Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Yapo matatizo manne ya viongozi vijana Tanzania

11378 Uongozi+pic TanzaniaWeb

Sat, 11 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kuna video iliwekwa kwenye mtandao wa YouTube, Machi 5, ikimwonesha mfanyabiashara tajiri mwenye asili ya Sudan, Mohammed Ibrahim ‘Mo’ katika jukwaa moja na viongozi mbalimbali wa Afrika.

Video hiyo imekuwa maarufu kwa sababu ya kile ambacho Mo Ibrahim anakisema. Mo ndiye Mwenyekiti wa Taasisi ya Mo Ibrahim Foundation, inayohamasisha utawala bora na wa sheria, ikiwemo kutoa tuzo kwa viongozi wakuu wastaafu Afrika wenye kuonyesha uongozi uliotukuka.

Mo alisema, Afrika ni bara la vijana kwa sababu idadi kubwa ya wakazi wake wana wastani wa umri wa miaka ya 20. Akasema, ukipiga hesabu wastani wa umri wa marais wa Afrika, utapata miaka 63 mpaka 64. Akaonyesha mshangao wake ni kwa nini vijana ambao ndiyo wenye bara lao hawaaminiwi na kupewa uongozi mkuu?

Alitolea mfano Marekani yenye uchumi wa dola 15-16 trilioni, kuwa iliweza kumchagua Mmarekani mwenye asili ya Afrika, Barack Obama kuwa Rais akiwa na umri wa miaka 46. Aliongeza kuwa Obama hakuwa Rais kijana zaidi Marekani, kwani Bill Clinton (Rais wa 42) na John Kennedy (Rais wa 35), walichaguliwa wakiwa vijana kuliko Obama.

Mo alihoji; ikiwa nchi yenye uchumi mkubwa, mitambo na silaha zenye nguvu ya kinyuklia, inawaamini vijana wenye umri wa miaka ya 40, kwa nini Afrika bara ambalo uchumi wa nchi zake ni jumla ya dola 3 trilioni, linashindwa kutoa fursa kwa vijana kuongoza?

Alisema, kama Obama angekuwa Kenya ambayo ni nchi asili ya baba yake, kwa umri wake pengine angefanya kazi ya udereva wa basi, lakini Marekani alichaguliwa kuwa Rais.

Mo alisema kwa hisia kuwa Afrika ndilo bara ambalo, kiongozi mwenye umri wa miaka ya 90, akiwa kwenye kiti cha magurudumu, na hawezi hata kupunga mkono kusalimia, lakini anagombea muhula mpya na anachaguliwa.

Aliposema maneno haya, ukumbi mzima uliangua kicheko, Mo akasema: “Ni sawa chekeni, mna haki ya kucheka, maana dunia nzima inatucheka. Hivi huu ni wehu?”

Tuulete mjadala nyumbani

Mo amechokonoa mjadala mzuri sana. Katika kuujadili na kuuchambua katika muktadha wa Kitanzania, naomba nichukue ripoti ya Taasisi ya Utafiti ya Gallup, Marekani, iliyotolewa Juni 4, 2015, ikiwa na kichwa; “Kipaji cha uongozi kinaadimika Kusini-Mashariki ya Asia.”

Ripoti hiyo ilieleza kuwa ndani ya nchi kumi zinazounda Chama cha Mataifa ya Kusini-Mashariki ya Asia (Asean); Brunei, Cambodia, Indonesia, Laos, Malaysia, Myanmar, Ufilipino, Singapore, Thailand na Vietnam, kipaji cha uongozi kimekuwa adimu. Ripoti hiyo ni kabla ya Mahathir Mohamad kuchaguliwa kuwa waziri mkuu wa Malaysia kwa mara ya pili, akiwa na umri wa miaka 93, Mei mwaka huu.

Ningekuwa kwenye kongamano hilo na Mo Ibrahim, kisha ningepewa nafasi ya kuzungumza baada yake, ningeshauri kabla ya kupigania vijana kuongoza mataifa yao, tuwaombe kwanza Gallup wafanye utafiti waje na majibu kuhusu uwepo wa kipaji cha uongozi kwa vijana wa Afrika.

Pengine tungepokea majibu yenye kuumiza kuliko nchi za Asia. Hapa nitaitumia Tanzania kama kielelezo cha kuadimika kwa kipaji cha uongozi wa vijana Afrika. Ni kwa sababu mazingira ya kisiasa na uongozi Afrika yanafanana, tena maeneo mengi hali ni mbaya kuliko Tanzania.

Kwa kutafsiri hali halisi ya Tanzania, tunaweza kuona matatizo katika mafungu manne yenye kuhusu kipaji cha uongozi wa vijana Afrika. Fungu la kwanza ni vijana wenye kujitokeza katika uongozi kuonyesha dhahiri kwamba hawana vipaji vya kuongoza. La pili ni vijana wenye vipaji kutojitokeza ili waonekane.

Fungu la tatu ni vijana wenyewe kutotambua njia za kuuelekea uongozi na kujipambanua kama viongozi, badala yake wanageuka wapambe wa viongozi wenye umri mkubwa. Matokeo yake hawadhihirishi vipaji vyao, bali wanakuwa wasifiaji na watetezi wa viongozi walioamua kuishi chini ya vivuli vyao.

Nne ni vijana kukosa maandalizi ya uongozi. Vyama vya siasa vimepoteza msingi wake wa kuchakata vipaji vipya vya uongozi kupitia jumuiya zao za vijana. Matokeo yake siku hizi viongozi wa jumuiya za vijana kwenye vyama, wamekuwa wakiropoka na kutoa matamshi ambayo si ya kiuongozi.

