu kwa kukipigia chenyewe kura.

“Watanzania, wanaukonga mmekuwa wajinga kiasi hiki? Mtu mlimchagua kwa kura nyingi hadi akawa miongoni mwa wabunge 10 waliopata kura nyingi. Akaondoka mwenyewe anarudi tena na kuwaomba mumchague!” anahoji Sumaye.

Wanawake kuelezwa wenye huruma

Vyama viwili kati ya vitatu vinavyofanya kampeni kwenye uchaguzi huo, Chadema na CUF vimesimamisha wagombea wanawake.

Chadema imemsimamisha Asia Msangi na CUF Salama Masudi, lakini CCM inategemea kura za wanawake zaidi ili iweze kupata ushindi.

Ni kutokana na nguvu hiyo, Katiba kampeni za chinichini chama hicho kimekuwa kinawakusanya akina mama na kuwapa ahadi tamutamu za mikopo katika vikundi.

Kaimu mwenyekiti wa CUF Wilaya ya Ilala, Hamisi Chambuso anasema kuwa Salama anafaa kwa sababu ni mwanamke ana huruma.

“Miongoni mwa changamoto nyingi zinazotajwa kwenye jimbo hili zinawahusu wanawake moja kwa moja ikiwamo maji, umeme na huduma bora za afya,” anasema Chambuso.

Akimnadi Msangi, Diwani wa Chadema Kata ya Kipawa Kenedy Simioni, anasema, “Mchagueni mwanamke ana huruma, hawezi kucheza na akili yenu kwa kuwasaliti, mmempa kura Waitara amewapuuza na kuhama chama kabisa, mpeni Msangi awatatulie changamoto zenu.”

Kampeni hizo zilishika kasi katika wiki ya lala salama ambapo mikutano kwa vyama vyote vitatu iliongezeka ambapo badala ya kufanya mkutano mmoja jioni walikuwa wakifanya mikutano miwili hadi mitatu.

Columnist: mwananchi.co.tz