Tubaki kwenye msingi

Oktoba 2, 1920, Kiongozi wa zamani wa Urusi na Dola ya Sovieti (USSR), Vladimir Lenin, alihutubia Jumuiya ya Vijana wa Kikomunisti wa Urusi na kueleza kuwa majukumu ya jumuiya yoyote ile ya vijana, yanapaswa kuwekwa kwenye neno moja; Kujifunza.

Lenin ambaye jina lake ndilo ambalo limebeba falsafa za Kikomunisti za Leninism, aliwaambia vijana wa jumuiya hiyo kwa wakati huo kuwa pamoja na kila kitu, wanatakiwa kujifunza na kuziishi itikadi za kikomunisti ili waweze kuutetea ukomunisti dhidi ya ubepari.

Aya hizo mbili, zinatosha kutoa tafsiri ya kile ambacho Lenin alikisema, ni kwamba jumuiya za vijana zipo kwa ajili ya maandalizi ya vijana kuwa viongozi bora kupitia itikadi na falsafa ambazo wanapitishwa katika makuzi yao ya kiuongozi.

Mwaka 1944, mashujaa wa wakati wote wa Taifa la Afrika Kusini, Ashley Peter Mda, Walter Sisulu na Oliver Tambo, walipokuwa wanaanzisha Jumuiya ya Vijana ya ANC (ANC Youth League), walieleza malengo yake kuwa jumuiya hiyo ifanye kazi kama kiwanda cha kuchakata fikra za vijana ili wawe viongozi bora wa kizazi kipya.

Kwamba pamoja na shabaha ya ANC Youth League kuwaunganisha vijana na kuchochea hamasa yenye wigo mpana katika mapambano dhidi ya makaburu na utawala wao wa ubaguzi wa rangi, muhimu zaidi ni kuwaandaa kuwa viongozi wenye busara na wazalendo kwa nchi yao.

Kitabu kuhusu uanzishaji wa Jumuiya ya Vijana cha chama tawala cha Namibia, Swapo (Swapo Youth League), kinaeleza kuwa madhumuni yake ni kuwapika vijana kuwa wanajeshi imara wenye kujifunga mkanda kwa ajili ya kutetea itikadi za Swapo, vilevile kuwa viongozi wazuri nyakati zijazo.

Turudi kwenye tafsiri ya Lenin, ni kwamba palipo na kila jumuiya ya vijana, maana yake ni chuo cha mafunzo ambayo huwawezesha vijana kufuzu maono ambayo yanakuwa yamekusudiwa.

Hata Jumuiya ya Vijana ya Tanu na baadaye Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), shabaha yake ilikuwa ni kupika vijana kiitikadi, kiuongozi, vilevile kuwatengeneza kuwa wazalendo kwa nchi yao.

Hiyo ikawa sababu majukumu mengi yaliyokuwa yakitekelezwa na Tanu, wakati huo, kuingizwa kwenye mpango wa mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa wahitimu wa elimu ya kidato cha sita ili kuwajenga vijana kikakamavu, kuwa viongozi wazuri na wazalendo kwa taifa lao.

Kiongozi aliyeandaliwa

Sifa ya kwanza ya kiongozi aliyeandaliwa hupaswa kuwa na kauli thabiti. Kinachotoka kinywani hutakiwa kiwe na maana. Hutumia muda kutafakari anayotaka kuyasema.

Kiongozi aliyeandaliwa huwa hazungumzi kama mashine, kwamba maneno yanamtoka halafu baadaye ndiyo anajuta. Huyapima maneno yake katika nafasi ya uongozi, akiwa na tahadhari kuwa ulimi wake unaweza kujenga au kubomoa taifa.

Kijana aliyeandaliwa kiuongozi utamuona jinsi ambavyo anavyokuwa msikivu mwenzake anapozungumza, na anapopata nafasi anaitumia vizuri kujenga hoja zake. Pale anapoguswa anavumilia na anatoa ufafanuzi kwa wakati.

Utamtambua kiongozi aliyeandaliwa kwa jinsi ambavyo anazungumza utatuzi badala ya kulaumu. Kiongozi aliyeandaliwa huwa hajishughulishi na siasa za kutafuta upungufu wa upande wa pili ili autumie kujijenga, badala yake hushughulika na kuupambanua uzuri wake ili akubalike.

Pita mitandao ya kijamii hivi sasa, vijana wengi wanajikita katika kutafuta kasoro za upande mmoja ili wazitumie kujenga ngome zao. Kelele nyingi kwenye mitandao ya kijamii lakini si za kujijenga ni za kushambulia dosari za vyama pinzani.

Kijana aliyeandaliwa vizuri lazima awe anajiheshimu, anaheshimu wengine, anajiamini na uzalendo wake hautakiwi kutiliwa shaka. Kijana mzuri huwa hakimbilii kutaka kuongoza kabla hajafuzu vigezo vya uongozi.

Muhimu kupita yote, kijana anapaswa kuwa mkali kwa ustawi wa nchi yake, kwa amani na maendeleo, maana anaishi zaidi kuliko wazee, vilevile kijana ni daraja la watoto wake. Kijana kama kiongozi, hapaswi kuwa mpigadebe wa wazee wenye sura ya kuharibu nchi.

Janga la taifa tulilonalo ni kuwa kizazi cha vijana ambao hawajengi hoja kwa maslahi ya nchi, bali wanabishana kwa manufaa ya itikadi zao za kisiasa. Vijana wanaponzwa na viongozi wa vyama vyao ambao hawatarajiwi kuishi miaka mingi kama wao. Tukubali kuwa kweli vijana wanatakiwa kuongoza, lakini hawajaandaliwa. Wengi wanaonekana lakini hawaoneshi utulivu wa kiuongozi. Vijana wenye kumezwa na itikadi za vyama hawawezi kulifaa Taifa.

Columnist: mwananchi.co.tz